Friday, 18 October 2024

MWANAUME KWENYE NAFASI YA "MUME"

Mume ni mwanaume aliyeoa kwa kuzingatia vigezo na taratibu za kijamii, kishria na za kiroho. Mume si rafiki wa kiume (boyfriend), hawara, wala si mzazi mwenza (kwamba tu umezaa naye). Ili mtu awe mume ni lazima akamilishe taratibu za kijamii, za kisheria na za kiroho katika kuanzisha ndoa.

Ndoa kibiblia, ni muunganiko wa kudumu kati ya mtu mke na mtu mume; na mwanzilishi wa muunganiko huu ni Mungu mwenyewe. Katika Mithali 19:14 tunasoma, “Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana.” Hivyo, katika kuanzishwa kwa ndoa kibiblia ni lazima Mungu ahusike. Tangu Agano la kale hata sasa, tunaona Mungu akihusika kwa ukaribu sana kwenye ndoa. Ndoa ya kwanza aliifunga mwenyewe kati ya Adam una Eva.

Ibrahimu alipewa Sara kuwa mkewe, Isaka alipewa Rebeka kuwa mkewe, Yakobo alipewa Lea na Raheli kuwa wake zake. Hata kama walijihusisha na wanawake wengine, bado hawa walibaki kuwa na nafasi ya pekee kwao. Kwa hiyo, kuwa mume kwa mke si jambo rahisi na la kawaida, ni jambo lenye kusudi la Mungu ndani yake.

Ukifuatilia ndoa hizi niliziozitaja utagundua kwamba familia zilihusika kwa ukaribu sana katika kuianzisha ndoa. Mfano Rebeka aliulizwa na wazazi wake kama yuko tayari kuambatana na yule aliyetumwa kuja kumchukua. “Wakamwita Rebeka wakamwuliza, Je! Utakwenda na mtu huyu? Akasema, Nitakwenda.” (Mwanzo 24:58) Sheri ana kanuni za jamii zao nazo zilizingatiwa kwa karibu sana.

Maagizo ya Mungu kwa Mume

                                                                                      i.          Kuambatana na Mkewe

Makubaliano kati ya mwanaume na mwanamke katika mahusiano siku zote yamekuwa yakizingatiwa. Tangu zamani iliwalazimu, mwanaume na mwanamke kukubali kuambatana pamoja. Kibiblia, mume ni lazima aambatane na mkewe na kumpokea kama sehemu ya mwili wake (Mwanzo 2:24, Waefeso 5:31, Mathayo 19:5). Tangu uumbaji, mwanamke ni sehemu ya mwili wa mwanaume.

Mungu aliuchukua ubavu mmoja wa Adamu na kumuumba Eva. Naye Eva alipoletwa kwa Adamu, kwa furaha, na kwa kumkubali Adamu lisema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume.” Kule kutolewa katika mwanaume ndiko kulikomfanya Eva aitwe mwanamke.

Mwanaume akimwona mkewe katika mtazamo huu ni rahisi kuambatana naye. Kuambatana kunahusu mambo yote katika Maisha: yaani kimwili na kiroho. Mume hana maisha binafsi tena, kila kitu ni shirika. Kwa kukazia Zaidi Paulo anasema, “Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe.” (1 Wakorintho 7:4)

Kuambatana kati ya mume na mke, ni kwa lazima. Japo changamoto ni kubwa katika kizazi hiki, inawezekana kuliko vizazi vyote. Ile neno aliloambiwa Eva kusema “tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.” Limekuwa gumu kwa wanawake walio wengi. Hivyo mashindano, chuki, na kutendeana kwa hiyana kumetawala kati ya wanaume na wanawake.

Kuambatana ni jambo pana katika Maisha ya wanandoa.  Mume ni lazima akubali na ajitoe:

Kuambatana na mkewe katika kuhudumiana, huku kunahusisha kujitoa kwa kila mmoja kwa mwenzake. Huduma ya tendo la ndoa ni moja ya huduma za msingi katika ndoa. Paulo anasema, “msinyimane” (1 Wakorintho 7:5). Kuhudumiana kiroho na kimahitaji na mengineyo pia ni sehemu ya kuambatana kwa wanandoa.

Kuambatana na mkewe katika kazi; huku ni kuunganisha mikono pamoja katika kuzalisha. Kazi za nyumbani, za kiuchumi, za kanisa na nyinginezo ni lazima zifanyike katika ushirika wa mume na mke katika ndoa. Mke n msaidizi, mume ni mwongoza njia. Wote wawili ni wasafiri katika chombo kimoja kiitwacho ndoa au familia. Kutiana moyo, kusaidiana, kuwezeshana, na kupeana nafasi katika kazi katika kuambatana hakuepukiki.

Kuambatana na mkewe katika mapato na matumizi; hili ni eneo linalohusu uchumi katika ndoa. Kimsingi uchumi wa ndoa hujengwa na mume na mke, hivyo wote ni lazima wahusike vilivyo katika kupata na kutumia mali zinazozalishwa. Japo jukumu la kuzalisha amepewa Adamu, Eva hawezi kujiweka pembeni kwani naye ni msaidizi. Na Zaidi ni mwili mmoja na Adamu.

Kuambatana na mkewe katika huduma na maisha ya kiroho (kiimani): Imani hubeba hatima ya mwanadamu. Tena huathiri maamuzi ya mtu moja kwa moja. Ikitokea mke na mume hawako pamoja kiimani au kihuduma, kuambatana huwa kugumu. Mume ni lazima akubali kuambatana na mkewe katika mambo ya kiroho ili wawe na hatima njema, vivyo hivyo na mke. Maombi, kusoma neno, utoaji, kutumika, na kumtafuta Mungu kwa pamoja ni msingi wa Maisha ya kiroho katika ndoa.

Kuambatana na mkewe katika malezi ya watoto (kabla na baada ya kuzaliwa): huku kunahusisha kupanga idadi ya watoto, aina ya malezi ya kuwapa watoto, jinsi ya kukidhi mahitaji ya Watoto, na jinsi ya kutunza maadili ya familia.  Mambo haya hayawezi kufanyika kwa ufanisi bila maridhiano na maamuzi ya pamoja. Mume bora ni yule anayeweza kusafiri salama akiwa bega kwa bega na mkewe pamoja na Watoto.

Kuambatana na mkewe katika mipango (iweni na nia moja) na kukuza uchumi wa ndoa na familia: katika ndoa ni lazima kupanga pamoja. Mume atoe mawazo yake, mke naye atoe yak wake. Ndoa iliyogawanyika mara nyingi, huanzia kwenye mipango. Mipango ikishatofautiana, matumizi hayawezi kwenda sawa. Kushirikishana mipango ni njia muhimu katika kudumisha kuambatana. Mume ni lazima amshirikishe mkewe mipango yote aliyonayo.

Mume pia ana jukumu kuambatana na mkewe katika matatizo mfano magonjwa, misiba na mengineyo. Mwanaume anayekimbia matatizo, hana sifa ya kuwa mume. Kuoa ni kukubali kuchukua madhaifu ya mke, na kumshirikisha mke udhaifu wako. Kutafuta suluhu ya matatizo ni moja ya jukumu la msingi la mume katika ndoa.

Mungu ni lazima aambatane na mkewe katika kusaidia ndugu na kuwatunza wazazi. Japo hili linakwenda kwa pande zote mbili, ni lazima mume awe mstari wa mbele kuwasaidia ndugu wa mkewe. Kuambatana kunadai kubebeana mizigo. Katika familia zetu za kiafrika tuna majukumu Fulani ambayo hatwezi kuyaepuka, hivyo kusaidiana ni kwa lazima.

Haya ni baadhi ya maeneo ya msingi, yanaweza kuwepo mengine zaidi. Jambo la msingi hap ani kujua kwamba kuwa ‘mume’ ni kuwa mshirika wa karibu na wa pekee kwa mkeo. Mke ameumbwa kufurahia ushirika na kujaliana katika mahusiano. Hajaumbwa kupambana peke yake, hivyo kuambatana naye ni njia muhimu katika kujenga amani ya ndoa. Mume naye hawezi peke yake, hata  Adamu yalimshinda, hivyo ni lazima mke akubali kuambatana na mumewe.

