SIKU YA HUKUMU,
KILA MMOJA ATATOA HESABU YA UTUMISHI WAKE.
(Each of us will
give an account of oneself on the Day of Judgment)
“Iangalie sana huduma ile uliyopewa katika Bwana, ili uitimize.
(Wakolosai 4:17).
Huduma katika
kanisa la Mungu ni kazi ya kila kiungo. Japo vipo viungo vilivyopewa heshima
zaidi ya vingine. Paulo anasema, “Basi katika nyumba kubwa havimo vyombo vya
dhahabu na fedha tu, bali na vya mti, na vya udongo; vingine vina heshima,
vingine havina.” (2 Timotheo 2:20) Vyombo vyote hivi havikujileta vyenyewe
ndani, vililetwa na mwenye nyumba akiwa na kusudi kwa kila kimoja. Vya dhahabu
japo ni vya thamani zaidi ya vingine havitatumika maeneo yote; kuna maeneo
tunahitaji vya udongo, kwingine vya mti au vya fedha. Mwenye nyumba ndiye
anayejua thamani na matumizi ya kila kimoja.
Ndivyo ilivyo
kwa kanisa la Mungu; kila aliyeokoka ni chombo na ameitwa kwa jinsi yake.
Anaweza akawa chombo cha dhahabu (wenye karama na vipawa zaidi), au cha fedha
(Wenye wito Fulani), au cha mti au cha udongo (washirika na wenye karama
zinazoonekana kibinaadamu kwamba hazina thamani). Sijui mimi na wewe ni vyombo
vya aina gani, ila ninachojua ni kwamba sote tu vyombo vya Bwana. Katika kitabu
cha Warumi 4:08 Paulo anatueleza juu ya kitu alichokifanya Yesu alipoinuliwa:
anasema, “Alipopaa juu aliteka mateka, Akawapa
wanadamu vipawa.” Kisha akavitaja: “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na
wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa
wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi
ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe”
Hapa
neno linatuweka wazi kwamba kusudi la Mungu kuwapa watu vipawa ni ‘kazi ya
huduma itendeke na mwili wa Kristo (kanisa) ujengwe” Hili ndilo lengo kuu,
hivyo mtumishi yeyote anayefanya kinyume na hayo ni mharibifu. Kama amekuwa
kwazo kwenye kazi ya huduma au anaubomoa mwili wa Kristo (kanisa) huyo ni
mchungaji au mtumishi aliyepoteza sifa kabisa. Sifa mojawapo ya mtumishi ni
kuwa mtendakazi mwenye uchungu na kondoo (kazi). Ni lazima aone wale kondoo
(watu) anaowatumikia kama mali yake (japo si mali yake). Awapende na awatumikie
kwa upendo.
Warumi
12:4-14
Kwa
kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote
havitendi kazi moja; Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika
Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake. Basi kwa kuwa tuna karama zilizo
mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa
kadiri ya imani; ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha,
katika kufundisha kwake; mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu,
kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu, kwa furaha. Pendo
na lisiwe na unafiki lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema. Kwa
pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu; kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana;
kwa tumaini, mkifurahi; katika dhiki, mkisubiri; katika kusali, mkidumu; kwa
mahitaji ya watakatifu, mkifuata ukarimu; katika kukaribisha wageni
mkijitahidi. Wabarikini wanaowaudhi; barikini, wala msilaani.
Mistari
hii inatuweka wazi zaidi juu ya utofauti wetu katika kazi ya Mungu na jinsi
ambayo tunaweza kuzitumia tofauti hizo kutumikiana kwa utukufu wa Mungu. Paulo
anasema ‘sisi ni kama viungo katika mwili’ na tunapaswa kufanya kazi katika
pendo lisilo na unafiki, tena kwa bidii tukiwatanguliza wengine. Mtumishi wa
Mungu anapokwenda kinyume na kanuni hizi alizoziweka Mungu, moja kwa moja
anakuwa mharibifu. Ona Paulo anavyosema tena: “ili kusiwe na faraka
katika mwili, bali viungo vitunzane kila kiungo
na mwenziwe.” (1 Wakorintho 12:25)
Kila
mtumishi aliyeitwa na Mungu haijalishi ni mtume au nabii au mchungaji au
mwinjilisti au mwimbaji au mwingine yeyote, ni kiungo kimoja katika mwili wenye
viungo vingi. Ni chombo miongoni mwa vyombo vingine. Ni (mtumishi) mtumwa wa
Kristo miongoni mwa watumishi wengine. Paulo anasema tena, “Basi uvueni uongo,
mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo
cha wenzake. (Waefeso 4:25). Kwa hiyo hakuna jinsi ambavyo mtumishi awaye yote
anaweza kudai kwamba yeye yuko juu ya wengine au mkuu kuliko wengine; akifanya
hivyo anakuwa mharibifu.
