Saturday, 21 March 2020

MAARIFA YA MUNGU HULETA MAHUSINO MAZURI KATIKA FAMILIA


Maarifa ni uwezo wa kutumia ufahamu ili kusababisha mabadiliko au matokeo mazuri au mafanikio.  Unaweza ukawa ni ufahamu wa kiroho au ufahamu wa kawaida wa kibinadamu. Kuwa na ufahamu tu hakutoshi, bali ni lazima mtu aweze kuutumia huo ufahamu vizuri kwa ajili ya maisha ya kila siku. Chanzo cha maarifa yote ni uchaji mbele za Mungu (Mithali 1:7) Yaani kuwa na hofu ya Mungu kunakodhihirika katika ibada na utii katika neno lake. Katika maisha yetu yapo mengi yanayohitaji maarifa na hekima ya Mungu. Maarifa huleta hekima na hekima hutuwezesha kuishi vizuri na watu, hivyo kuwa na maisha ya furaha na amani.

Katika Muhubiri 11:8-9 Maandiko yanasema,

Naam, mtu akiishi miaka mingi, na aifurahie yote; lakini na azikumbuke siku zijazo za giza, kwa maana zitakuwa nyingi…..Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote Mungu atakuleta hukumuni.”

Katika mistari hii tunajifunza kwamba ni mpango wa Mungu tuifurahie miaka yote ya maisha yetu, ikiwepo miaka ya utoto, ujana, utu uzima na uzee. Swali langu ni kwamba, “Ni kwa nini vijana na watoto wengi wanaishi maisha ya huzuni, majuto, maumivu makali moyoni, migogoro, chuki, dhiki nk? Katika kutafakari nikagundua kwamba ipo shida kubwa kwenye mahusiano kati ya watoto/vijana na wazazi/walezi. Watoto wengi wamewaumiza wazazi/walezi wao kwa tabia zao mbaya za dharau na dhambi, kwa upande mwingine nao wazazi/walezi wamewaumiza watoto/vijana kwa kutotimiza wajibu wao na kuwatendea mabaya.

Tena katika Hosea 4:6 Mungu anasema, “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako.” Kukosa maarifa ya Mungu katika kujenga mahusiano ya kifamilia imekuwa ni tatizo kubwa kwa dunia, katika kizazi hiki. Kwa sababu hiyo shetani anazidi kuangamiza kizazi hiki kwa kasi sana.

Kwenye isaya Isaya 5:13 tunasoma matokeo mengine mabaya sana yanayoletwa na kukosa maarifa ya ki-Mungu, hapo tunasoma, “Kwa sababu hiyo watu wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa; na watu wao wenye cheo wana njaa, na wengi wao waona kiu sana.” Kumbe kwa kukosa maarifa ndipo tunaweza kuona jinsi ambavyo kizazi hiki kimeingia katika uteka wa Ibilisi kupitia mifumo ya kisasa ya maisha. Maeneo mengi watu wanalia kuhusu tabia za watoto wa kizazi hiki.

Wazazi/walezi wamekuwa na wakati mgumu sana katika malezi ya watoto wao. Hapa dawa ni Mungu aingilie kati, maombi na sala pamoja na kuwekeza kwenye kuwajaza maarifa ya Mungu ndilo suluhisho la kudumu. Uteka hauvunjiki kwa vikao na adhabu, au kutishiwa kufungwa gerezani; Mungu ndiye mwenye uwezo wa kuwaweka huru waliosetwa katika mateka ya Ibilisi.

Katika Luka 4:18 Yesu anasema, “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa” Watoto/vijana wetu wengi wanahitaji mguso wa Mungu watoke katika vifungo vilivyowafunga. Nimeshuhudia matukio mengi katika shule ambazo nimepita, watoto wengi watukutu wanakuwa wana uvamizi wa kipepo ndani yao, si wao katika hali ya kawaida. Kwa maombi yetu na jitihada zetu za kuwafundisha ili wajae maarifa ya kiMungu, ndivyo vitakavyoleta mapinduzi.

Shetani anashughulika kuwazuilia watoto/vijana maarifa ya Mungu ili apate kuwachota kwa urahisi kila siku. Katika Mithali 1:7, tunasoma,  “Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa” Ukiangalia katika kizazi hiki watoto na vijana wengi wamejaa mambo machafu sana, haya mambo ndiyo yanayochafua kabisa mahusiano na wazazi na kuwafanya watoto/vijana waingie kwenye uteka wa Ibilisi. Maswala ya mitandao yamechochea sana uasherati kwa kizazi hiki, siku hizi ni kawaida kukuta binti mdogo waa shule ya msingi ameshaanza maswala ya mapenzi.

Kwenye Mithali 1:28-29 tunaona matokeo mengine mabaya YA kuyakataa maarifa ya Mungu, Neno linasema, “Ndipo watakaponiita, lakini sitaitika; Watanitafuta kwa bidii, wasinione. Kwa kuwa walichukia maarifa, Wala hawakuchagua kumcha Bwana.” Hakuna mwanadamu asiyemwitaji Mungu katika mambo mbalimbali ya maisha yake. Hapa tunaona hali ya hatari inayojitokeza kizazi kinapokuwa na watu walioyakataa maarifa ya Mungu. Kwanza maombi hayatasikiwa na Mungu, pili, Mungu hawezi kuonekana wakati anahitajika. Hivyo ni lazima kila mtu akajua ana wajibu wa kutafuta maarifa ya Mungu ili kwa hayo tuweze kufanya mambo kwa hekima na ufahamu mzuri.

Wito wangu kwa wazazi, waalimu, viongozi, mitume, wachungaji, manabii, jamii na serikali ni kwamba kila mmoja aiangalie nafasi yake. Tuna jukumu la kuhakikisha kwamba watoto na vijana wetu wanazidi kupata maarifa ya Mungu,wanapoendelea kusoma katika elimu mbalimbali. Tusipuuze mambo ya Mungu; vipindi vya dini mashuleni vipewe nafasi yake. Watoto na vijana wasisitizwe kwenda kwenye nyumba za ibada. Vifaa vya kujifunzia elimu ya kiroho navyo vipatikane kwa wingi. Tena kila mmoja wetu awe mfano bora kwa watoto na vijana wetu. Vijana nao wawe tayari, na waamue kuwekeza muda wao katika kujifunza. Wawaheshimu viongozi na waalimu wa kiroho kama inavyowapasa. Hili litadumisha mahusiano kati yao na Mungu, kisha kati yao na wazazi/walezi.

Mungu awabariki,

Mwl. Stephen Swai
Simu: +255713511544

No comments:

Post a Comment

MWANAUME KWENYE NAFASI YA "MUME"

Mume ni mwanaume aliyeoa kwa kuzingatia vigezo na taratibu za kijamii, kishria na za kiroho. Mume si rafiki wa kiume (boyfriend), hawara, wa...

Powered By Blogger