                                                                                          ii.          Kumpenda Mkewe 

Paulo anasema, “Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. (Waefeso 5:28-29)

Hapa Paulo anasema juu ya kuwapenda wake zetu kama miili yetu, hili ni fumbo zito kwa mume. Waume wote tungeweza jambo hili, ndoa zetu zingekuwa paradiso. Kizazi chetu kinashangaza sana, kwani kesi za waume kuwapiga, kuwaumiza, kuwaacha, wakati mwingine hata kuwaua wake zao zimekuwa nyingi sana. Paulo amatuambia “haiwezekani mtu akauchukia mwili wake. Bali huchukua jukumu la Kuulisha na kuutunza.

Kutokea kwa matukio haya mabaya kunadhihirisha kwamba wanaume wengi hawajawapokea wake zao kama miili yao wenyewe au hawana upendo wa kweli kwa wake zao. Mume aliyempokea mkewe kama mwili wake na kumpenda ni lazima awe na upendo ulio hai. Yaani:

v    Upendo kwa mkewe huambatana na kuhakikisha kwamba anakula na anapata mahitaji yake yote (matunzo). Hata kama ana kazi yake usikubali mkeo akajigharamikia kila kitu, tumia fedha yako kumlisha na kumnunulia mahitaji yake. Kumjali mke kimahitaji ni jukumu la msingi la manaume. Mume ni lazima awe na macho ya kuona mahitaji ya mkewe.

Si lazima mke aombe kila kitu. Vitu vingine ukiona anavihitaji mnunulie naye atajisikia kupendwa kila wakati. Kama mume unayempenda mkeo, hupaswi kuishia kwenye maneno tu, ni lazima upendo wako uambatane na kujali mahitaji. Ukumbuke kabla ya kumwoa mkeo alikuwa anapewa mahitaji na wazazi wake na pengine wanaume wengine, au kujihangaikia mwenyewe. Hakikisha unazipa mapengo yote kwa kufanya Zaidi ya wote.

 

v    Upendo unadai kujitoa: Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake. (Waefeso 5:25). Kujitoa ni kwenda Zaidi ya ile hali ya kawaida ya kutimiza majukumu. Unapofika mahali kama mume ukatafuta muda wa ziada, ukafanya zaidi, ukakubali kuumia kwa sababu ya mkeo basi unakuwa unautimiza upendo.

Linapotokea jambo gumu kwa mkeo, hakikisha unakuwa mstari wa mbele kama mume kutafuta utatuzi. Hata kama litakugharimu kupoteza baadhi ya vitu, Mungu atawajalia neema mtapata vingine baada ya jambo hilo kupita. Kazi zipo tu, ila kujitoa kumsaidia mwenzako wakati wa taabu au hata mazuri yenye gharama ni muhimu.

NiIisikia habari za kijana mmoja (mume) ambaye alimwacha mkewe hospitalini akiwa mahututi kwa sababu ya kuogopa hasara ya kazi aliyokuwa anaifuatilia. Mkewe alipotoka hospitalini, alikuwa na uchungu mwingi sana kwa kuona mumewe amethamini kazi kuliko Maisha yake. Kurekebisha kosa kama hilo, ni gharama kubwa kuliko kuacha faida ikapita.

v Upendo unadai kusamehe na kusahau: Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao. (Wakolosai 3:19) Wanaume wasio na moyo wa kusamehe mara nyingi huwatendea wake zao mabaya. Upendo hauhesabu mabaya (1 Wakorintho 13:4 “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya”

Hivyo, mume mwenye upendo ni lazima ajifunze kumsemehe mkewe. Ni muhimu kukumbuka wamba, wanawake ni watu wa mahusiano zaidi kuliko kazi, hali wanaume ni watu wa kazi zaidi. Kupishana katika mazingira kama haya ni kawaida. Wanawake huwa hawapendi kukosea, hivyo kusamehewa wakikosea ni lenye nafasi kubwa kwenye maisha yao.

v    Upendo unadai heshima: Paulo anafundisha  na kusema, “Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe. (1 Petro 3:7). Mume ana jukumu la kuitunza heshima ya mkewe kwa kumvisha vizuri, kumpamba, kumwendeleza, kumpa nafasi na kumsikiliza.

Kwa sababu ya maumbile yao au hali ya maisha au historia wakati mwingine mke anaweza kuonekana kama hana heshima. Kwa mume, mke ni lazima awe malikia katika hali zote. Mume hatakiwi kumvunjia mkewe heshima, kwa kwenda nje ya ndoa, vivyo hivyo mke. Kama mume, ni muni kuyaheshimu mawazo ya mkeo, hisia zake, na nafasi yake kwa ujumla.

v    Upendo unaambatana na kumlinda mkeo: Kwa hiyo jihadharini roho zenu; mtu awaye yote asimtende mke wa ujana wake mambo ya hiana. (Malaki 2:14-15) Wanapoinuka watu kumshambulia mkeo usinyamaze, usiwape ndugu (wazazi, wadogo zako, dada zako au marafiki) kumshambulia mkeo. Katika changamoto zote, tunza heshima ya mkeo (chukua aibu yake, na Mungu atakubariki). Zaidi sana usimgeuke na kumtendea mambo ya hiana. Mweke mkeo kwenye mzingira salama, na hakikisha anakuwa salama wakati wote.

Kila mwanamume au mwanamke anapaswa kutunza heshima ya ndoa: Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu. (Waebrania 13:4) Usafi wa ndani na wa nje ni muhimu katika ndoa. Usafi wa tabia ni wa muhimu zaidi sana. Tabia za uzinzi na uasherati zimeharibu mahusiano ya wanadoa wengi, na yameleta aibu isiyofutika.

Mambo ya kufanya kama mume ili mkeo akufurahie

Pamojana maagizo haya makubwa mawili tuliyokwisha kuyaona, kuna mambo kadhaa ya kiutendaji yatakayomfanya mume awe mtu wa kutamanika kwa mkewe kila wakati.

1.               Fanya kazi kwa bidi ili kukidhi mahitaji ya familia, kwa kiwango chako. Mke hujisikia salama akiwa na mume mpambanaji na anayezalisha.

2.               Timiza wajibu wako kwa jamii, mfano kanisani au kazini au pale unapoishi. Mke hujisikia vizuri sana akiona mumewe anaheshimiwa na kusemwa vizuri na watu.

3.               Jifunze kumpongeza mkeo akifanya vizuri, na kumkosoa kwa upendo akifanya vibaya. Hili litampa uhakika wa wewe kuambatana naye, hivyo kuvutiwa na wewe zaidi.

4.               Jifunze kumsikiliza na kuongea na mkeo. Hili ni la muhimu sana, mwanamke hujisikia kama malkia akiona mumewe ametulia akimsikiliza. Mume mwema humsikiliza mkewe kwa uvumilivu na busara. Wanawake wengi hupenda kuongea kuliko kusikiliza. Japo wapo ambao hupenda kusikiliza pia, hivyo msome mkeo na kuhakikisha unakwenda naye alivyo.

5.               Msifie mkeo kwa kumpa majina mazuri, sifia umbile lake na kumtia moyo kila wakati. Mwite mkeo “mpenzi, laazizi, malikia, mke; ikiwezekana weka na kiingereza kidogo kama “honey”, “sweetie” “baby” “sweetheart” na mengine. Haya humpa mke ujasiri na kujikubali zaidi, hivyo kila wakati atatamani uwe naye ili umsifie zaidi.

6.               Mnunulie mkeo zawadi za hap ana pale. Hili litampa kukuamini zaidi, na kuona kumbe unamwaza kila wakati.

7.               Jitahidi kumtosheleza mkeo katika tendo la ndoa. Hapa niongee kwa herufi kubwa “kilichomtoa mkeo kwao pamoja na mengine yote, nit endo la ndoa. Hakikisha kama mume unaongeza ufanisi kila siku. Mkeo atakufurahia sana ukimpa kile anachokihitaji chumbani mwako.

