Mithali 29:4 “Mfalme huithibitisha nchi kwa hukumu; Bali yeye apokeaye rushwa huipindua.”
Rushwa/Ufisadi
(Corruption) – Ni kukosa uaminifu na kutumia vibaya mamlaka, au ni matumizi
yasiyo halali ya ofisi kwa jili ya kujinufaisha mwenyewe. Mla rushwa (corrupt)
ni mtu aliyeamua mwenyewe kutumia nafasi yake ya uongozi, au ofisi kwa manufaa
binafsi. Rushwa huwa inatumika kama msukumo wa kupotosha hukumu na kuwatolea
wenye haki, haki zao; kisha kuwapa wasiohaki nafasi. Tangu zamani watu maskini,
wajane, mayatima walinyimwa haki zao kwa sababu ya rushwa; na jambo hili
limekuwa likimuudhi sana Mungu.
Rushwa/ufisadi
hubeba sura mbali mbali, inaweza ikawa kwa mfumo wa hongo yaani kutoa fedha au
mali kwa ajili ya kushawishi maamuzi Fulani yasiyo halali au sahihih kufanyika.
Katika nyakati hizi pia tuna aina nyingine ambayo imekuwa ikisemwa sana na
mabinti wanaokwenda kuomba kazi maofisini – Rushwa ya ngono.
Mfumo
mwingine ni ule wa kuchota hela kutoka kwenye serikalini kwa kutumia mgongo wa
miradi na shughuli mbalimbali za serikali. Au kupunguza hela za matumizi ya
serikali na kujiwekea kwa matumizi binafsi. Kutumia ofisi za uma kwa manufaa ya
kibiashara binafsi, kujiwekea rasilimali ambazo zilipaswa ziwe za wengi mfano
mashamba na viwanja.
Mara
nyingi wanyonge na maskini wasio na uwezo wakutoa rushwa ndio huteseka na
kuishi maisha magumu, huku wachache wenye fedha wakifanya wanavyotaka. Hali hii
ni hatari sana kwa maisha ya watu na taifa kwa ujumla. Zipo sababu nyingi
lakini katika makala hii nitataja sababu chache, ni kwa nini rushwa ni hatari
kwa taifa:
1. Rushwa hulifarakanisha Taifa na Mungu kwani Mungu anachukizwa sana na Rushwa.
1. Rushwa hulifarakanisha Taifa na Mungu kwani Mungu anachukizwa sana na Rushwa.
Katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati 10:17
tunasoma, “Kwa maana Bwana, Mungu wenu,
yeye ndiye Mungu wa miungu,
na Bwana wa mabwana, Mungu mkuu, mwenye kuogofya, asiyependelea nyuso za watu,
wala hakubali RUSHWA.” Kama Yeye mwenyewe hakubali, basi hawezi kukubaliana
nayo. Watu wanapotoa na kupokea rushwa moja kwa moja wanakuwa kinyume cha Mungu
asiyependa upendeleo. Maagizo ya Mungu kwa viongozi wote ni:
-
Kuhukumu kwa haki
-
Kuwa na usawa
-
Kutenda mema kwa watu wote
- Kusimamia watu kulingana na utaratibu uliowekwa na
kukubalika mbele za Mungu.
- Kusimama kwa niaba ya Mungu kutoa maagizo
yanayostahili kwa watu
- Kuyashika maagizo na sheria za Mungu, huku wakijua Mungu ndiye aliyewapa mamlaka.
- Anapotokea viongozi wakaenda kinyume na haya yote, wanakuwa wanajisababishia hatia mbele za Mungu. Na kwa sababu Mungu anachukizwa nao, mambo mabaya hayapungui kwao. Magonjwa, majaribu, shida, misiba, na majanga mengi yanaambatana nao. Taifa lenye viongozi kama hawa liko kwenye hatari kubwa kwani kuna uwezekano mkubwa mambo mengi yakaharibika kwa sababu viongozi wamejikita katika kutatua shida zao.
Kwa
kinywa cha nabii Isaya Mungu anazungumza juu ya wakuu wa watu wake, Isaya
1:23 anasema, “Wakuu wako ni waasi, na rafiki za wevi; kila mtu hupenda rushwa,
hufuata malipo; hawampatii yatima haki yake, wala maneno ya mjane
hayawawasilii.” Mungu
hapendezwi kabisa na hali hii.
