Mume ni mwanaume aliyeoa kwa
kuzingatia vigezo na taratibu za kijamii, kishria na za kiroho. Mume si rafiki
wa kiume (boyfriend), hawara, wala si mzazi mwenza (kwamba tu umezaa naye). Ili
mtu awe mume ni lazima akamilishe taratibu za kijamii, za kisheria na za kiroho
katika kuanzisha ndoa.
Ndoa kibiblia, ni muunganiko wa
kudumu kati ya mtu mke na mtu mume; na mwanzilishi wa muunganiko huu ni Mungu
mwenyewe. Katika Mithali 19:14 tunasoma, “Nyumba na mali ni urithi apatao
mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana.” Hivyo, katika
kuanzishwa kwa ndoa kibiblia ni lazima Mungu ahusike. Tangu Agano la kale hata
sasa, tunaona Mungu akihusika kwa ukaribu sana kwenye ndoa. Ndoa ya kwanza
aliifunga mwenyewe kati ya Adam una Eva.
Ibrahimu alipewa Sara kuwa mkewe,
Isaka alipewa Rebeka kuwa mkewe, Yakobo alipewa Lea na Raheli kuwa wake zake.
Hata kama walijihusisha na wanawake wengine, bado hawa walibaki kuwa na nafasi
ya pekee kwao. Kwa hiyo, kuwa mume kwa mke si jambo rahisi na la kawaida, ni
jambo lenye kusudi la Mungu ndani yake.
Ukifuatilia ndoa hizi niliziozitaja
utagundua kwamba familia zilihusika kwa ukaribu sana katika kuianzisha ndoa.
Mfano Rebeka aliulizwa na wazazi wake kama yuko tayari kuambatana na yule
aliyetumwa kuja kumchukua. “Wakamwita Rebeka wakamwuliza, Je! Utakwenda na
mtu huyu? Akasema, Nitakwenda.” (Mwanzo 24:58) Sheri ana kanuni za jamii
zao nazo zilizingatiwa kwa karibu sana.
Maagizo ya Mungu kwa Mume
i.
Kuambatana na Mkewe
Makubaliano kati ya mwanaume na
mwanamke katika mahusiano siku zote yamekuwa yakizingatiwa. Tangu zamani iliwalazimu,
mwanaume na mwanamke kukubali kuambatana pamoja. Kibiblia, mume ni lazima
aambatane na mkewe na kumpokea kama sehemu ya mwili wake (Mwanzo 2:24, Waefeso
5:31, Mathayo 19:5). Tangu uumbaji, mwanamke ni sehemu ya mwili wa mwanaume.
Mungu aliuchukua ubavu mmoja wa Adamu
na kumuumba Eva. Naye Eva alipoletwa kwa Adamu, kwa furaha, na kwa kumkubali
Adamu lisema, “Sasa huyu ni mfupa katika mifupa
yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa
katika mwanamume.” Kule kutolewa katika
mwanaume ndiko kulikomfanya Eva aitwe mwanamke.
Mwanaume akimwona mkewe
katika mtazamo huu ni rahisi kuambatana naye. Kuambatana kunahusu mambo yote
katika Maisha: yaani kimwili na kiroho. Mume hana maisha binafsi tena, kila
kitu ni shirika. Kwa kukazia Zaidi Paulo anasema, “Mke hana amri juu ya
mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali
mkewe.” (1 Wakorintho 7:4)
Kuambatana kati ya mume
na mke, ni kwa lazima. Japo changamoto ni kubwa katika kizazi hiki, inawezekana
kuliko vizazi vyote. Ile neno aliloambiwa Eva kusema “tamaa yako itakuwa kwa
mumeo, naye atakutawala.” Limekuwa gumu kwa wanawake walio wengi. Hivyo
mashindano, chuki, na kutendeana kwa hiyana kumetawala kati ya wanaume na
wanawake.
Kuambatana ni jambo pana
katika Maisha ya wanandoa. Mume ni
lazima akubali na ajitoe:
Kuambatana na mkewe katika
kuhudumiana, huku kunahusisha kujitoa
kwa kila mmoja kwa mwenzake. Huduma ya tendo la ndoa ni moja ya huduma za
msingi katika ndoa. Paulo anasema, “msinyimane” (1 Wakorintho 7:5).