8.               Mwamini mkeo, japo wapo wanawake wasioaminika, tunajua aliyetoka kwa Mungu ni wa kuaminika. Mke akiaminiwa kuna asilimia nyingi za kufanya vizuri kuliko asipoaminiwa. Mpe uhuru, akikuambia jambo likubali bila kuona shaka. Kama una shaka na jambo mwambie wazi ili akupe maelezo. Wanawake ni wasiri lakini wapewa uaminifu, ni lazima walipe uaminifu.

9.               Jenga urafiki wa karibu na mkeo, wakati mwingine muwe na muda wa kucheza, kutaniana kidogo, kukumbushana mambo mbalimbali na mengineyo.

10.            Jifunze kumshukuru mkeo kwa huduma anazokupa mfano tendo la ndoa, chakula, kukufulia, kusafisha ndani, kukutunzia vitu, kulea Watoto na mengineyo.

11.            Pale inapowezekana jiepushe na yale asiyoyapenda, na kuweka muda kwa yale anayoyapenda.

12.            Usimtanie kwenye madhaifu aliyo nayo. Ukifanya hivyo unaweza kumuumiza moyo na kuleta hisia tofauti.

13.            Usimlinganishe mkeo na wanawake wengine, mkubali kama alivyo na mzungumzie yeye zaidi ukiwa naye. Epuka kuwasifia wanawake wengine ukiwa na mkeo.

14.            Ipende familia, ikiwa ni pamoja na kuwahudumia watoto na ndugu. Mke hufurahishwa sana na mume anayeipenda familia. Niliongea na binti mmoja akaniambia moja vitu vinavyomuumiza duniani ni kuona baba yake hajali familia yake. Usilete maumivu kama haya kwenye ndoa yako.

15.            Jiamini na simamia maamuzi yako. Mke huwa hapendi kuona mumewe anatawaliwa na watu wengine. Uthabiti na ujasiri wa kuamua humtia moyo mke.

16.            Uwe mkweli kwa mkeo. Hakuna ukweli ambao mkeo anayekupenda kwa dhati atashindwa kuchukuliana nao. Uongo ni sumu mbaya sana, ukimdanganya kisha akaja kuujua ukweli itakuwa mbaya mara mbili ya kumwambia ukweli.

17.            Usikae mbali na mkeo kwa muda mrefu bila sababu za msingi na makubaliano ya pamoja; ikitokea inakulazimu, hakikisha unakuwa na mawasiliano ya mara kwa mara.

18.            Msaidie mkeo kazi za nyumbani, hasa akiwa amelemewa Na majukumu, amechoka, au anaumwa. Hii itmfanya akuone kama rafiki yake wa karibu sana.

19.            Pale inapowezekana, uwe na mtoko na mkeo; mara kwa mara uwe na faragha naye. Huyo ndiye make wa ujana wako. Kuambatana naye, kutembea pamoja naye, kwenda kanisani pamoja naye, kula pamoja naye, na mengine kama hayo, huongeza sana ladha ya mahusiano.

20.            Usiogope kuwa uchi mbele ya mkeo. Kuoga pamoja ni dsturi nzuri kwa wanandoa. Kuwa huru kwa mkeo Ni ishara ya wazi kwamba unamwamini, na umejitoa kwa ajili yake. Hii inaongeza furaha na mahaba kwenye ndoa.

21.            Dumisha ukaribu na mkeo. Usipende kukaa mbali naye muwapo pamoja. Mkumbatie, mbusu, ongea naye kwa kamnong’oneza. Hili litampa kuona kwamba unamkubali Na hatimaye naye atajibu mapigo.

22.            Heshimu hisia zake - usiwe mtu wa kulazimisha mambo bila sababu. Kama Kuna ulazima kwenye jambo Fulani tumia lugha nzuri kulizungumza, mweleweshe. Usitake kusikilizwa wewe tu. Wakati mwingine mwenzako naye ana namna anatamani mambo yaende. Akikuhitaji pia Ni vizuri ukapatikana.

Saturday, 19 December 2020

MGOGORO WA "CASFETA TAYOMI" NA "CASFETA" NI TISHIO KWA KANISA LA KESHO

Wapendwa Nawasalimu katika Jina la Yesu!

Nianze kwa kuuliza "Je! Kristo amegawanyika?" (1Wakorintho 1:13) Je, Yesu wa CASFETA TAYOMI ni yupi, na wa CASFETA ni yupi? Je, ni Yesu wawili tofauti? Kwa nini mgogoro kati ya makundi haya mawili hauishi? Maswali haya yamenijia baada ya kushuhudia visanga kadhaa kwenye shule za sekondari kwa miaka mingi sasa.  Nakumbuka mkuu mmoja wa shule alisema, “katika shule yangu sitaki kusikia mgogoro wowote wa vikundi vya dini, hasa kwa walokole kwa sababu huwa hawapatani siku zote”

Nimekuwa nikitafakari juu ya hatima ya tofauti kubwa zinazojitokeza katika makundi haya mawili yenye jina moja. Nilichogundua ni kwamba hatima yake si njema, zaidi ni kuendelea kuligawa na kulidhohofisha kanisa. Watoto na vijana wakijengwa katika misingi ya migogoro na kutoelewana hawataweza kusimama pamoja tena, labda ifanyike toba na matengenezo mapema. Kwa kipindi kirefu sasa, kumekuwa na migogoro mingi mashuleni na vyuoni ambayo badala ya kutafutiwa tiba ya kudumu, imekuwa ikifunikwa tu ili maisha yaendelee. Kuna mshangao mkubwa kwa wengi juu ya kutokuelewana kwa walokole. Wengi huuliza: "Kama wana Yesu kweli, mbona hawaelewani." Baadhi ya wakuu wa shule wamekuwa wakikosoa vikali hali ya uhasama iliyopo miongoni mwa CASFETA hizi mbili.

Sijataka kuamini kwamba mithali isema “Baba za watu wamekula zabibu kali, na meno ya watoto wao yametiwa ganzi” itatimia kwetu. Najua viongozi wengi wa kanisa huwa hawapendi mjadala katika swala hili. Naamini hili haliwazuii watu kuendelea kusema kile wanachokiona juu ya kanisa la Mungu. Ili kanisa la Mungu lijengeke katika utakatifu na umoja ni lazima mambo yote yawe sawasawa. Migogoro miongoni mwa vijana waliookoka mashuleni na vyuoni si ishara nzuri. Ni ishara kwamba kuna nyufa ambazo hazijazibwa. Migogoro ikitawala kati ya ndugu, inakuwa rahisi wao kwa wao kuangamizana. Adui pia anapata nafasi kwa urahisi.

Kuwa na vikundi viwili au hata zaidi ya viwili haina tatizo, inaweza kuwa njia nzuri kabisa ya kupanua wigo wa huduma, lakini vikundi hivi ni lazima viwe huru. Maana yake viwe na katiba isiyoingiliana na vingine, vifanye kazi kwa kuheshimu uwepo wa vikundi vingine, kila kimoja kiwe na misingi isiyoshawishi migogoro na vingine. Ni lazima inapotokea Mungu ameamua kupanua huduma amani izidi kuwepo. Paulo na Barnaba walipopishana, hawakuachana kwa ubaya. Kila mmoja alichukua njia yake kwa amani, na hakuna mahali ambapo mmojawapo alisimama kuusema ubaya wa mwenzake.

Hali sivyo ilivyo kwa CASFETA Tayomi na CASFETA: vimekuwa ni vikundi vya kuvunjiana heshima, kusemana vibaya hata kuitana waasi, kushindania matawi, kunyanganyana wahiriki na hata kuvutana wazi wazi.  Nina hakika jambo hili si jema, ni baya na halimpendezi Mungu. Tunapokuwa na viongozi wa wanafunzi wenye uwezo wa kuwasema wenzao vibaya au hata kuwatendea mabaya, hatujengi kanisa. Ujasiri wa kushuhudia unapungua, uwezo wa kuishawishi dunia unapungua.

Maono ya CASFETA zote mbili ni mazuri, na yana nafasi ya kuleta mapinduzi makubwa kwa kanisa. Changamoto ni kwamba hakuna amani kati yao. Kunapokuwa na Kamba inayovutwa na makundi mawili, kila kundi kuvuta kuelekea upande wake. Mwisho wadhaifu wataangukia upande wa wale wenye nguvu. Kiroho hali haiku hivyo! Tuliookoka wote tunapaswa kukaa upande mmoja ili tuzidi kuivuta dunia ije kwa Yesu. Tunapovutana sisi kwa sisi ni rahisi kuangukia upande wa shetani. Kwa nini tuwaache Watoto wetu wazidi kuvutana? Bilas haka kuna ugumu Fulani katika kuamua. Katika kutafakari nimegundua mambo machache:

Kwa nini mgogoro huu ni mgumu?