Kwa utangulizi huu mfupi nasimama kwa
ujasiri wote kukuambia wewe mtumishi mharibifu: Ole wako, tena narudia Ole
wako, usipotubu na kugeuka Ole wako. Yeremia alitabiri akasema, “Ole wao wachungaji, wanaoharibu kondoo za malisho
yangu na kuwatawanya! Asema Bwana.” (Yeremia 23:1) Hapa Mungu alikuwa anazungumza
juu ya watu wake Israeli. Na mimi juu ya kanisa la Kristo niseme, “Ole wako
mchungaji au mtumishi yeyote unayewaharibu kondoo wa malisho ya Mungu (kanisa)
na kuwatawanya! Utakuja kutoa hesabu. Usijitie moyo kama sifa unazopewa na
watu, usifurahie kusanyiko kubwa linalokujia, usiangalie hiyo fedha ya aibu
unayojikusanyia ukajiona mjanja! Kiburi chako kitashushwa hakika! Hata
ukiharibu sasa, hautaharibu milele. Geukaaa!
- Wewe unayefundisha mafundisho ya uongo ili kujikusanyia watu kwa hila:
Ole wako!
- Wewe unayeshika mapokeo ya dini na kuikataa kweli ya Mungu: Ole wako!
- -
Wewe unayejiita nabii wa Mungu huku ukijua kuwa wewe ni mchawi na
mshirikina: Ole wako!
- -
Wewe unayewadanganya watu wa Mungu na kujikusanyia fedha ili
kujishibisha mwenywe badala ya kuujenga mwili wa Kristo: Ole wako!
- -
Wewe uliyegeuza nyumba ya Mungu kuwa pango la wanyang’anyi kwa kuuza
kipawa cha Mungu: Ole wako!
- -
Wewe unayefanya mzaha na kazi ya Mungu, na kuwavunja wengine moyo, na
umeshupaza shingo ukijifaanya husikii maonyo: Ole wako!
- -
Wewe uliyejiinua juu na kujipa utukufu mwenyewe, ukilitangaza jina lako
kuliko jina la Yesu: Ole wako! Mungu atakapokuangusha, hutainuka tena.
- -
Wewe unayelichezea Neno la Mungu, kwa kulichanganya na uongo,
ukiwafurahisha watu kwa unafiki, utaunywa uchungu wa unafiki wako: Ole wako!
- -
Wewe unayejiita Mkuu, na kujipa majina makubwa, huku ukiwanyanyasa watu,
na kuwalaghai, kazi yako inanuka mbele za Mungu, hutafika mbali: Ole wako usipogeuka
na kutubu.
- -
Wewe unayejisumbukia huku ukivutwa na tamaa ya mali, tamaa ya mwili na
kiburi cha uzima, na kusahau wito ulioitiwa, mali zimekuwa Mungu wako, umekataa
kumtii Mungu kwa sababu ya tumbo: Ole wako!
- -
Yesu anasema, “Hakuja kuleta amani duniani, alikuja kuleta upanga! Wewe
nabii unapata wapi amani ya kujistarehesha na anasa, kula na makahaba na
wazinzi, umepata wapi nafasi hiyo! Ole wako!
- -
Ole wako unayelinajisi kanisa la Mungu kwa uzinzi na uasherati, jina
lako linanuka mbele za Mungu. Unazini na wale unaowatumikia, Ole wako!
- -
Ole wako mchungaji mvivu na mzembe, unaowaacha kondoo wakitaabika; na
wewe unazurura mitaani kutafuta mali, hakika utatoa hesabu.
- -
Kazi ya Mungu inafanyika kwa mazoea, mizaha imepanda mpaka madhabahuni,
uhuni umejaa, ukahaba umelitawala kanisa na wachungaji mmenyamaza: Ole wenu!
- -
Heri yao waliokubali kuonekana wabaya, wakapiga kelele juu ya ukahaba!
Kanisa la Mungu limechubuka, linavuja damu. Wachungaji wanachekelea mapato, na
kujenga majumba makubwa! Huu ni msiba, manabii wa kweli mko wapii? Mitume mko
wapi? Waalimu mbona mmenyamaza? Wainjilisti hamwoni shetani akikokota roho za
watu Jehanamu? Waimbaji mnaimba nini? Ni nani aliyewaita? Baba yenu ni nani?
- -
Heri yako wewe ulichagua kufa kwa ajili ya Haki, heri yako uliyeamua
kubaki maskini wa mali huku ukiihubiri kweli ukimngoja Mungu akukweze kwa
wakati wake. Ujapokuwa maskini, unawatajirisha wengi katika ufalme wa Mungu.