Kuhudumiana kiroho na kimahitaji na mengineyo pia ni sehemu ya kuambatana kwa
wanandoa.
Kuambatana na mkewe katika
kazi; huku ni kuunganisha mikono pamoja
katika kuzalisha. Kazi za nyumbani, za kiuchumi, za kanisa na nyinginezo ni lazima
zifanyike katika ushirika wa mume na mke katika ndoa. Mke n msaidizi, mume ni
mwongoza njia. Wote wawili ni wasafiri katika chombo kimoja kiitwacho ndoa au
familia. Kutiana moyo, kusaidiana, kuwezeshana, na kupeana nafasi katika kazi
katika kuambatana hakuepukiki.
Kuambatana na mkewe katika
mapato na matumizi; hili ni eneo linalohusu
uchumi katika ndoa. Kimsingi uchumi wa ndoa hujengwa na mume na mke, hivyo wote
ni lazima wahusike vilivyo katika kupata na kutumia mali zinazozalishwa. Japo
jukumu la kuzalisha amepewa Adamu, Eva hawezi kujiweka pembeni kwani naye ni
msaidizi. Na Zaidi ni mwili mmoja na Adamu.
Kuambatana na mkewe katika
huduma na maisha ya kiroho (kiimani): Imani hubeba hatima ya mwanadamu. Tena huathiri maamuzi ya mtu moja kwa
moja. Ikitokea mke na mume hawako pamoja kiimani au kihuduma, kuambatana huwa
kugumu. Mume ni lazima akubali kuambatana na mkewe katika mambo ya kiroho ili
wawe na hatima njema, vivyo hivyo na mke. Maombi, kusoma neno, utoaji,
kutumika, na kumtafuta Mungu kwa pamoja ni msingi wa Maisha ya kiroho katika
ndoa.
Kuambatana na mkewe katika
malezi ya watoto (kabla na baada ya kuzaliwa): huku kunahusisha kupanga idadi ya watoto, aina ya malezi ya kuwapa
watoto, jinsi ya kukidhi mahitaji ya Watoto, na jinsi ya kutunza maadili ya
familia. Mambo haya hayawezi kufanyika
kwa ufanisi bila maridhiano na maamuzi ya pamoja. Mume bora ni yule anayeweza
kusafiri salama akiwa bega kwa bega na mkewe pamoja na Watoto.
Kuambatana na mkewe katika
mipango (iweni na nia moja) na kukuza uchumi wa ndoa na familia: katika ndoa ni lazima kupanga pamoja. Mume atoe mawazo
yake, mke naye atoe yak wake. Ndoa iliyogawanyika mara nyingi, huanzia kwenye
mipango. Mipango ikishatofautiana, matumizi hayawezi kwenda sawa.
Kushirikishana mipango ni njia muhimu katika kudumisha kuambatana. Mume ni
lazima amshirikishe mkewe mipango yote aliyonayo.
Mume pia ana jukumu kuambatana
na mkewe katika matatizo mfano magonjwa, misiba na mengineyo. Mwanaume
anayekimbia matatizo, hana sifa ya kuwa mume. Kuoa ni kukubali kuchukua
madhaifu ya mke, na kumshirikisha mke udhaifu wako. Kutafuta suluhu ya matatizo
ni moja ya jukumu la msingi la mume katika ndoa.
Mungu ni lazima aambatane
na mkewe katika kusaidia ndugu na kuwatunza wazazi. Japo hili linakwenda
kwa pande zote mbili, ni lazima mume awe mstari wa mbele kuwasaidia ndugu wa
mkewe. Kuambatana kunadai kubebeana mizigo. Katika familia zetu za kiafrika
tuna majukumu Fulani ambayo hatwezi kuyaepuka, hivyo kusaidiana ni kwa lazima.
Haya ni baadhi ya maeneo
ya msingi, yanaweza kuwepo mengine zaidi. Jambo la msingi hap ani kujua kwamba
kuwa ‘mume’ ni kuwa mshirika wa karibu na wa pekee kwa mkeo. Mke
ameumbwa kufurahia ushirika na kujaliana katika mahusiano. Hajaumbwa kupambana
peke yake, hivyo kuambatana naye ni njia muhimu katika kujenga amani ya ndoa.