1.     WANAOGOMBANA WAMETOKA KWENYE FAMILIA MOJA.

Mgogoro kati ya CASFETA (Tayomi) na CASFETA) hauna tofauti na ule wa ndani ya familia. Watoto wanaweza kugombana lakini mwisho wanakutana kwa baba na mama mmoja. Wazazi na walezi wa vijana waliookoka wote walioko mashuleni na vyuoni ni makanisa yetu ya kipentekoste. Wakitoka shuleni wanakutana kanisani pamoja, na mchungaji wao ni mmoja. Kinachoshangaza ni vita na malumbano yanayoendelea kushamiri kati ya watoto hawa. Ile hali ya kugombana shuleni kwa sababu ya vyama na kurudi kanisani kuabudu pamoja inaonyesha udhaifu katika kanisa.

Baadhi ya watu niliowauliza juu ya jambo hili gumu, wamenipa majibu mepesi. Mmoja aliniambia, “Hili jambo limeshindikana huko tulipotokea sidhani kama linawezekana, wanaolisimamia ndio wanaojua zaidi” Nilipotafakari kauli hii nikagundia kwamba hakuna anayetaka kukubali lawama. Kila mmoja anataka aonekane ni mwema huku ukweli akiujua. Kinacholeta shida ni hali ya kutokuelewana ambayo haijapatiwa ufumbuzi. Ninafikiri kuna haja ya kuwapa vijana na watoto wetu mashuleni na vyuoni ufafanuzi wa kina ili wasije wakajikwaa.

Hatari kubwa zaidi inajitokeza pale ambapo Watoto wanakataliwa wanakwenda kwa wazazi kutaka msaada au uwezesho kwa ajili ya huduma. Nimeshuhudia baadhi ya wachungaji wakiwakataa wanafunzi waziwazi kwa sababu wanatoka CASFETA Fulani tofauti na ile anayoitaka yeye. Jambo hili limaleta majeraha kwa vijana wengi. Nilikutana na binti mmoja aliyekwenda kuomba mchango wa Injili kwenye kanisa alilokuwa anaabudu, akajibiwa vibaya akaumia. Watoto wa familia moja wanapokosa upendo wa walezi, au wakabaguliwa kwa namna yoyote ile huleta maumivu.

2.     SABABU YA KUTOFAUTIANA HAIKO WAZI IPASAVYO

Wengi hawaoni umuhimu wa kuwepo kwa mamkundi haya mawili kwa pamoja. Swali rahisi ambalo huuliza ni “Ni kwa nini msiwe pamoja” Ni kweli si lazima kuwa pamoja ikiwa Mungu hajakusudia hivyo, lakini ni lazima tutofautiane kwa amani. Kuna kanuni moja ya kibiashara ambayo nimejifunza kwa wafanyabiashara katika masoko makubwa. Mara nyingi maduka yanayouza vitu vinavyofanana hujikusanya pamoja. Nia yao ni kuwavitua wateja wengi zaidi ili kila mmoja apate. Huwezi kukuta wakigombana, kila mmoja hujitahidi kufanya ubunifu wake kuimarisha biashara yake.

Kwa CASFETA (Tayomi) na CASFETA hali sivyo ilivyo: mvutano ni mkubwa, hakuna anayetaka kumwona mwenzake. Kwenye tawi la CASFETA, CASFETA (Tayomi) akijitokeza ni shida, na vivyo hivyo kwa CASFETA (Tayomi). Kila mmoja anataka atawale yeye. Nilipata mgogoro mmoja wa tawi lililoanzishwa na CASFETA ila hawakujishughulisha kulihudumia, Tayomi walipokuja wakawahudumia na mwisho wakaligeuza tawi. Baadaye CASFETA walipojua, walikuja kwa hasira na kusababisha mgogoro mkubwa. Mambo hay ani chukizo kwa Mungu.

Fundisho linapokuwa moja inakuwa rahisi kwa washirika kuhama kutoka kundi moja kwenda jingine. Wengi waliokuwa katika moja ya makundi haya wakiwa sekondari (O-Level) waliingia kwenye kundi jingine wakiwa A-Level na hawakuona tofauti yoyote. Vijana wengi hawaoni sababu ya kutofautiana japo wameambiwa mengi. Hali ya kutokuwa na sababu za msingi za kutofautiana imeleta ugumu katika kulitangua fumbo hili. Nafikiri ni vizuri sababu zingeangaliwa kwa undani Zaidi ili kuona kama bado zinaweza kueleweka kwa kizazi hiki na kile kinachokuja. Yapo mambo yanayoweza kueleweka kwenye kizazi Fulani na yasiweze kueleweka kwenye kizazi kingine.

Katika mazingira hay ani lazima matengenezo yafanyike ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kwa kizazi kisichojua chimbuko la jambo. Alipoinuka Farao asiyemjua Yusufu Wana wa Yakobo waliingia kwenye utumwa. Kama sababu zikiwa ni za mtu binafsi, mtu huyo akishaondoka ni lazima aache mateso. Akiwepo anaweza kujirudi na kusema tofauti, asipokuwepo waliopo ni lazima wasimame kuziba nafasi yake.

3.     NI JAMBO LA KIHISTORIA

Kizazi kilichokuwepo wakati makundi haya yanaanza haikosi wanajua mambo mengi kuhusu makundi haya. Kizazi kinachoibuka na vitakavyokuja vitaathiriwa na umbali wa muda, hivyo tafsiri yao juu ya tofauti zilizopo ni lazima iwe tofauti na ya wale walioshuhudia mambo yote yakitendeka. Nilichogundua katika utafiti wangu ni kwamba mgawanyiko juu ya makundi haya uliimarishwa Zaidi na mpasuko uliokuwepo ndani ya kanisa kwa kipindi hicho. Majeraha ya mgogoro mkubwa wa kanisa yaliendelea kuchokonolewa na uwepo wa makundi haya mawili.

Si jambo rahisi kurekebisha jambo la kihistoria. Inagharimu kizazi cha mashuhuda kukaa na kizazi kinachoibuka ili kuweka mambo sawa. Kizazi cha mashuhuda kikiondoka bila kusuluhisha au kuandika ushuhuda wao katika kile kilichotokea ni rahisi kuleta shida kwa kizazi kinachofuata. Ninafikiri kuna haja ya kizazi cha mashuhuda kulitazama jambo hili kwa kina na kupata muafaka wake. Migogoro ikishazoeleka mara nyingi huwa kawaida lakini kiroho ni chanzo cha anguko.

Kila upande katika migongano inayoendelea, hujihesabia haki kihistoria. Hili haliondoi ukweli kwamba mgogoro wowote husababishwa na mambo kutokwenda sawa. Hivyo ni lazima kuna mahali mambo hayako sawa. Mabaya mangi yaliyomkuta Esau katika Maisha yake yalisababishwa na kule kuuza uzaliwa wake wa kwanza. Kwa hiyo watu wasiojua kwamba Esau alishauza uzaliwa wake wa kwanza, ni rahisi kumlaumu Yakobo. Ni muhimu mambo yaliyotokea yakawekwa sawa. Suluhu ya kudumu ikapatikana.

Kanisa kama mzazi na mlezi wa vijana ni lazima linie mamoja, na kuhakikisha linaondoa tofauti zote zinazoleta changamoto miongoni mwa vijana. Ipo sumu mbaya ya matengano na uhasama inaendelea kutafuta njia ya kuvuka kwenda kwenye kizazi kinachofuata. Ninaamini kwa msaada wa Mung una kwa kuunganisha maombi na jitihada za pamoja hatutaruhusu Watoto wetu wakaingia kwenye magumu tuliyopitia.  Ni wito wangu kwa maaskofu wote, wachungaji wote na kila aliye na nafasi katika kanisa la Mungu lililo hai, kwamba tujitoe kuangalia mstakabali wa kanisa la kesho.