2. Rushwa hupofusha macho ya viongozi
Ili taifa liweze kuendelea katika eneo
lolote ni lazima pawe na viongozi wanaoweza kuona ili kuwapa watu maelekezo ya
kuwasaidia; na kufungua fursa kwa wenye uwezo kuzitumia. Viongozi wanapaswa
kuziona fursa na changamoto zinazoweza kujitokeza huko tuendako. Mataifa mengi
ya kiafrika yanataabika kwa sababu ya mambo ambayo hayakutazamwa ipasavyo na
viongozi waliotangulia. Wengi walipopata nafasi walijitazama wenyewe, hawakuwa
na wa kuangalia mbele kitakachotokea.
Viwanda vingi vilivyoachwa na wakoloni
vilifungwa baada ya miaka michache kwa sababu walioachiwa hawakuweza kuona
changamoto ambazo zingejitokeza, hivyo wakakwama baada ya muda mfupi. Na
wengine wa sababu ya kujipenda wenyewe wakajilimbikizia vitu na kuua shughuli
zote za kuufaidisha uma.
Katika kitabu cha kutoka Mungu anaongea
na uongozi wa Israeli kusema, “Nawe
usipokee rushwa; kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hao waonao, na kuyapotoa
maneno ya wenye haki.” Kutoka 23:8. Hapa Mungu anatoa madhara makubwa
mawili ya rushwa, yaani kupofusha macho ya waonao na kupotoa maneno ya wenye
haki. Maneno ya wenye haki ndiyo huliinua taifa, kama wenye haki wakinyamaza
taifa litakuwa kwenye hali ngumu.
Katika
Kumbukumbu la Torati 16:19 Mungu anaagiza tena kwa kiongozi, “Usipotoe maamuzi;
wala usipendelee uso wa mtu; WALA USITWAE RUSHWA; kwa kuwa rushwa hupofusha
macho ya wenye akili, na kugeuza daawa ya wenye haki”.
Kwa hiyo, taifa lenye viongozi wala
rushwa ni taifa lenye viongozi wasioona (vipofu) na kama viongozi ni vipofu
basin a watu wao wanakuwa vipofu. Hii ni hatari sana kwa taifa, taifa lolote
linahitaji viongozi wenye maono katika Nyanja mbalimbali ili liweze kuinuka.
3. Rushwa husababisha laana
Vilio na
manung’uniko ya waliyoonewa na kunyimwa haki zao sio Baraka kwa taifa. Viongozi
wanapowaacha watu wakateseka na kuumia bila kuwajali huku uwezekano wa
kuwasaidia ukiwepo ni laana. Laana hii huwakalia viongozi na uzao wake na taifa
lote kwa ujumla. Baadhi ya viongozi wamewafanyia watu ukatili mgumu sana bila
kujua, wakati mwingine kiongozi anaweza kuwaza kwamba ni akili kuwadhulumu watu
na kutumia nafasi yake kuwakandamiza watu wa hali ya chini; kimsingi hii ni laana.
Mpango wa
Mungu ni kwamba wale waliofanikiwa na wenye mamlaka wawasaidie watu wanyonge.
Na huu ndio mfumo wa kiroho unaokubalika mbele za Mungu. Taifa linalowajali
wanyonge halikosi kubarikiwa. Katika
Yeremia 23:1 Mungu anatoa Ole kwa wachungaji ambao kwa
tafsiri nyingine tunaweza kusema “kwa viongozi” , anasema “Ole
wao wachungaji, wanaoharibu kondoo za malisho yangu na kuwatawanya! Asema
Bwana. Kondoo hapa ni watu wanaoongozwa. Kwa hiyo, tunaweza kusema,
“Ole wao viongozi wanaoharibu watu (kwa kupotosha hukumu) na kuwatawanya (kwa
kuwakosesha amani).
Isaya
10:1 “Ole wao wawekao amri zisizo za haki, na waandishi waandikao maneno ya
ushupavu” Hili nalo linawahusu
viongozi kwa maana wao ndio waliopewa dhamana ya kuweka sheria. Kumbe ni lazima
waweke sheria au amri za haki na wanaohusika na kuandika waandike vizuri kwa
kuzingatia utaratibu aliouweka Mungu.
