Tuesday, 27 August 2013

JE, NI FAIDA GANI?



Ev. C. Shijanga
JE, NI FAIDA GANI?

Kuna vitu vingi ambavyo hufanya maisha yakawepo au yakawezekana kwa hali ya kimwili; hapa utakuta vitu kama maji, hewa (oksijeni), chakula na nyumba na mavazi (ulinzi). Vitu hivi ndivyo wanadamu wengi huhangaikia sana, usiku na mchana kuvitafuta; utawakuta wakivitafuta kwa njia mbalimbali. Ukiwauliza wengi hasa vijana watakupa jibu rahisi tu, kwamba, "Tunatafuta maisha" sasa swali langu ni hili Je, hivi vitu wanavyovitafuta ndivyo maisha? Najua ni rahisi sana kujibu ndiyo kwa sababu kiuhalisia mtu akikosa vitu hivi hawezi kuendelea kuishi.
Swali lingine, Kama hivi vitu kweli ndivyo maisha, mbona watu bado wanakufa hali wakiwa navyo? Hujaona watu wakifa wakilazimishwa wale vyakula vingi walivyokuwa navyo?Hujaona matajiri kwa masikini wakifa? Kumbe maisha si tu kuwa na vitu hivi, ni lazima kuwe na vitu zaidi ya hivi. Hebu soma maneno ya mtu huyu na uuone mtazmo wake: Muhubiri 2:1-11

"1 Nikauambia moyo wangu, Haya, nitakujaribu kwa njia ya furaha basi ujifurahishe kwa anasa. Na tazama, hayo nayo yakawa ubatili.
 2 Nikasema juu ya kicheko, Ni wazimu; na juu ya furaha, Yafaa nini?
 3 Moyoni mwangu nikapeleleza jinsi ya kuuburudisha mwili kwa mvinyo, na (moyo wangu ukali ukiniongoza kwa hekima) jinsi ya kushikana na upumbavu, hata niyaone yaliyo mema ya kuwafaa wanadamu, ili wayafanye hayo chini ya mbingu siku zote za maisha yao.
 4 Nikajifanyizia kazi zilizo kubwa; nikajijengea nyumba; nikajipandia mashamba ya mizabibu;
 5 nikajifanyizia bustani na viunga, na kuipanda humo miti yenye matunda ya kila namna;
 6 nikajifanyizia birika za maji, ya kuunyweshea mwitu mlimopandwa miti michanga.
 7 Nami nikanunua watumwa na wajakazi, nikawa na wazalia nyumbani mwangu; tena nikawa na mali nyingi za ng'ombe na kondoo, kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu;
 8 tena nikajikusanyia fedha na dhahabu, na tunu za kifalme na za kutoka katika majimbo. Nikajipatia waimbaji, waume kwa wake, nao wale ambao wanadamu wanawatunuka, masuria wengi sana.
 9 Basi nikawa mkuu, nikaongezeka kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu; pia hekima yangu nikakaa nayo.
 10 Wala sikuyanyima macho yangu cho chote yalichokitamani; wala sikuuzuia moyo wangu katika furaha yo yote; maana moyo wangu ulifurahi kwa sababu ya kazi yangu yote, na hii ilikuwa sehemu yangu katika kazi yangu yote.