Haitoshi kujaza makanisa leo, na kupata sadaka za kutosha leo, na kufurahia mafanikio leo; yatupasa kuiangalia kesho. Uamsho endelevu ni lazima ujengewe misingi itayorithishwa kizazi hadi kizazi. Wasomi wengi wanajikuta hawana mizizi katika Imani kwa sababu hawakupata watu wa kuwalelea walipokuwa mashuleni. Wengi wamejikuta wakijeruhika kwa sababu ya mambo wanayokutana nayo mashuleni na vyuoni. Kama kanisa tukiamua kuiangalia kesho, migogoro kama hii ya CASFETA haitaachwa tu. Ni lazima iangaliwe kwa ukaribu ili kuwapa Watoto wetu fursa ya kupendana, kutumikiana, na kupendwa na wachungaji wote bila ubaguzi.

Mungu akubariki!

Saturday, 14 November 2020

MAISHA YA UNYENYEKEVU NA TOBA

“Ingawa Bwana yuko juu, amwona mnyenyekevu, Naye amjua mwenye kujivuna tokea mbali” (Zaburi 138:6)

Unyenyekevu ni ile hali ya kukubali kuwa chini hata kama una sababu nzuri za kukaa juu. Ni kukubali kukaa chini ya mamlaka au kanuni au sheria au mfumo Fulani kwa nia ya kujenga. Mtu akikubali kukaa kwenye mamlaka ya Mungu, maana yake ni mnyenyekevu kwa Mungu. Katika hali ya ubinadamu, unyenyekevu umahusishwa sana na umaskini kwani mara nyingi mtu mwenye shida analazimika kujishusha kwa wale wenye navyo ili watoke kwenye shida. Kwenye mazingira ya kazi, wafanyakazi hulazimika kunyenyekea kwa mabosi wao ili waendelee kuwa na kazi; kwenye maswala ya kijeshi pia, wakuu hunyenyekewa na wale walio chini yao.

Unyenyekevu tunaojifunza hapa si huu unaosababishwa na mazingira; hapa tunaangalia unyenyekevu kama tabia ya mwamini inayosababishwa na usafi wa moyo. Hakuna mtu anayeweza kukaa na Mungu bila kuwa na tabia hii. Isaya 57:15 inasema, “Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu.”

Mtu mwenye kiburi na kujiinua hawezi kukaa na Mungu au kuwa juu au kufanikiwa. Mithali 29:23 inasema “Kiburi cha mtu kitamshusha; Bali mwenye roho ya unyenyekevu ataheshimiwe” Nimeona watu wengi wanyenyekevu wakipata heshima sana. Jifunze kwa watumishi wote waliofanikiwa katika Biblia utagundua kwamba hakuna hata mmoja aliyekuwa na kiburi, wote walikuwa wanyenyekevu Mungu akawainua. Hivyo ni lazima sisi kama waamini tujifunze unyenyekevu. Tuwe wanyenyekevu kwa Mungu na kwa watu wanaotuzunguka. Kimsingi, tuwe na maisha ya unyenyekevu.

Unyenyekevu una mambo mengi unafanya katika maisha yetu kama tulivyoona, yaani:

a.       Unatupa nafasi ya kupewa neema na Mungu. Mithali 3: 34 inasema, “Hakika yake huwadharau wenye dharau, Bali huwapa wanyenyekevu neema”

b.      Unatupa kuwa na uhusiano mzuri na wengine: Watu watakuheshimu, utakuwa na ujasiri kwa watu, Watu watakupenda Mithali 15:33 inatuambia, “Kumcha Bwana ni maonyo ya hekima; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu.” Kumbe hakuna heshima bila unyenyekevu kwanza.

c.       Faida kubwa zaidi ni kutupa kukaa na Mungu

 

Unyenyekevu unatupa kuhudumiana: Mtumishi wa Mungu Petro anatuambia, “…Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema. Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.” (1Petro 5:5-7) Unyenyekevu ndio chanzo cha kuinuka au kuinuliwa kwa mtu wa Mungu. Yeyote asiye mnyenyekevu hakika atapingwa na Mungu hata kushushwa chini.

Kunyenyekea chini ya mkono wa Mungu utasababisha Mungu atuinue kwa wakati wake. Neema ya Mungu ipo pamoja na wote wanaonyenyekea. Katika Mathayo 23:12 Yesu anasema, “Na ye yote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa.” Maisha ya kujinyenyekesha ndiyo maisha ya Mkristo. Yesu mwenyewe kama kielelezo chetu alijinyenyekesha hata mauti ya msalaba ndipo sisi tukainuliwa pamoja naye (Wafilipi 2:6-8) Neno linasema, “ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata” (Waebrania 5:8) Baada ya kunyenyekea alikirimiwa jina lipitalo majina yote (Wafilipi 2:9), tena ametufanyia wokovu wa milele hata akatajwa na Mungu kama kuhani mkuu kwa mfano wa Melikizedeki. (Waebrania 5:9)

Hebu tuuangazie macho mfano huu tunaoupata katika Luka 18:10 – 14: “Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru.Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”

Hapa tunaona jinsi ambavyo Farisayo alipata hasara kwa sababu ya kiburi, kujihesabia haki kwa kutimiza taratibu za dini. Yeye alijiona “si kama wengine” ni kweli hakuwa kama wengine lakini haikupasa iwe sababu ya kujihesabia haki. Tunapofanya vizuri au kutimiza majukumu Fulani katika kanisa Mungu anategemea tuendelee kunyenyekea na kuwathamini wengine. Mtoza ushuru yeye alijishusha, akakaa mbali kwa unyenyekevu (alipiga magoti) na kumwomba Mungu akimwambia “uniwie radhi mimi ni mwenye dhambi” Hii ndiyo siri ya kufanikiwa kwake. Mimi na wewe leo tunakwendaje mbele za Mungu? Tunawaonaje wengine ambao hawafanyi kwa viwango kama sisi?

Katika kitabu cha 1Samwel 2:3 tunakutana na maneno haya, “Msizidi kunena kwa kutakabari hivyo; Majivuno yasitoke vinywani mwenu; Kwa kuwa Bwana ni Mungu wa maarifa, Na matendo hupimwa na yeye kwa mizani.” Kumbe Mungu ndiye hupima matendo yetu, hatuna haja ya kujisifia kwayo. Tukiyabeba matendo yetu kama sababu ya kujihesabia haki tutajikuta tumebaki wenyewe, kwani hakuna hata tendo moja linalotosha kulipa gharama ya uhai wetu. Ni vema tukamwishia Mungu kwa unyenyekevu, na shukrani kwa yale aliyotuwezesha kufanya.

Mungu hawezi kumwacha mnyenyekevu: “Naye mnyenyekevu Mungu atamwokoa.” (Ayubu 22: 29). Hata kama unapita katika magumu kiasi gani, ukiendelea kunyenyekea mbele za Mungu kwa moyo uliopondeka hakika Mungu hatakuacha. Daudi alipoona ameanguka, hakuanza kujitetea. Alishuka akamlilia Mungu kwa kuyararua mavazi yake (ishara ya unyenyekevu), na Mungu akamsamehe. Kutenda dhambi kisha ukaficha na kujifanya mtakatifu si Ukristo huo, ni unafiki mbaya, ni kiburi. Ni vema ukajinyenyekesha ukaomba Mungu akusamehe, utakuwa salama.

Angalia mafanikio yasiufanye moyo wako ukainuka ukamsahau Mungu aliyekutoa kwenye utupu na kukubariki (Kumb. 8:11-14). Watu wengi huwa wanyenyekevu wakiwa hawana kitu ila wakifanikiwa wanapoteza heshima kwa Mungu na watumishi wake. Maisha yetu kama waamini hayapaswi kuwa hivi. Tunapaswa kuendelea kunyenyekea hata kama tutabarikiwa kwa kiasi gani. Mungu anataka tutafute pamoja naye, tumiliki pamoja naye, tutumie pamoja naye na tuendelee kuishi pamoja naye hata tukipoteza. Maisha ya Ayubu yanatufundisha somo la unyenyekevu mbele za Mungu.