Neno ‘ole’, sio neno la Baraka. Ni neno
linaloonyesha kutakuwa na madhara baada ya muda. Kwa hiyo ni lazima viongozi
wajiepushe na rushwa ili kuliepusha taifa na laa (mabaya). Taifa lenye viongozi
waliolaaniwa ni taifa ambalo halina mwelekeo mzuri, viongozi waliobarikiwa
huinua taifa.
4. Rushwa hupanda uchungu ndani ya watu, na
kuwafanya watu kuchukia taifa lao wenyewe
Uchungu ni kitu kibaya sana kwa watu,
uchungu huleta mateso, huchoche malumbano na migomo. Watu wenye uchungu ni
rahisi kwenda kinyume na uongozi, na kuleta maafa makubwa. Taifa lenye watu waliojaa uchungu liko kwenye
hatari kubwa sana, kwani watu wengi wanakuwa hawako tayaya
Mungu anataka watu
ambao watapenda watu wake wafanikiwe, kwenye Zaburi 15:5 anasema, “Hakutoa
fedha yake apate kula riba, Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia. Mtu
atendaye mambo hayo Hataondoshwa milele.” Hapa
tunaona mtu ambaye anawekeza kwa haki, asiyetoa rushwa anakuwa na maisha
marefu.
5. Rushwa kufunga fursa za maendeleo
Taifa
lolote lenye watu wanaopenda rushwa, haliwezi kuwa na fursa za kutosha kwa
ajili ya watu wake. Sababu kubwa ni kwamba fursa huwa zinaambatana, kwa hiyo
kama mtu amefunga fursa moja kwa sababu ya faida binafsi basi anakuwa amefunga
fursa nyingine nyingi. Mfano mtu aliyepewa dhamana ya kusimamia shule au
kiwanda kisha akakubali kutumia hiyo nafasi vibaya kwa kujiangalia binafsi,
akapindua mambo na mwisho kiwanda kikafa. Mtu huyu atakuwa amezuia biashara
zilizokuwa zinafanyika kupitia hicho kiwanda, amepunguza uzalishaji, amewafanya
watu wakose ajira na kadhalika.
Ili fursa
za maendeleo zifunguke ni lazima fursa zilizopo zitumiwe vizuri. Rasilimali
watu, fedha pamoja na maliasili ni lazima zitumiwe kwa uaminifu kwa kuzingatia
mipango ya maendeleo iliyowekwa vinginevyo baada ya muda kilio cha kukosekana
kwa fursa kitaendelea kuwa kikubwa zaidi. Vijana wanapoinuka wakakutana na watu
waliojeruhiwa, viwanda vilivyokufa, maduka yaliyofungwa, maliasili zilizotumiwa
bila utartibu wanabaki kwenye wakati mgumu.
Siri
iliyowafanya walioendelea wakaendelea ni kule kuwa makini na kila fursa
iliyojitokeza, baada ya kuzitumia vema hizo fursa ikafika mahali kila siku
fursa mpaya zinafunguka, vijana wakizaliwa wanakuta mazingira mazuri
yanayowasaidia kuziona fursa mbalimbali. Serikali inahusika moja kwa moja
katika kuhakikisha watu wanazitumia vema fursa zinazofunguka.
6. Rushwa huleta mafarakano na visasi kati ya
watu
Watu
walioonewa na kunyimwa haki zao, hawawezi kuwa na mahusiano mazuri na wale
waliosababisha wao wakapoteza haki zao. Kinachotokea ni roho ya kisasi
kujengeka, na kwa sababu ile shida inaingia mpaka kwa watoto basi unakuta jamii
nzima inakuwa na hali ya visasi. Wengine watatumia nguvu za uharibifu
walizonazo, wengine migomo, wengine nguvu za giza na wengine kutafuta nafasi za
uongozi ili kupata fursa ya kulipiza kisasi.