Mume naye hawezi peke yake, hata Adamu
yalimshinda, hivyo ni lazima mke akubali kuambatana na mumewe.
ii.
Kumpenda Mkewe
Paulo anasema, “Vivyo
hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye
mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote;
bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. (Waefeso 5:28-29)
Hapa Paulo anasema juu ya kuwapenda
wake zetu kama miili yetu, hili ni fumbo zito kwa mume. Waume wote tungeweza
jambo hili, ndoa zetu zingekuwa paradiso. Kizazi chetu kinashangaza sana, kwani
kesi za waume kuwapiga, kuwaumiza, kuwaacha, wakati mwingine hata kuwaua wake
zao zimekuwa nyingi sana. Paulo amatuambia “haiwezekani mtu akauchukia mwili
wake. Bali huchukua jukumu la Kuulisha na kuutunza.
Kutokea kwa matukio haya mabaya
kunadhihirisha kwamba wanaume wengi hawajawapokea wake zao kama miili yao
wenyewe au hawana upendo wa kweli kwa wake zao. Mume aliyempokea mkewe kama
mwili wake na kumpenda ni lazima awe na upendo ulio hai. Yaani:
v
Upendo kwa mkewe huambatana na
kuhakikisha kwamba anakula na anapata mahitaji yake yote (matunzo). Hata kama ana kazi yake usikubali mkeo akajigharamikia kila kitu, tumia
fedha yako kumlisha na kumnunulia mahitaji yake. Kumjali mke kimahitaji ni
jukumu la msingi la manaume. Mume ni lazima awe na macho ya kuona mahitaji ya
mkewe.
Si lazima mke aombe kila kitu. Vitu
vingine ukiona anavihitaji mnunulie naye atajisikia kupendwa kila wakati. Kama
mume unayempenda mkeo, hupaswi kuishia kwenye maneno tu, ni lazima upendo wako
uambatane na kujali mahitaji. Ukumbuke kabla ya kumwoa mkeo alikuwa anapewa
mahitaji na wazazi wake na pengine wanaume wengine, au kujihangaikia mwenyewe.
Hakikisha unazipa mapengo yote kwa kufanya Zaidi ya wote.
v
Upendo unadai kujitoa: Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda
Kanisa, akajitoa kwa ajili yake. (Waefeso 5:25). Kujitoa ni kwenda
Zaidi ya ile hali ya kawaida ya kutimiza majukumu. Unapofika mahali kama mume
ukatafuta muda wa ziada, ukafanya zaidi, ukakubali kuumia kwa sababu ya mkeo
basi unakuwa unautimiza upendo.
Linapotokea jambo gumu kwa mkeo, hakikisha unakuwa mstari wa mbele kama
mume kutafuta utatuzi. Hata kama litakugharimu kupoteza baadhi ya vitu, Mungu
atawajalia neema mtapata vingine baada ya jambo hilo kupita. Kazi zipo tu, ila
kujitoa kumsaidia mwenzako wakati wa taabu au hata mazuri yenye gharama ni
muhimu.
NiIisikia habari za kijana mmoja (mume) ambaye alimwacha mkewe
hospitalini akiwa mahututi kwa sababu ya kuogopa hasara ya kazi aliyokuwa
anaifuatilia. Mkewe alipotoka hospitalini, alikuwa na uchungu mwingi sana kwa
kuona mumewe amethamini kazi kuliko Maisha yake. Kurekebisha kosa kama hilo, ni
gharama kubwa kuliko kuacha faida ikapita.
v Upendo unadai kusamehe na kusahau:
Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao. (Wakolosai 3:19)
Wanaume wasio na moyo wa kusamehe mara nyingi huwatendea wake zao mabaya.
Upendo hauhesabu mabaya (1 Wakorintho 13:4 “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo
hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti
mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya”
Hivyo, mume mwenye upendo ni lazima
ajifunze kumsemehe mkewe. Ni muhimu kukumbuka wamba, wanawake ni watu wa
mahusiano zaidi kuliko kazi, hali wanaume ni watu wa kazi zaidi. Kupishana
katika mazingira kama haya ni kawaida. Wanawake huwa hawapendi kukosea, hivyo
kusamehewa wakikosea ni lenye nafasi kubwa kwenye maisha yao.
v
Upendo unadai heshima: Paulo anafundisha na kusema, “Kadhalika
ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo
kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba
kwenu kusizuiliwe. (1 Petro 3:7). Mume ana jukumu la kuitunza heshima ya
mkewe kwa kumvisha vizuri, kumpamba, kumwendeleza, kumpa nafasi na kumsikiliza.