Maisha baada ya kuokoka ni maisha ya unyenyekevu kwa Mungu, kwa viongozi wa kanisa, kwa watu wanaotuzunguka kulingana na Neno la Mungu. Ndani ya maisha ya wokovu tunapaswa kuwa na mioyo ya toba na unyenyekevu. Kila wakati tuhitaji rehema za Mungu, na kumtii Mungu kutoka moyoni. Tuwape heshima viongozi na kuwasikiliza katika mapenzi ya Mungu. Petro anaagiza na kusema, “ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.”

Unyenyekevu unatupa kuweza kuhudumiana: Katika kanisa sisi ni viungo, kila mmoja na mwenzake; hivyo hatuwezi kuepuka kuhudumiana. Katika unyenyekevu kila mmoja wetu akiwatanguliza wengine, tutahudumiana. Paulo anaeleza jinsi ambavyo amekuwa  “akimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote” (Matendo 20:19) Je, sisi tunatumika kwa jinsi gani? Nabii Sefania anasema, “Utafuteni unyenyekevu” (Sefania 2:3) Huwezi kuwa mhudumu ndani ya nyumba ya Mungu, na ukatumika kwa mafanikio, bila kuwa mnyenyekevu. Jifunze unyenyekevu. Paulo anahitimisha kwa kusema, “Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.” Wafilipi 2:3

 

KUOKOKA NI ZAIDI YA KUONGOKA

Watu wengi wanachanganya maana ya maneno haya kwa nia ya kutetea imani zao potofu.  Baada ya kulichambua kwa kina swala wokovu (kuokoka), hebu sasa tuone utofauti uliopo kati ya wokovu na swala la kuongoka. Baadhi ya madhehebu ya kikristo, hudai kwamba kuongoka ni sawa tu na kuokoka. Kiuhalisia haya ni maneno mawili tofauti kabisa katika Imani. Tukisema mtu ameongoka hatumaanishi ameokoka, japo kuna mazingira ambayo yanaweza kuleta maana hiyo. Hebu angalia tafsiri zifuatazo kutoka kwenye biblia ya Kingereza:

... declaring the CONVERSION of the Gentiles: and they caused great joy unto all the brethren (Acts 15:3 KJV) Kiswahili chake kinasema, wakitangaza habari za kuongoka kwao Mataifa; wakawafurahisha ndugu sana. Katika mazingira haya neno kuongoka linaweza kuwa na maana sawa na kuokoka kwa sababu wamataifa walitoka kwenye miungu yao na kugeuka kupitia Injili ya kweli iliyohubiriwa na Paulo na Barnaba.

But I have prayed especially for you [Peter], that your [own] faith may not fail; and when you yourself have turned again, strengthen and establish your brethren. (Luke 22:32 AMP) Mstari huohuo katika tafsiri nyingine unasomeka, But I have prayed for thee, that thy faith fail not: and when thou art converted, strengthen thy brethren. (Luke 22:32 KJV) Neno Conversion limetafsiriwa kama kubadili mfumo au matumizi ya kitu (kikawaida), ila kidini ni kule kubadili dini au Imani mfano kutoka Uislamu kwenda Ukristo.

 Katika mstari huu unaomzungumzia Petro, neno kuongoka limetafsiriwa kama to have turned again likimaanisha kujirudi au kurejea upya. Kwenye (KJV) – limeandikwa - art converted likiturudisha kwenye neno la kwenye Matendo 15:3. Katika Luka 22:32 Yesu anamwambia Petro “lakini nimekuombea wewe (Petro) ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.

Kwa hiyo neno kuongoka linaweza kuwa ni kule kuingia au kuhamia tu kwenye dini fulani, au kubadili imani (kutoka imani moja kwenda nyingine) bila kuleta maana sawa na neno kuokoka/kuokolewa (Saved) – linalomaanisha kutolewa kwenye maangamizo au hali ya uharibifu na kuwekwa kwenye usalama. Au kutolewa kwenye mauti (mshahara wa dhambi), nguvu za giza, na utumwa wa dhambi; na kuingizwa kwenye ufalme wa Mungu (maisha mapya ndani ya Kristo Yesu). Au kutengwa na dunia kwa ajili ya ufalme wa Mungu katika Kristo Yesu.

Kama tulivyoona kwamba kuokoka ni mpango wa Mungu wa kumtoa mwanadamu kwenye dhambi na mikono ya shetani (Mautini) na kumweka penye uzima (katika ufalme wake). Kuokoka ni zaidi ya kuongoka, mtu akiokoka maana yake amemwamini Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yake ila akiongoka anaweza kuwa amebadili tu msimamo au dini huku akiwa hajamkiri Yesu.

Kwa kifupi neno kuongoka ni neno la kidini, bali Kuokoka ni Imani kwa Mungu kupitia Yesu Kristo. Ndiyo maana Yesu hakututuma kuwahubiri watu habari za dini ili waongoke, bali habari za Ufalme wake (Injili) ili waamini na kubatizwa – waokoke. Marko 16:16 Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Kwa hiyo kuokoka ni zaidi ya kuongoka. Neno la kingereza linalotumika kwenye neno ataokoka si converted bali ni saved. Whoever believes and is baptized will be saved -  (Mark 16:16 NIV).

Wanafunzi wa Yesu (mitume) walipotumia neno kuongoka, inawezekana walimaanisha kuokoka kwa sababu watu walikuwa wanatoka kwenye dini ya kiyahudi au kwenye upagani au kwenye miungu yao na kuingia kwenye kanisa la Kristo ambapo hapakuwa na madhehebu kama ilivyo sasa. Kimsingi, kuingia kwenye dini si kuingia kwenye wokovu, japo ukishaingia kwenye wokovu ni lazima uwe na mahali pa kuabudu pamoja na waamini wenzako. Kuongoka kunakotokana na Injili ya kweli ya Yesu Kristo ndiko kuokoka.

Kazi iliyomtoa Yesu mbinguni na kuja duniani, hata kupata mateso ni kutafuta na kuokoa kile kilichopotea. Luka 19:10 inasema "Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea." Kuokoa ni kulipa gharama ya upotevu wa mtu. Yesu alifanyika fidia ya dhambi za wanadamu wote. Tunapotubu na kumwamini Yesu kama Mungu, na Bwana katika maisha Yetu tunaingia katika usalama wa milele. Neno linasema, "Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake (Wakolosai 1:13). Wokovu upo ndani yake Kristo.

Tuesday, 7 April 2020

JIANDAYE KUTOA HESABU


 SIKU YA HUKUMU, KILA MMOJA ATATOA HESABU YA UTUMISHI WAKE.
(Each of us will give an account of oneself on the Day of Judgment)

“Iangalie sana huduma ile uliyopewa katika Bwana, ili uitimize. (Wakolosai 4:17).

Huduma katika kanisa la Mungu ni kazi ya kila kiungo. Japo vipo viungo vilivyopewa heshima zaidi ya vingine. Paulo anasema, “Basi katika nyumba kubwa havimo vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali na vya mti, na vya udongo; vingine vina heshima, vingine havina.” (2 Timotheo 2:20) Vyombo vyote hivi havikujileta vyenyewe ndani, vililetwa na mwenye nyumba akiwa na kusudi kwa kila kimoja. Vya dhahabu japo ni vya thamani zaidi ya vingine havitatumika maeneo yote; kuna maeneo tunahitaji vya udongo, kwingine vya mti au vya fedha. Mwenye nyumba ndiye anayejua thamani na matumizi ya kila kimoja.