- -
Heri yako unayelia juu ya uharibifu unaoendelea juu ya dunia; heri yako
ambaye moyo wako umeja huruma unapowatazama wajane, mayatima, maskini, wenye
njaa, omba omba barabarani, wakimbizi, wafungwa, wagonjwa na wanaoteseka katika
dhambi; Mungu wetu ni mwenye huruma, hakika atakukumuka.
Huu si wakati wa
kutafuta umaarufu, si wakati wa kufanya maigizo madhabahuni, si wakati wa
kutafuta vyeo, si wakati wa kung’ang’ania madhehebu, si wakati wa kupasuka
pasuka na kujitenga na wengine, si wakati wa kuoneana wivu, si wakati wa
kugombana watumishi, si wakati wa kujiona bora kuliko wengine; ni wakati wa
kudhihirisha kufa kwetu pamoja na Kristo, ni wakati wa kuyatafuta mapenzi ya
Mungu na kuyatenda. Yesu yu karibu kurudi kulichukua kanisa lake. Ni wakati wa
kuliandaa kanisa kwa ajili ya unyakuo.
Ni nyakati za
mitume kusimama kama mitume katika mapenzi ya MUNGU, manabii kusimama kama
manabii katika mapenzi ya Mungu, na wachungaji nao vivyo hivyo, wainjilisti,
waalimu, viongozi, waimbaji nawengine wote vivyo hivyo. Kanisa si majengo, ni
kusanyiko la watu waliotengwa kwa ajili ya kusudi la Mungu. Wewe
unayeng’ang’ania kumiliki kanisa mwenyewe, pole! Wewe unayeng’ang’ania dhehebu
linalomkataa Yesu na kufundisha uongo, pole: Wewe ni mtumishi wa shetani, na
shetani ndiye baba yako. Huwezi kuwa mtumishi wa Mungu huku wewe ni mlevi,
mzinzi, mwalimu wa uongo, mnafiki, msengenyaji, mla rushwa, mkatili, na mengine
kama hayo; hakika huwezi.
Nabii Ezekieli aliambiwa atoe unabii juu ya Wachungaji (viongozi,
watumishi) wa watu wa Mungu Israeli. Neno linasema, “Mwanadamu, toa unabii
juu ya wachungaji wa Israeli, toa unabii, uwaambie, naam, hao wachungaji, Bwana
MUNGU asema hivi; Ole wao wachungaji wa Israeli, wanaojilisha wenyewe;
je! Haiwapasi wachungaji kuwalisha kondoo?” Jambo hili ni jambo la
kusikitisha sana; yaani wachungaji kujilisha wenyewe na kusahau kulisha kondoo.
Ubinafsi wa namna hii ndio uliolivamia kanisa la nyakati za leo, hasa kanisa
lililo Afrika. Matumbo yetu yamekuwa makubwa kiasi cha kutupofusha tusione
mateso ya kondoo tuliopewa kuwachunga. Mahitaji yetu yametufanya viziwi
tusiweze kusikia vilio vya kondoo wanaotaabika katika nyika wasione wa kuwapa
hata tone la maji.
Paulo akiwa katika Roho Mtakatifu,
aliongea katika hali ya huzuni kubwa juu ya watu wanaohubiri Injili ya namna
nyingine na kuipotosha kweli ya Mungu. Alisema, “Lakini ijapokuwa sisi au
malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo
tuliyowahubiri, na alaaniwe.” Tena akarudia kwa mkazo zaidi akasema, “Kama
tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi
injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe.” (Wagalatia 1:8-9)
Wewe nabii na mwalimu wa uongo, laana hii huwezi kuiepuka! Labda uamue leo
kutubu na kuamua kuihubiri iliyo Kweli. Ninajua nafsi yako inakushuhudia kitu
juu ya hayo unayofundisha. Wewe unayefundisha ili upate mali na kulishibisha
tumbo, ole wako.
Ujumbe huu umekujia ili usiwe na la
kujitetea mbele za Mungu. Biblia unayoichezea kwa kuitafsiri kama unavyotaka au
kwa kusukumwa na Ibilisi uliyeamua kumtumikia, iliandikwa kwa machozi na damu.
Mitume walikubali kuteswa hata kuuawa wakiitetea Imani ya kweli. Leo hii
unasimama, unajiita nabii, mtume, mwalimu au hata mchungaji, kumbe ni
mwigizaji, mlaghai na mjumbe wa shetani; hakika hutafika mbali. Jiulize leo
umeua wangapi na uongo uliofundisha! Angalia vilio ulivyosababisha kwa sababu
ya tamaa yako ya fedha. Watu wanakufa kwenye dhambi, huku ukujitajirisha na
kuona fahari. Unatabiri uongo hata wewe mwenyewe unajua! Saa yaja na sasa ipo,
utakaposimama mbele ya kiti cha hukumu kutoa hesabu mbele za Mungu. Sijui utajibu
nini!