Kwa sababu ya maumbile yao au hali ya maisha au historia wakati mwingine
mke anaweza kuonekana kama hana heshima. Kwa mume, mke ni lazima awe malikia
katika hali zote. Mume hatakiwi kumvunjia mkewe heshima, kwa kwenda nje ya
ndoa, vivyo hivyo mke. Kama mume, ni muni kuyaheshimu mawazo ya mkeo, hisia
zake, na nafasi yake kwa ujumla.
v Upendo unaambatana na kumlinda mkeo: Kwa
hiyo jihadharini roho zenu; mtu awaye yote asimtende mke wa ujana wake mambo ya
hiana. (Malaki 2:14-15) Wanapoinuka watu kumshambulia mkeo usinyamaze,
usiwape ndugu (wazazi, wadogo zako, dada zako au marafiki) kumshambulia mkeo.
Katika changamoto zote, tunza heshima ya mkeo (chukua aibu yake, na Mungu
atakubariki). Zaidi sana usimgeuke na kumtendea mambo ya hiana. Mweke mkeo
kwenye mzingira salama, na hakikisha anakuwa salama wakati wote.
Kila mwanamume au mwanamke anapaswa
kutunza heshima ya ndoa: Ndoa na iheshimiwe na watu
wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu
atawahukumia adhabu. (Waebrania 13:4) Usafi wa ndani na wa nje ni muhimu katika
ndoa. Usafi wa tabia ni wa muhimu zaidi sana. Tabia za uzinzi na uasherati
zimeharibu mahusiano ya wanadoa wengi, na yameleta aibu isiyofutika.
Mambo ya kufanya kama mume ili mkeo akufurahie
Pamojana maagizo haya makubwa mawili
tuliyokwisha kuyaona, kuna mambo kadhaa ya kiutendaji yatakayomfanya mume awe
mtu wa kutamanika kwa mkewe kila wakati.
1.
Fanya
kazi kwa bidi ili kukidhi mahitaji ya familia, kwa kiwango chako. Mke hujisikia
salama akiwa na mume mpambanaji na anayezalisha.
2.
Timiza
wajibu wako kwa jamii, mfano kanisani au kazini au pale unapoishi. Mke
hujisikia vizuri sana akiona mumewe anaheshimiwa na kusemwa vizuri na watu.
3.
Jifunze
kumpongeza mkeo akifanya vizuri, na kumkosoa kwa upendo akifanya vibaya. Hili
litampa uhakika wa wewe kuambatana naye, hivyo kuvutiwa na wewe zaidi.
4.
Jifunze
kumsikiliza na kuongea na mkeo. Hili ni la muhimu sana, mwanamke hujisikia kama
malkia akiona mumewe ametulia akimsikiliza. Mume mwema humsikiliza mkewe kwa
uvumilivu na busara. Wanawake wengi hupenda kuongea kuliko kusikiliza. Japo
wapo ambao hupenda kusikiliza pia, hivyo msome mkeo na kuhakikisha unakwenda
naye alivyo.
5.
Msifie
mkeo kwa kumpa majina mazuri, sifia umbile lake na kumtia moyo kila wakati.
Mwite mkeo “mpenzi, laazizi, malikia, mke; ikiwezekana weka na kiingereza
kidogo kama “honey”, “sweetie” “baby” “sweetheart” na mengine. Haya humpa mke
ujasiri na kujikubali zaidi, hivyo kila wakati atatamani uwe naye ili umsifie
zaidi.
6.
Mnunulie
mkeo zawadi za hap ana pale. Hili litampa kukuamini zaidi, na kuona kumbe
unamwaza kila wakati.
7.
Jitahidi
kumtosheleza mkeo katika tendo la ndoa. Hapa niongee kwa herufi kubwa
“kilichomtoa mkeo kwao pamoja na mengine yote, nit endo la ndoa. Hakikisha kama
mume unaongeza ufanisi kila siku. Mkeo atakufurahia sana ukimpa kile
anachokihitaji chumbani mwako.