Ndivyo ilivyo kwa kanisa la Mungu; kila aliyeokoka ni chombo na ameitwa kwa jinsi yake. Anaweza akawa chombo cha dhahabu (wenye karama na vipawa zaidi), au cha fedha (Wenye wito Fulani), au cha mti au cha udongo (washirika na wenye karama zinazoonekana kibinaadamu kwamba hazina thamani). Sijui mimi na wewe ni vyombo vya aina gani, ila ninachojua ni kwamba sote tu vyombo vya Bwana. Katika kitabu cha Warumi 4:08 Paulo anatueleza juu ya kitu alichokifanya Yesu alipoinuliwa: anasema, “Alipopaa juu aliteka mateka, Akawapa wanadamu vipawa.” Kisha akavitaja: “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe”

Hapa neno linatuweka wazi kwamba kusudi la Mungu kuwapa watu vipawa ni ‘kazi ya huduma itendeke na mwili wa Kristo (kanisa) ujengwe” Hili ndilo lengo kuu, hivyo mtumishi yeyote anayefanya kinyume na hayo ni mharibifu. Kama amekuwa kwazo kwenye kazi ya huduma au anaubomoa mwili wa Kristo (kanisa) huyo ni mchungaji au mtumishi aliyepoteza sifa kabisa. Sifa mojawapo ya mtumishi ni kuwa mtendakazi mwenye uchungu na kondoo (kazi). Ni lazima aone wale kondoo (watu) anaowatumikia kama mali yake (japo si mali yake). Awapende na awatumikie kwa upendo.

Warumi 12:4-14
Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja; Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake. Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake; mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu, kwa furaha. Pendo na lisiwe na unafiki lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema. Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu; kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana; kwa tumaini, mkifurahi; katika dhiki, mkisubiri; katika kusali, mkidumu; kwa mahitaji ya watakatifu, mkifuata ukarimu; katika kukaribisha wageni mkijitahidi. Wabarikini wanaowaudhi; barikini, wala msilaani.

Mistari hii inatuweka wazi zaidi juu ya utofauti wetu katika kazi ya Mungu na jinsi ambayo tunaweza kuzitumia tofauti hizo kutumikiana kwa utukufu wa Mungu. Paulo anasema ‘sisi ni kama viungo katika mwili’ na tunapaswa kufanya kazi katika pendo lisilo na unafiki, tena kwa bidii tukiwatanguliza wengine. Mtumishi wa Mungu anapokwenda kinyume na kanuni hizi alizoziweka Mungu, moja kwa moja anakuwa mharibifu. Ona Paulo anavyosema tena: “ili kusiwe na faraka katika mwili, bali viungo vitunzane kila kiungo na mwenziwe.” (1 Wakorintho 12:25)

Kila mtumishi aliyeitwa na Mungu haijalishi ni mtume au nabii au mchungaji au mwinjilisti au mwimbaji au mwingine yeyote, ni kiungo kimoja katika mwili wenye viungo vingi. Ni chombo miongoni mwa vyombo vingine. Ni (mtumishi) mtumwa wa Kristo miongoni mwa watumishi wengine. Paulo anasema tena, “Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake. (Waefeso 4:25). Kwa hiyo hakuna jinsi ambavyo mtumishi awaye yote anaweza kudai kwamba yeye yuko juu ya wengine au mkuu kuliko wengine; akifanya hivyo anakuwa mharibifu.

Kwa utangulizi huu mfupi nasimama kwa ujasiri wote kukuambia wewe mtumishi mharibifu: Ole wako, tena narudia Ole wako, usipotubu na kugeuka Ole wako. Yeremia alitabiri akasema, “Ole wao wachungaji, wanaoharibu kondoo za malisho yangu na kuwatawanya! Asema Bwana.” (Yeremia 23:1) Hapa Mungu alikuwa anazungumza juu ya watu wake Israeli. Na mimi juu ya kanisa la Kristo niseme, “Ole wako mchungaji au mtumishi yeyote unayewaharibu kondoo wa malisho ya Mungu (kanisa) na kuwatawanya! Utakuja kutoa hesabu. Usijitie moyo kama sifa unazopewa na watu, usifurahie kusanyiko kubwa linalokujia, usiangalie hiyo fedha ya aibu unayojikusanyia ukajiona mjanja! Kiburi chako kitashushwa hakika! Hata ukiharibu sasa, hautaharibu milele. Geukaaa!
  •           Wewe unayefundisha mafundisho ya uongo ili kujikusanyia watu kwa hila: Ole wako!
  •       Wewe unayeshika mapokeo ya dini na kuikataa kweli ya Mungu: Ole wako!
  • -          Wewe unayejiita nabii wa Mungu huku ukijua kuwa wewe ni mchawi na mshirikina: Ole wako!
  • -          Wewe unayewadanganya watu wa Mungu na kujikusanyia fedha ili kujishibisha mwenywe badala ya kuujenga mwili wa Kristo: Ole wako!
  • -          Wewe uliyegeuza nyumba ya Mungu kuwa pango la wanyang’anyi kwa kuuza kipawa cha Mungu: Ole wako!
  • -          Wewe unayefanya mzaha na kazi ya Mungu, na kuwavunja wengine moyo, na umeshupaza shingo ukijifaanya husikii maonyo: Ole wako!
  • -          Wewe uliyejiinua juu na kujipa utukufu mwenyewe, ukilitangaza jina lako kuliko jina la Yesu: Ole wako! Mungu atakapokuangusha, hutainuka tena.
  • -          Wewe unayelichezea Neno la Mungu, kwa kulichanganya na uongo, ukiwafurahisha watu kwa unafiki, utaunywa uchungu wa unafiki wako: Ole wako!
  • -          Wewe unayejiita Mkuu, na kujipa majina makubwa, huku ukiwanyanyasa watu, na kuwalaghai, kazi yako inanuka mbele za Mungu, hutafika mbali: Ole wako usipogeuka na kutubu.
  • -          Wewe unayejisumbukia huku ukivutwa na tamaa ya mali, tamaa ya mwili na kiburi cha uzima, na kusahau wito ulioitiwa, mali zimekuwa Mungu wako, umekataa kumtii Mungu kwa sababu ya tumbo: Ole wako!
  • -          Yesu anasema, “Hakuja kuleta amani duniani, alikuja kuleta upanga! Wewe nabii unapata wapi amani ya kujistarehesha na anasa, kula na makahaba na wazinzi, umepata wapi nafasi hiyo! Ole wako!
  • -          Ole wako unayelinajisi kanisa la Mungu kwa uzinzi na uasherati, jina lako linanuka mbele za Mungu. Unazini na wale unaowatumikia, Ole wako!
  • -          Ole wako mchungaji mvivu na mzembe, unaowaacha kondoo wakitaabika; na wewe unazurura mitaani kutafuta mali, hakika utatoa hesabu.
  • -          Kazi ya Mungu inafanyika kwa mazoea, mizaha imepanda mpaka madhabahuni, uhuni umejaa, ukahaba umelitawala kanisa na wachungaji mmenyamaza: Ole wenu!
  • -          Heri yao waliokubali kuonekana wabaya, wakapiga kelele juu ya ukahaba! Kanisa la Mungu limechubuka, linavuja damu. Wachungaji wanachekelea mapato, na kujenga majumba makubwa! Huu ni msiba, manabii wa kweli mko wapii? Mitume mko wapi? Waalimu mbona mmenyamaza? Wainjilisti hamwoni shetani akikokota roho za watu Jehanamu? Waimbaji mnaimba nini? Ni nani aliyewaita? Baba yenu ni nani?
  • -          Heri yako wewe ulichagua kufa kwa ajili ya Haki, heri yako uliyeamua kubaki maskini wa mali huku ukiihubiri kweli ukimngoja Mungu akukweze kwa wakati wake. Ujapokuwa maskini, unawatajirisha wengi katika ufalme wa Mungu.
  • -          Heri yako unayelia juu ya uharibifu unaoendelea juu ya dunia; heri yako ambaye moyo wako umeja huruma unapowatazama wajane, mayatima, maskini, wenye njaa, omba omba barabarani, wakimbizi, wafungwa, wagonjwa na wanaoteseka katika dhambi; Mungu wetu ni mwenye huruma, hakika atakukumuka.

Huu si wakati wa kutafuta umaarufu, si wakati wa kufanya maigizo madhabahuni, si wakati wa kutafuta vyeo, si wakati wa kung’ang’ania madhehebu, si wakati wa kupasuka pasuka na kujitenga na wengine, si wakati wa kuoneana wivu, si wakati wa kugombana watumishi, si wakati wa kujiona bora kuliko wengine; ni wakati wa kudhihirisha kufa kwetu pamoja na Kristo, ni wakati wa kuyatafuta mapenzi ya Mungu na kuyatenda. Yesu yu karibu kurudi kulichukua kanisa lake. Ni wakati wa kuliandaa kanisa kwa ajili ya unyakuo.

