Saturday, 14 November 2020

MAISHA YA UNYENYEKEVU NA TOBA

“Ingawa Bwana yuko juu, amwona mnyenyekevu, Naye amjua mwenye kujivuna tokea mbali” (Zaburi 138:6)

Unyenyekevu ni ile hali ya kukubali kuwa chini hata kama una sababu nzuri za kukaa juu. Ni kukubali kukaa chini ya mamlaka au kanuni au sheria au mfumo Fulani kwa nia ya kujenga. Mtu akikubali kukaa kwenye mamlaka ya Mungu, maana yake ni mnyenyekevu kwa Mungu. Katika hali ya ubinadamu, unyenyekevu umahusishwa sana na umaskini kwani mara nyingi mtu mwenye shida analazimika kujishusha kwa wale wenye navyo ili watoke kwenye shida. Kwenye mazingira ya kazi, wafanyakazi hulazimika kunyenyekea kwa mabosi wao ili waendelee kuwa na kazi; kwenye maswala ya kijeshi pia, wakuu hunyenyekewa na wale walio chini yao.

Unyenyekevu tunaojifunza hapa si huu unaosababishwa na mazingira; hapa tunaangalia unyenyekevu kama tabia ya mwamini inayosababishwa na usafi wa moyo. Hakuna mtu anayeweza kukaa na Mungu bila kuwa na tabia hii. Isaya 57:15 inasema, “Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu.”

Mtu mwenye kiburi na kujiinua hawezi kukaa na Mungu au kuwa juu au kufanikiwa. Mithali 29:23 inasema “Kiburi cha mtu kitamshusha; Bali mwenye roho ya unyenyekevu ataheshimiwe” Nimeona watu wengi wanyenyekevu wakipata heshima sana. Jifunze kwa watumishi wote waliofanikiwa katika Biblia utagundua kwamba hakuna hata mmoja aliyekuwa na kiburi, wote walikuwa wanyenyekevu Mungu akawainua. Hivyo ni lazima sisi kama waamini tujifunze unyenyekevu. Tuwe wanyenyekevu kwa Mungu na kwa watu wanaotuzunguka. Kimsingi, tuwe na maisha ya unyenyekevu.

Unyenyekevu una mambo mengi unafanya katika maisha yetu kama tulivyoona, yaani:

a.       Unatupa nafasi ya kupewa neema na Mungu. Mithali 3: 34 inasema, “Hakika yake huwadharau wenye dharau, Bali huwapa wanyenyekevu neema”

b.      Unatupa kuwa na uhusiano mzuri na wengine: Watu watakuheshimu, utakuwa na ujasiri kwa watu, Watu watakupenda Mithali 15:33 inatuambia, “Kumcha Bwana ni maonyo ya hekima; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu.” Kumbe hakuna heshima bila unyenyekevu kwanza.

c.       Faida kubwa zaidi ni kutupa kukaa na Mungu

 

Unyenyekevu unatupa kuhudumiana: Mtumishi wa Mungu Petro anatuambia, “…Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema. Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.” (1Petro 5:5-7) Unyenyekevu ndio chanzo cha kuinuka au kuinuliwa kwa mtu wa Mungu. Yeyote asiye mnyenyekevu hakika atapingwa na Mungu hata kushushwa chini.

Kunyenyekea chini ya mkono wa Mungu utasababisha Mungu atuinue kwa wakati wake. Neema ya Mungu ipo pamoja na wote wanaonyenyekea. Katika Mathayo 23:12 Yesu anasema, “Na ye yote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa.” Maisha ya kujinyenyekesha ndiyo maisha ya Mkristo. Yesu mwenyewe kama kielelezo chetu alijinyenyekesha hata mauti ya msalaba ndipo sisi tukainuliwa pamoja naye (Wafilipi 2:6-8) Neno linasema, “ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata” (Waebrania 5:8) Baada ya kunyenyekea alikirimiwa jina lipitalo majina yote (Wafilipi 2:9), tena ametufanyia wokovu wa milele hata akatajwa na Mungu kama kuhani mkuu kwa mfano wa Melikizedeki. (Waebrania 5:9)

Hebu tuuangazie macho mfano huu tunaoupata katika Luka 18:10 – 14: “Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru.Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”

Hapa tunaona jinsi ambavyo Farisayo alipata hasara kwa sababu ya kiburi, kujihesabia haki kwa kutimiza taratibu za dini. Yeye alijiona “si kama wengine” ni kweli hakuwa kama wengine lakini haikupasa iwe sababu ya kujihesabia haki. Tunapofanya vizuri au kutimiza majukumu Fulani katika kanisa Mungu anategemea tuendelee kunyenyekea na kuwathamini wengine. Mtoza ushuru yeye alijishusha, akakaa mbali kwa unyenyekevu (alipiga magoti) na kumwomba Mungu akimwambia “uniwie radhi mimi ni mwenye dhambi” Hii ndiyo siri ya kufanikiwa kwake. Mimi na wewe leo tunakwendaje mbele za Mungu? Tunawaonaje wengine ambao hawafanyi kwa viwango kama sisi?

