Kiongozi ni mtu aliyejitoa au aliyeminiwa na kupewa dhamana ya kusimamia, kutoa dira na kuonyesha mfano wa jinsi mambo yanapaswa kufanyika. Kuwa kiongozi si jambo rahisi, wala si jambo gumu. Si rahisi kwani linahitaji kujitoa kikamilifu ili maono au malengo yapate kufukiwa, na si gumu kwani si kila kiongozi ni kiongozi. Kukubali nafasi tu hakumfanyi mtu kuwa kiongozi.
Kukubali nafasi pamoja na kukamilisha majukumu ya nafasi hiyo ndio uongozi. Kiongozi ni lazima awe na uwezo wa kuwashawishi wengine na kuwafanya wawe tayari kutekeleza majukumu yanayolenga kutimiza malengo. Mfano mzuri wa kiongozi ni Musa, yeye alifanikiwa kuwashawishi wana wa Israeli kuondoka Misri na kwenda Kanaani. Mfano mwingine ni Yesu, yeye aliwaongoza wafuasi wake kwa kuonyesha mfano katika mambo yote. Yesu alikuwa kiongozi mwenye ushawishi mkubwa sana. Ushawishi wake ulitokana na uwezo wake wa kufundisha, uwezo wake wa kutatua matatizo ya watu, na ujasiri wa kuwaita wengine katika wajibu aliokuwa nao.
Mara nyingine aliwaita wanafunzi wake wamfuate, japo wengi walimfuata pasipo hata kuwaita. Baada ya maelezo haya mafupi napenda kukupa sifa kadhaa za kiongozi bora:
1. Kiongozi ni mtu anayejitambua. Yeye ni nani, ana wajibu gani, ana mapungufu gani na ana uwezo (strength) gani. Si mtu anayefanya mambo kiholela. Kila alifanyalo huwa na sababu.
2. Ni mtu anayeweza kusimamia mambo yake mwenyewe, yakiwemo masomo, familia, biashara, kazi nk.
3. Ni mtu wenye upendo na watu. Kiongozi asiye na upendo hawezi kujitoa kwa dhati kwa ajili ya watu wake. Yesu alikuwa tayari hata kufa kwa ajili ya watu. Ni mtu anayewatanguliza wengine.
4. Kiongozi ni mtumwa wa wengine. Mtu asiyetaka kutumikishwa na maswala ya wengine jawezi kuwa kiongozi
5. Mtu mwenye maono au anayejia maono anayotakiwa kuyasimamia. Maono hutoa mwelekeo, na majukumu muhimu yanayohitajika. Kiongozi asiyejua maono hataweza kuwapanga watu wake ipasavyo, wala hawezi kuweka vipaumbele.
6. Mtu mwenye uwezo wa kuwashawishi wengine. Je, maisha ya mtu yanadhihirisha nini? Je, ni mtu anayeweza kuaminika na wengine. Maneno na matendo yake yanaashiria uwezo alionao? Je, ana karama au vipawa gani? Ongea yake inadhihisha hekima kwa kiasi gani? Je, anaweza kuwavutia wengine? Bila ushawishi kiongozi ni mtu aliye na cheo tu. Uongozi mzuri ni ule unaotokana na uwezo wa mtu, kielimu, kiakili, au kiroho.
7. Uongozi unahitaji kutokuwa mbinafsi na kujua kuwainua wengine. Kiongozi ni lazima awe tayari kuwapa wengine nafasi, na kuwainua. Kiongozi anayejiangalia mwenyewe tu si kiongozi. Tamaa sio sifa ya kiongozi bora. Kiongozi bora hufurahi wengine wakifurahi, na kuhuzunika wengine wakihuzunika.
8. Kiongozi ni mtu mwenye hekima na busara. Si mtu wa hasira na kukurupuka. Anaweza kutatua shida za watu. Tena ni mtu mwenye utulivu katika kukabiliana na changamoto. Si mtu wa malalamiko. Musa aliweza kusimama katikati ya watu wenye manung'uniko kwa kumtegemea Mungu na kuwahimiza watu wasichoke. Kiongozi mwenye busara hapendi mashindano, magomvi na mivutano.
9. Kiongozi bora ni mfano bora. Kila anachokifanya ni kielelzo cha mafanikio. Ni wa kwanza kwenye kila jambo liwe gumu au jepesi. Si mtu wa maneno tu, bali ni mtu wa vitendo.
10. Kiongozi ni mzazi na mlezi wa viongozi wengine. Kiongozi asiyezaa na kulea viongozi wengine hana sifa ya kuwa kiongozi. Kuzaa viongozi huthibitisha kuwa yeye ni kiongozi (mtoto wa nyoka ni nyoka). Kuwalea iongozi huthibisha ushawishi wake kwa wengine. Viongozi hupenda kukaa nyuma ya viongozi.
11. Kiongozi bora ni mcha Mungu. Mtu asiyetambua uwepo wa Mungu, na kuheshimu nafasi ya Mungu kwenye maisha yake na ya wengine hawezi kusimama na watu hata wakafikia maono. Mungu ndiye kila kitu kwa watu wake. Hofu ya Mungu humfanya kiongozi kuwa mtu mwenye utu. Imani kwa Mungu ni nguzo muhimu katika kufikia maono yoyote yenye tija kwa wengine.
12. Kiongozi bora ni mtu mwenye kutunza kumbukumbu. Anaandika maono, mikakati na mambo yanayojitokeza kwenye kazi. Anawakumbuka watu wake. Na anazikumbuka ahadi zake. Ni mtu mkweli, akisema anamaanisha alichokisema. Na anakumbuka alikotoka, si mtu wa kujisahau na kujiona bora kuliko wengine. Ni mtu wa daftari wakati wote.
14. Ni mtu wa watu, na anapenda kufanya kazi kwenye umoja (timu). Ni mtu anayejua naye ni mmoja wa wachezaji kwenye timu, si mtazamaji. Anajali maumivu ya wengine na anaweza kuvaa viatu vya wengine. Ni mtu anayejali jamii, hata akiwa nje ya jamii. Hana makuu, na anapenda kunyenyekea na kuwasikiliza wengine. Si roboti, wala si sanamu. Ni mtu anayeishi kama mtu.
15. Ni mzalendo kwa nchi au taasisi anayoiongoza. Uzalendo ni upendo wa dhati kwa nchi au taasisi. Ni kujitoa kwa kimaanisha kuibeba nchi au taasisi hata kama maslahi binafsi yataguswa. Mzalendo hafurahii udhali au watu kuonewa. Ni mtu anayeweza akupiga kelele kukemea uovu hata akiwa peke yake. Mzalendo anaweka maslahi ya nchi au taasisi mbele.
Je, wewe ni kiongozi? Je, wewe ni kiongozi bora? Uongozi una nafasi kubwa ya kupoteza, kubomoa au kuharibu taswira ya kesho. Kila mafanikio huanza na kiongozi mwenye maono. Ni maombi yangu kuwa Mungu akufanye kuwa kiongozi bora. Ni wito wangu kwako leo, kwamba usimame kikamilifu ili kuweka msingi wa mafanikio kwa kizazi cha kesho. Je, watoto wetu wanajifunza nini kutoka kwetu?