Ni nyakati za mitume kusimama kama mitume katika mapenzi ya MUNGU, manabii kusimama kama manabii katika mapenzi ya Mungu, na wachungaji nao vivyo hivyo, wainjilisti, waalimu, viongozi, waimbaji nawengine wote vivyo hivyo. Kanisa si majengo, ni kusanyiko la watu waliotengwa kwa ajili ya kusudi la Mungu. Wewe unayeng’ang’ania kumiliki kanisa mwenyewe, pole! Wewe unayeng’ang’ania dhehebu linalomkataa Yesu na kufundisha uongo, pole: Wewe ni mtumishi wa shetani, na shetani ndiye baba yako. Huwezi kuwa mtumishi wa Mungu huku wewe ni mlevi, mzinzi, mwalimu wa uongo, mnafiki, msengenyaji, mla rushwa, mkatili, na mengine kama hayo; hakika huwezi.
          Nabii Ezekieli aliambiwa atoe unabii juu ya Wachungaji (viongozi, watumishi) wa watu wa Mungu Israeli. Neno linasema, “Mwanadamu, toa unabii juu ya wachungaji wa Israeli, toa unabii, uwaambie, naam, hao wachungaji, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wachungaji wa Israeli, wanaojilisha wenyewe; je! Haiwapasi wachungaji kuwalisha kondoo?” Jambo hili ni jambo la kusikitisha sana; yaani wachungaji kujilisha wenyewe na kusahau kulisha kondoo. Ubinafsi wa namna hii ndio uliolivamia kanisa la nyakati za leo, hasa kanisa lililo Afrika. Matumbo yetu yamekuwa makubwa kiasi cha kutupofusha tusione mateso ya kondoo tuliopewa kuwachunga. Mahitaji yetu yametufanya viziwi tusiweze kusikia vilio vya kondoo wanaotaabika katika nyika wasione wa kuwapa hata tone la maji.

            Paulo akiwa katika Roho Mtakatifu, aliongea katika hali ya huzuni kubwa juu ya watu wanaohubiri Injili ya namna nyingine na kuipotosha kweli ya Mungu. Alisema, “Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe.” Tena akarudia kwa mkazo zaidi akasema, “Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe.” (Wagalatia 1:8-9) Wewe nabii na mwalimu wa uongo, laana hii huwezi kuiepuka! Labda uamue leo kutubu na kuamua kuihubiri iliyo Kweli. Ninajua nafsi yako inakushuhudia kitu juu ya hayo unayofundisha. Wewe unayefundisha ili upate mali na kulishibisha tumbo, ole wako.

            Ujumbe huu umekujia ili usiwe na la kujitetea mbele za Mungu. Biblia unayoichezea kwa kuitafsiri kama unavyotaka au kwa kusukumwa na Ibilisi uliyeamua kumtumikia, iliandikwa kwa machozi na damu. Mitume walikubali kuteswa hata kuuawa wakiitetea Imani ya kweli. Leo hii unasimama, unajiita nabii, mtume, mwalimu au hata mchungaji, kumbe ni mwigizaji, mlaghai na mjumbe wa shetani; hakika hutafika mbali. Jiulize leo umeua wangapi na uongo uliofundisha! Angalia vilio ulivyosababisha kwa sababu ya tamaa yako ya fedha. Watu wanakufa kwenye dhambi, huku ukujitajirisha na kuona fahari. Unatabiri uongo hata wewe mwenyewe unajua! Saa yaja na sasa ipo, utakaposimama mbele ya kiti cha hukumu kutoa hesabu mbele za Mungu. Sijui utajibu nini!

            Mtume Yakobo anaonya na kusema, “Ndugu zangu, msiwe waalimu wengi, mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi.” (Yakobo 3:1) Leo kila mtu anajiita nabii, mwalimu, mchungaji, mtume na mengine, wakifikiri ni sifa. Kumbe ni msalaba, huduma si ufahari. Huduma ni msalaba, ni kushiriki mateso pamoja na Kristo. Ufahari wetu u katika Kristo. Tukiishi tunaishi pamoja naye, tukifa tunakufa pamoja naye, tukiudhiwa tunaudhiwa pamoja naye, tukitukanwa na kukakataliwa tunakuwa pamoja naye! Hii ndiyo fahari tuliyonayo. Magari, majumba, fedha na vyote vya ulimwengu huu ni ziada kwetu. Ufalme wa Mungu ndio kipaumbele chetu.
          Mwisho niseme, “Watumishi wenzangu, “tukiwa tumefufuliwa pamoja na Kristo tuyatafute yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Tusikubali kuwa na majina ya kuwa hai kumbe tumekufa, tung’ang’anie uhai wetu katika Kristo. Tuwe watu wa kujichunguza kila siku tukijikumbusha kama Paulo alivyojisema, “bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.” (1Wakorintho 9:27) Tena tukatae kulichanganya Neno la Mungu nauongo. Tusiwe watu wa kupenda fedha ya aibu, tutumike kwa uaminifu hata kufa. Tuungane na mtume Paulo tena katika maneno haya:
 “Kwa sababu hiyo, kwa kuwa tuna huduma hii, kwa jinsi tulivyopata rehema, hatulegei; lakini tumekataa mambo ya aibu yaliyositirika, wala hatuenendi kwa hila, wala kulichanganya neno la Mungu na uongo; bali kwa kuidhihirisha iliyo kweli twajionyesha kuwa na haki, dhamiri za watu zikitushuhudia mbele za Mungu.” (2 Wakorintho 4:1-3)

            Neno linasema,Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka. (1 Petro 5:4) Naye Mungu antayafuta machozi yetu tukishaondoka katika ulimwengu huu. Tusikubali kubaki na miujiza, kunena kwa lugha na matendo ya Imani huku tukiwa hatuna upendo wa kweli na Mungu. Yesu anasema, “Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu. Usijitie moyo na miujiza, angalia mahusiano yako na Mungu zaidi ya miujiza. Angalia usije ukapata hasara ya nafsi yako! Utumishi si tiketi ya kuingia mbinguni. Ni lazima tuwe watakatifu.

Ifike mahali kuishi kwetu kuwe ni Kristo. Na tuwe watakatifu kama Mungu wetu alivyo mtakatifu. Tusitumike kwa hila, bali kwa adili tukimzalia Mungu matunda kwa utumishi uliotumika. Tusiwe kwazo la namna yoyote ili utumishi wetu usilaumiwe, bali kwa kila jambo tujipatie sifa njema (2Wakorintho 6:3-4). Tukubali kuwa Nuru ing’aayo gizani, tukikataa kila lililo baya. Tusiwe rafiki wa dunia (tusiipende), bali tuzidi kuimarisha uhusiano wetu na Mungu kila siku (1Yohana 2:15) Tuepukane na tamaa za mwili, tamaa za macho na kiburi cha uzima. Tuimarike katika uchaji, na unyenyekevu wa kweli. Tukiyaishi mafundisho yetu, na kumtambulisha Yesu tuliyembeba kwa ujasiri. Huu ndio utumishi utakaotupa heshima mbele za Mungu (Yohana 12:26) Tunapaswa kuimarika katika Imani, kisha tuzidi sana kuitenda kazi ya Mungu (1Wakorintho 15:58), hakika taabu yetu haitakuwa bure.

Ni mimi mtumishi mwenzako nikibubujikwa na machozi kwa ajili ya kanisa la Mungu. Nakutakia neema na uwezezo kutoka juu katika kuyatenda mapenzi ya Mungu. Upendo wa Mungu, na ushirika wetu katika Roho Mtakatifu uzidi kudumu daima. Mwokozi wetu Yesu adhihirike kwako kwa matendo makuu. Huduma yako iliyokuwa imenyauka ichanue tena kama mti wakati wa masika. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na ikae pamoja nawe. Amina.


Na: Mwl. Stephen M. Swai
AMKA GOSPEL MINISTRIES INT’L
Simu: +255 713 511 544


MWANAUME KWENYE NAFASI YA "MUME"

Mume ni mwanaume aliyeoa kwa kuzingatia vigezo na taratibu za kijamii, kishria na za kiroho. Mume si rafiki wa kiume (boyfriend), hawara, wa...

Powered By Blogger