Katika kitabu cha 1Samwel 2:3 tunakutana na maneno haya, “Msizidi kunena kwa kutakabari hivyo; Majivuno yasitoke vinywani mwenu; Kwa kuwa Bwana ni Mungu wa maarifa, Na matendo hupimwa na yeye kwa mizani.” Kumbe Mungu ndiye hupima matendo yetu, hatuna haja ya kujisifia kwayo. Tukiyabeba matendo yetu kama sababu ya kujihesabia haki tutajikuta tumebaki wenyewe, kwani hakuna hata tendo moja linalotosha kulipa gharama ya uhai wetu. Ni vema tukamwishia Mungu kwa unyenyekevu, na shukrani kwa yale aliyotuwezesha kufanya.

Mungu hawezi kumwacha mnyenyekevu: “Naye mnyenyekevu Mungu atamwokoa.” (Ayubu 22: 29). Hata kama unapita katika magumu kiasi gani, ukiendelea kunyenyekea mbele za Mungu kwa moyo uliopondeka hakika Mungu hatakuacha. Daudi alipoona ameanguka, hakuanza kujitetea. Alishuka akamlilia Mungu kwa kuyararua mavazi yake (ishara ya unyenyekevu), na Mungu akamsamehe. Kutenda dhambi kisha ukaficha na kujifanya mtakatifu si Ukristo huo, ni unafiki mbaya, ni kiburi. Ni vema ukajinyenyekesha ukaomba Mungu akusamehe, utakuwa salama.

Angalia mafanikio yasiufanye moyo wako ukainuka ukamsahau Mungu aliyekutoa kwenye utupu na kukubariki (Kumb. 8:11-14). Watu wengi huwa wanyenyekevu wakiwa hawana kitu ila wakifanikiwa wanapoteza heshima kwa Mungu na watumishi wake. Maisha yetu kama waamini hayapaswi kuwa hivi. Tunapaswa kuendelea kunyenyekea hata kama tutabarikiwa kwa kiasi gani. Mungu anataka tutafute pamoja naye, tumiliki pamoja naye, tutumie pamoja naye na tuendelee kuishi pamoja naye hata tukipoteza. Maisha ya Ayubu yanatufundisha somo la unyenyekevu mbele za Mungu.

Maisha baada ya kuokoka ni maisha ya unyenyekevu kwa Mungu, kwa viongozi wa kanisa, kwa watu wanaotuzunguka kulingana na Neno la Mungu. Ndani ya maisha ya wokovu tunapaswa kuwa na mioyo ya toba na unyenyekevu. Kila wakati tuhitaji rehema za Mungu, na kumtii Mungu kutoka moyoni. Tuwape heshima viongozi na kuwasikiliza katika mapenzi ya Mungu. Petro anaagiza na kusema, “ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.”

Unyenyekevu unatupa kuweza kuhudumiana: Katika kanisa sisi ni viungo, kila mmoja na mwenzake; hivyo hatuwezi kuepuka kuhudumiana. Katika unyenyekevu kila mmoja wetu akiwatanguliza wengine, tutahudumiana. Paulo anaeleza jinsi ambavyo amekuwa  “akimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote” (Matendo 20:19) Je, sisi tunatumika kwa jinsi gani? Nabii Sefania anasema, “Utafuteni unyenyekevu” (Sefania 2:3) Huwezi kuwa mhudumu ndani ya nyumba ya Mungu, na ukatumika kwa mafanikio, bila kuwa mnyenyekevu. Jifunze unyenyekevu. Paulo anahitimisha kwa kusema, “Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.” Wafilipi 2:3

 

No comments:

Post a Comment

MWANAUME KWENYE NAFASI YA "MUME"

Mume ni mwanaume aliyeoa kwa kuzingatia vigezo na taratibu za kijamii, kishria na za kiroho. Mume si rafiki wa kiume (boyfriend), hawara, wa...

Powered By Blogger