Mtume Yakobo anaonya na kusema,
“Ndugu zangu, msiwe waalimu wengi, mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi.”
(Yakobo 3:1) Leo kila mtu anajiita nabii, mwalimu, mchungaji, mtume na mengine,
wakifikiri ni sifa. Kumbe ni msalaba, huduma si ufahari. Huduma ni msalaba, ni
kushiriki mateso pamoja na Kristo. Ufahari wetu u katika Kristo. Tukiishi
tunaishi pamoja naye, tukifa tunakufa pamoja naye, tukiudhiwa tunaudhiwa pamoja
naye, tukitukanwa na kukakataliwa tunakuwa pamoja naye! Hii ndiyo fahari tuliyonayo.
Magari, majumba, fedha na vyote vya ulimwengu huu ni ziada kwetu. Ufalme wa
Mungu ndio kipaumbele chetu.
Mwisho niseme,
“Watumishi wenzangu, “tukiwa tumefufuliwa pamoja na Kristo tuyatafute yaliyo
juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Tusikubali kuwa na majina ya
kuwa hai kumbe tumekufa, tung’ang’anie uhai wetu katika Kristo. Tuwe watu wa
kujichunguza kila siku tukijikumbusha kama Paulo alivyojisema, “bali nautesa
mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe
mtu wa kukataliwa.” (1Wakorintho 9:27) Tena tukatae kulichanganya Neno la
Mungu nauongo. Tusiwe watu wa kupenda fedha ya aibu, tutumike kwa uaminifu hata
kufa. Tuungane na mtume Paulo tena katika maneno haya:
“Kwa sababu hiyo, kwa kuwa tuna huduma hii,
kwa jinsi tulivyopata rehema, hatulegei; lakini tumekataa mambo ya aibu
yaliyositirika, wala hatuenendi kwa hila, wala kulichanganya neno la Mungu
na uongo; bali kwa kuidhihirisha iliyo kweli twajionyesha kuwa na haki,
dhamiri za watu zikitushuhudia mbele za Mungu.” (2 Wakorintho 4:1-3)
Neno linasema, “Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa,
mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka. (1 Petro 5:4) Naye Mungu
antayafuta machozi yetu tukishaondoka katika ulimwengu huu. Tusikubali kubaki
na miujiza, kunena kwa lugha na matendo ya Imani huku tukiwa hatuna upendo wa
kweli na Mungu. Yesu anasema, “Wengi wataniambia
siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako
kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni
kwangu, ninyi mtendao maovu. Usijitie moyo
na miujiza, angalia mahusiano yako na Mungu zaidi ya miujiza. Angalia usije
ukapata hasara ya nafsi yako! Utumishi si tiketi ya kuingia mbinguni. Ni lazima
tuwe watakatifu.
Ifike
mahali kuishi kwetu kuwe ni Kristo. Na tuwe watakatifu kama Mungu wetu alivyo mtakatifu.
Tusitumike kwa hila, bali kwa adili tukimzalia Mungu matunda kwa utumishi
uliotumika. Tusiwe kwazo la namna yoyote ili utumishi wetu usilaumiwe, bali kwa
kila jambo tujipatie sifa njema (2Wakorintho 6:3-4). Tukubali kuwa Nuru
ing’aayo gizani, tukikataa kila lililo baya. Tusiwe rafiki wa dunia
(tusiipende), bali tuzidi kuimarisha uhusiano wetu na Mungu kila siku (1Yohana
2:15) Tuepukane na tamaa za mwili, tamaa za macho na kiburi cha uzima.
Tuimarike katika uchaji, na unyenyekevu wa kweli. Tukiyaishi mafundisho yetu,
na kumtambulisha Yesu tuliyembeba kwa ujasiri. Huu ndio utumishi utakaotupa
heshima mbele za Mungu (Yohana 12:26) Tunapaswa kuimarika katika Imani, kisha
tuzidi sana kuitenda kazi ya Mungu (1Wakorintho 15:58), hakika taabu yetu
haitakuwa bure.
Ni mimi mtumishi mwenzako nikibubujikwa na
machozi kwa ajili ya kanisa la Mungu. Nakutakia neema na uwezezo kutoka juu
katika kuyatenda mapenzi ya Mungu. Upendo wa Mungu, na ushirika wetu katika
Roho Mtakatifu uzidi kudumu daima. Mwokozi wetu Yesu adhihirike kwako kwa
matendo makuu. Huduma yako iliyokuwa imenyauka ichanue tena kama mti wakati wa
masika. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na ikae pamoja nawe. Amina.
Na: Mwl. Stephen M. Swai
AMKA GOSPEL MINISTRIES INT’L
Simu: +255 713 511 544