8.
Mwamini
mkeo, japo wapo wanawake wasioaminika, tunajua aliyetoka kwa Mungu ni wa
kuaminika. Mke akiaminiwa kuna asilimia nyingi za kufanya vizuri kuliko
asipoaminiwa. Mpe uhuru, akikuambia jambo likubali bila kuona shaka. Kama una
shaka na jambo mwambie wazi ili akupe maelezo. Wanawake ni wasiri lakini wapewa
uaminifu, ni lazima walipe uaminifu.
9.
Jenga
urafiki wa karibu na mkeo, wakati mwingine muwe na muda wa kucheza, kutaniana
kidogo, kukumbushana mambo mbalimbali na mengineyo.
10.
Jifunze
kumshukuru mkeo kwa huduma anazokupa mfano tendo la ndoa, chakula, kukufulia,
kusafisha ndani, kukutunzia vitu, kulea Watoto na mengineyo.
11.
Pale
inapowezekana jiepushe na yale asiyoyapenda, na kuweka muda kwa yale
anayoyapenda.
12.
Usimtanie
kwenye madhaifu aliyo nayo. Ukifanya hivyo unaweza kumuumiza moyo na kuleta
hisia tofauti.
13.
Usimlinganishe
mkeo na wanawake wengine, mkubali kama alivyo na mzungumzie yeye zaidi ukiwa
naye. Epuka kuwasifia wanawake wengine ukiwa na mkeo.
14.
Ipende
familia, ikiwa ni pamoja na kuwahudumia watoto na ndugu. Mke hufurahishwa sana
na mume anayeipenda familia. Niliongea na binti mmoja akaniambia moja vitu
vinavyomuumiza duniani ni kuona baba yake hajali familia yake. Usilete maumivu
kama haya kwenye ndoa yako.
15.
Jiamini
na simamia maamuzi yako. Mke huwa hapendi kuona mumewe anatawaliwa na watu
wengine. Uthabiti na ujasiri wa kuamua humtia moyo mke.
16.
Uwe
mkweli kwa mkeo. Hakuna ukweli ambao mkeo anayekupenda kwa dhati atashindwa
kuchukuliana nao. Uongo ni sumu mbaya sana, ukimdanganya kisha akaja kuujua
ukweli itakuwa mbaya mara mbili ya kumwambia ukweli.
17.
Usikae mbali na mkeo kwa muda
mrefu bila sababu za msingi na makubaliano ya pamoja; ikitokea inakulazimu,
hakikisha unakuwa na mawasiliano ya mara kwa mara.
18.
Msaidie mkeo kazi za nyumbani, hasa akiwa amelemewa Na majukumu, amechoka, au anaumwa. Hii
itmfanya akuone kama rafiki yake wa karibu sana.
19.
Pale inapowezekana, uwe na mtoko na mkeo; mara kwa mara uwe na faragha naye. Huyo ndiye make wa ujana
wako. Kuambatana naye, kutembea pamoja naye, kwenda kanisani pamoja naye, kula
pamoja naye, na mengine kama hayo, huongeza sana ladha ya mahusiano.
20.
Usiogope
kuwa uchi mbele ya mkeo. Kuoga pamoja ni dsturi nzuri kwa wanandoa. Kuwa huru
kwa mkeo Ni ishara ya wazi kwamba unamwamini, na umejitoa kwa ajili yake. Hii
inaongeza furaha na mahaba kwenye ndoa.
21.
Dumisha
ukaribu na mkeo. Usipende kukaa mbali naye muwapo pamoja. Mkumbatie, mbusu,
ongea naye kwa kamnong’oneza. Hili litampa kuona kwamba unamkubali Na hatimaye
naye atajibu mapigo.
22.
Heshimu
hisia zake - usiwe mtu wa kulazimisha mambo bila sababu. Kama Kuna ulazima
kwenye jambo Fulani tumia lugha nzuri kulizungumza, mweleweshe. Usitake
kusikilizwa wewe tu. Wakati mwingine mwenzako naye ana namna anatamani mambo
yaende. Akikuhitaji pia Ni vizuri ukapatikana.
No comments:
Post a Comment