Kuna
kauli nimeisikia ikisemwa sana na watu wa hali ya chini kwa watoto wao
wanapowasisitiza juu ya swala la shule, utasikia wakisema, “Soma kwa bidii
angalau ukifika huko na sisi tutaonekana kuwa watu, siku hizi kama huna mtu
huwezi kufika popote”. Bila shaka hii ni
kauli ya mtu anayejiona katika hali ya kutengwa kutokana na umaskini wake.
Rushwa ni mbaya sana mioyo ya watu wengi katika nchi zinazoendelea imeharibiwa
na rushwa.
7. Rushwa huzuia marafiki na kuongeza maadui.
Taifa
lililojaa rushwa haliwezi kuwa na marafiki wengi, kwani baada watu waliokuwa
marafiki kugundua kwamba misaada waliyokuwa wanatoa iliwafaidisha wachache na
haikuwafikia walengwa wanajeruhika na kuvunja mahusiano. Hili ni dhahiri kabisa
mataifa mengi yaliyokuwa yanatoa misaada kwa nchi zinazoendelea yamevunjika
moyo kwa sababu wakifuatilia wanakuta shida walitaka kutatua zko palepale.
Yaani
barabara walizofadhili zimevunjika, majengo waliyojenga, watu waliiba hela
wakajenga chini ya kiwango, masikini waliotumika kutafutia misaada bado hali
zao ziko vilevile. Na mengine yanayovunja moyo hata kuliko haya. Mataifa mengi
yaliyoendelea wanapenda sana ushirikiano na viongozi waaminifu na wenye uchungu
na maisha ya watu.
8. Rushwa hupotosha hukumu na kuvunja utaratibu wa uongozi katika taifa (katiba).
8. Rushwa hupotosha hukumu na kuvunja utaratibu wa uongozi katika taifa (katiba).
Taifa
lenye watu wanaotoa na kupokea rushwa, linakuwa na watu wengi ambao mioyo yao
imeathirika na hawawezi tena kutoa hukumu inavyopasa. Wamesoma lakini wanakuwa
hawana akili, unakuta kesi ambazo wanaweza kuamua hata watu wa kawaida kwa
ufasaha zinawashinda waliosomea. Roho Rushwa inaharibu utaratibu wa uongozi
katika taifa.
Kiujumla,
Viongozi wanakosa uwezo wa kukaa kwenye nafasi zao, kuna wakati wanapaswa
wasema ila wanakaa kimya; kuna wakati wanapaswa wakatae ila wanakubali tu; kuna
wakati wanafanya yasiyowapasa. Hili liko dhahiri, kuna mahali ukipita unaweza
kusema hivi hapa palikuwa na kiongozi? Swali hili hujitokeza kwa sababu
kiongozi hutambulika kwa utendaji wake. Kwa kifupi, Kiongozi aliyekuwepo
alikuwa ameuza nafasi yake ya uongozi, akabaki kama pambo tu.
Kwa
sababu ya rushwa wakuu wanakosa ujasiri wa kuwakemea wa chini yao, kwanini? Kwa
sababu kuna siri wamefichiana. Anaogopa kukemea ili mambo yake yasiwekwe wazi.
Kwa hiyo, kwa jinsi hii mfumo mzima wa uongozi unakuwa umevurugika, watu
wachache wenye madaraka wanakuwa ndio waamuzi wa kila kitu. Katima inabaki kuwa
pambo tu. Taifa lililojaa rushwa ni gumu sana, linakuwa na sheria zisizofuatwa,
wanapanga bajeti isiyosimamiwa, wanaweka mipango ambayo haitekelezwi ipasavyo.
9. Husababisha kuinuka kwa viongozi wasio na
sifa.
Taifa linaweza
kuwa na watu wengi sana wasio na sifa, walioingia kwenye nafasi kwa kuteuliwa
au kwa kuchaguliwa kutoana na rushwa. Mwanya huu unapojitokeza unakuwa ndio
mlango wa rushwa zaidi na zaidi. Kwa nini? Sababu kubwa ni kwamba watu wasio na
uwezo wa kufanya mambo watafuta namna ya kuwafunga vinywa wafuatiliaji, na njia
rahisi ni kutoa rushwa/hongo. Kwa jinsi hii taifa linadorora kiuchumi.