 11 Kisha nikaziangalia kazi zote zilizofanywa kwa mikono yangu, na taabu yote niliyotaabika katika kuzitenda; na tazama, yote ni ubatili na kujilisha upepo, wala faida hakuna chini ya jua."
Hebu uangalie tena mstari wa 11, na uyaone maneno haya, "......Na tazana yote ni ubatili na kujilisha upepo..........." Ikiwa umesoma vizuri maneno aliyoyasema mtu huyu hapo juu, utaona kwamba mtu huyu alijitahidi sana katika kutafuta vitu tulivyovisema pale juu. Hata hivyo mwisho anasema maneno ya ajabu, nilifikiri angeonyesha furaha kubwa kwamba amepata maisha, ila anasema, "yote ni ubatili na kujlisha upepo" 
Sasa ni nini nataka uone? Ninachotaka uone kikubwa ni kwamba kuwa tu na mali za dunia hii hakutoshi kama hujajua hatima ya maisha yako. Ni muhimu sana ukajua mwisho wa vitu hivi unavyohangaika kutafuta. Muhubiri yeye aliona, "yote ni ubatili na kujlisha upepo"  Je, wewe unaona nini? yote uliyohangaikia hadi sasa yanakupeleka wapi? Je, hivi vitu vina uwezo wa kuushikilia uhai wako hata lini?
Mark 8:36 Yesu akauliza, "Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?"  Naamini unaona jinsi watu wanavyoangamia kwa sababu ya mali walizonazo, nikuulize, Je, mtu akifa mali zake zinakuwa na msaada gani juu ya maisha yake? Kumbe mali na vitu vyote tunavyohangaikia ni vitu vya kupita tu. 1 Timothy 6:7 "Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu" Hii ni hakika na tumewazika wengi na kuona watu wengine wakiendelea kuvitumia walivyoviacha.
 Na Muh. 8:15, Inasema, "....kwa sababu mwanadamu hana neno lo lote lililo jema chini ya jua, kuliko kula, na kunywa, na kucheka;....."  Maneno haya bado yanazidi kusisitiza kwamba hivi vitu bado havitoshi kuyafanya maisha yetu yawezekane japo ni vya muhimu.
Katika, Rumi 14:17, Paulo anasema, "Maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu". Hapa Mtume Paulo anatuhamisha fikra na kutueleza habari za Ufalme wa Mungu. Na anasema huu ufalme si kula wala kunywa, bali ni haki, na amani na furaha ktk Roho Mtakatifu.
Katika Math. 6:33 Yesu anasema, "Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa." 
Sasa ufalme wa Mungu tunaupataje? Jibu ni rahisi tu, Ufalme wa Mungu hupatikana pale mtu anapompa Yesu nafasi, anapomkubali Yesu.
Yesu anapoingia ndani ya mtu anafanya maisha ya mtu kuwa safi kwa kuyasafisha kwa damu yake, hivyo kufanya ufalme wa Mungu katika utatu uchukue nafasi ndani yake, yaani: Mungu Baba, Mwana na Roho mtakatifu anakaa ndani yake. Vivyo hivyo pasipo Yesu haiwezekani kusafishwa dhambi, kumbuka Yesu alikuja ili azichukue dhambi na mizigo ya wanadamu. 

 Math. 1:21, "Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao". Naye anaita na kusema, "Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. (Math. 11:28). Katika mazingira haya naamini umekwisha kuona umuhimu wa mtu kuwa na Yesu katika maisha yake. Ziko faida nyingi anazozipata mtu anapokuwa na Yesu:



  • Unasamehewa dhambi. Isaya 1:18
  • Jina lako linaandikwa mbinguni. Ufunuo 20:15
  • Unatawala na kumiliki pamoja na Yesu 
  • Unafanyika kuwa mtoto wa Mungu.yoh. 1:12
  • Unapata nafasi katika makao ya milele. yoh. 14:1-6 
  • Roho wa Mungu anaingia ndani yako. 2tim.1:14
  • Unapata nguvu za Kumshinda shetani .1yoh 3:8
  • Unapata nguvu ya kutenda mema. Effes. 2:8-10
  • Pendo la Mungu linaingia ndani yako
  • Unapata nguvu za kumshinda shetani pamoja na dunia

Sasa ukiyakosa haya yote maisha yako yanakuwa na faida gani? Je, hayo siyo ubatili na kujilisha upepo? ni faida gani utapata? HAKIKA MAISHA BILA YESU NI HASARA, TENA HASARA KUBWA TU. MKUBALI YESU LEO MAISHA YAKO YAWE NA THAMANI.

Ukimaanisha kuokoka maombi haya yatakuwa yako:
Mungu uliye Hai uliyeumba vyote vinavyoonekana na visivyoonekana, asante kwa wema na fadhili zako, umenipenda hata ukanipa kuishi hadi leo, nakusihi kwa rehema zako unitazame na kwa damu ya Yesu unioshe dhambi zangu zote, natubu kwa yote niliyokosea tangu utoto wangu na kwa sasa nakubali kuanza safari mpya ya maisha pamoja nawe Yesu. AMEN

MWANAUME KWENYE NAFASI YA "MUME"

Mume ni mwanaume aliyeoa kwa kuzingatia vigezo na taratibu za kijamii, kishria na za kiroho. Mume si rafiki wa kiume (boyfriend), hawara, wa...

Powered By Blogger