Saturday, 14 November 2020

KUOKOKA NI ZAIDI YA KUONGOKA

Watu wengi wanachanganya maana ya maneno haya kwa nia ya kutetea imani zao potofu.  Baada ya kulichambua kwa kina swala wokovu (kuokoka), hebu sasa tuone utofauti uliopo kati ya wokovu na swala la kuongoka. Baadhi ya madhehebu ya kikristo, hudai kwamba kuongoka ni sawa tu na kuokoka. Kiuhalisia haya ni maneno mawili tofauti kabisa katika Imani. Tukisema mtu ameongoka hatumaanishi ameokoka, japo kuna mazingira ambayo yanaweza kuleta maana hiyo. Hebu angalia tafsiri zifuatazo kutoka kwenye biblia ya Kingereza:

... declaring the CONVERSION of the Gentiles: and they caused great joy unto all the brethren (Acts 15:3 KJV) Kiswahili chake kinasema, wakitangaza habari za kuongoka kwao Mataifa; wakawafurahisha ndugu sana. Katika mazingira haya neno kuongoka linaweza kuwa na maana sawa na kuokoka kwa sababu wamataifa walitoka kwenye miungu yao na kugeuka kupitia Injili ya kweli iliyohubiriwa na Paulo na Barnaba.

But I have prayed especially for you [Peter], that your [own] faith may not fail; and when you yourself have turned again, strengthen and establish your brethren. (Luke 22:32 AMP) Mstari huohuo katika tafsiri nyingine unasomeka, But I have prayed for thee, that thy faith fail not: and when thou art converted, strengthen thy brethren. (Luke 22:32 KJV) Neno Conversion limetafsiriwa kama kubadili mfumo au matumizi ya kitu (kikawaida), ila kidini ni kule kubadili dini au Imani mfano kutoka Uislamu kwenda Ukristo.

 Katika mstari huu unaomzungumzia Petro, neno kuongoka limetafsiriwa kama to have turned again likimaanisha kujirudi au kurejea upya. Kwenye (KJV) – limeandikwa - art converted likiturudisha kwenye neno la kwenye Matendo 15:3. Katika Luka 22:32 Yesu anamwambia Petro “lakini nimekuombea wewe (Petro) ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.

Kwa hiyo neno kuongoka linaweza kuwa ni kule kuingia au kuhamia tu kwenye dini fulani, au kubadili imani (kutoka imani moja kwenda nyingine) bila kuleta maana sawa na neno kuokoka/kuokolewa (Saved) – linalomaanisha kutolewa kwenye maangamizo au hali ya uharibifu na kuwekwa kwenye usalama. Au kutolewa kwenye mauti (mshahara wa dhambi), nguvu za giza, na utumwa wa dhambi; na kuingizwa kwenye ufalme wa Mungu (maisha mapya ndani ya Kristo Yesu). Au kutengwa na dunia kwa ajili ya ufalme wa Mungu katika Kristo Yesu.

Kama tulivyoona kwamba kuokoka ni mpango wa Mungu wa kumtoa mwanadamu kwenye dhambi na mikono ya shetani (Mautini) na kumweka penye uzima (katika ufalme wake). Kuokoka ni zaidi ya kuongoka, mtu akiokoka maana yake amemwamini Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yake ila akiongoka anaweza kuwa amebadili tu msimamo au dini huku akiwa hajamkiri Yesu.

Kwa kifupi neno kuongoka ni neno la kidini, bali Kuokoka ni Imani kwa Mungu kupitia Yesu Kristo. Ndiyo maana Yesu hakututuma kuwahubiri watu habari za dini ili waongoke, bali habari za Ufalme wake (Injili) ili waamini na kubatizwa – waokoke. Marko 16:16 Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Kwa hiyo kuokoka ni zaidi ya kuongoka. Neno la kingereza linalotumika kwenye neno ataokoka si converted bali ni saved. Whoever believes and is baptized will be saved -  (Mark 16:16 NIV).

Wanafunzi wa Yesu (mitume) walipotumia neno kuongoka, inawezekana walimaanisha kuokoka kwa sababu watu walikuwa wanatoka kwenye dini ya kiyahudi au kwenye upagani au kwenye miungu yao na kuingia kwenye kanisa la Kristo ambapo hapakuwa na madhehebu kama ilivyo sasa. Kimsingi, kuingia kwenye dini si kuingia kwenye wokovu, japo ukishaingia kwenye wokovu ni lazima uwe na mahali pa kuabudu pamoja na waamini wenzako. Kuongoka kunakotokana na Injili ya kweli ya Yesu Kristo ndiko kuokoka.

Kazi iliyomtoa Yesu mbinguni na kuja duniani, hata kupata mateso ni kutafuta na kuokoa kile kilichopotea. Luka 19:10 inasema "Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea." Kuokoa ni kulipa gharama ya upotevu wa mtu. Yesu alifanyika fidia ya dhambi za wanadamu wote. Tunapotubu na kumwamini Yesu kama Mungu, na Bwana katika maisha Yetu tunaingia katika usalama wa milele. Neno linasema, "Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake (Wakolosai 1:13). Wokovu upo ndani yake Kristo.

No comments:

Post a Comment

MWANAUME KWENYE NAFASI YA "MUME"

Mume ni mwanaume aliyeoa kwa kuzingatia vigezo na taratibu za kijamii, kishria na za kiroho. Mume si rafiki wa kiume (boyfriend), hawara, wa...

Powered By Blogger