Rushwa
huwafanya watu wafanye maamuzi yasiyofaa wakati wa uchaguzi, rushwa huwafanya
wenye uwezo kukata tamaa hasa walio katika mazingira magumu/walio chini
kiuchumi. Taifa linakosa watu wabunifu; wanabaki walewale waliozaliwa katika
kambi ya wala rushwa ambao rushwa imeanza kuingia kwenye damu zao tangu mimba
ilipotungwa.
Mataifa
mengi ya ki-Afrika yamekuwa kwenye wakati mgumu kwa sababu ya baadhi ya
viongozi waliopenya nakuingia kwenye nafasi zao kwa njia isiyo halali.
Ninaposema viongozi simaanishi maraisi tu namaanisha kila mtu mwenye nafasi
kwenye eneo Fulani, iwe ni serikalini au sekta binafsi.
10. Hupindua
kweli, hivyo kulipindua taifa na kuliletea aibu.
Katika
Mithali 29:4 tunasoma jambo la ajabu sana. Neno linasema “Mfalme (kiongozi) huithibitisha
nchi kwa hukumu; Bali yeye apokeaye rushwa huipindua.” Kumbe mapinduzi hayafanywi na wanasiasa
tu, hata wala rushwa nao wana uwezo wa kuipindua nchi. Wanaipinduaje? Nafikiri
ni kwa njia ya kufanya mambo yaende ndivyo sivyo:
- Kutoka kwenye kuwa nchi ya amani na kuwa nchi ya
vita na migogoro
- Kutoka kwenye kuwa nchi ya kupendana kwenda kwenye
nchi ya chuki na visasi
- Kutoka kwenye nchi inayoendelea kuwa nchi
anayodaiwa
- Kutoka kwenye nchi inayojitegemea kwenda kwenye
nchi tegemezi na mapinduzi mengine
- Kutoka kwenye nchi inayoheshimiwa kwenda kwenye
nchi inayodharauliwa
Kumbuka
dhambi ni aibu ya taifa. Katika Mithali
14:34 tunasoma, “Haki huinua taifa; Bali
dhambi ni aibu ya watu wo wote.” Kwenye mstari huu tunapata pande mbili za
taifa:
-
Upande wa
Haki, pale ambapo watu wanafanyiwa mambo kwa haki, hakuna
anayemwonea mwingine, rasilimali zinatumika kwa usawa na watu wapewa
wanayostahili. Hapa tunaambiwa taifa huinuka (Mafanikio hutokea)
-
Upande wa pili tunakuta dhambi (ikiwepo dhambi ya rushwa ambayo ni dhambi ya karibu sana
kwa viongozi na wenye mamlaka). Hapa tunaambi ni aibu ya taifa. Mataifa mengi
ya Afrika yanasemwa vibaya kwa sababu ya Rushwa.
11. Viongozi wanakosa nguvu ya ushawishi kwa watu wao.
11. Viongozi wanakosa nguvu ya ushawishi kwa watu wao.
Mara
nyingi maswala ya rushwa au ufisadi hufanyika kwa siri, ila inapotokea hiyo
roho ikaendelea kudumu kwa muda mrefu, uovu wote uliofanyika kwa siri hufichuka
na mambo yote huwa wazi kwa watu. Hapo ndipo tafsiri na sura ya viongozi
hubadilika kabisa ndani ya watu. Watu huanza kuwaona viongozi kama wabinafsi na
watu wasio na uwezo wa kujizuia. Hapo inakuwa kila watalolisema linahusishwa
moja kwa moja na tabia yao ya kupenda rushwa/ufisadi.
Viongozi
waaminifu wanakuwa wanapendwa sana na watu, wanaweza kuwaambia watu mambo na
wakawaelewa. Watu wanawaona ni watu wenye uwezo mkubwa wa kuweza kutatua
matatizo yao, sio kuongeza matatizo. Viongo kama Mwalimu Julius K. Nyerere
raisi wa Kwanza wa Jamhuru ya Muungano wa Tanzania walikuwa na ushawishi mkubwa
kwa sababu ya kuchukia rushwa.
Taifa
lenye viongozi mafisadi/wala rushwa linakuwa na viongozi wasioweza kusikilizwa
na watu wao. Wanaweza kuitisha mikutano watu wasihudhurie. Ila kama viongozi ni
wema, waaminifu, waadilifu na wanaofanya mambo kwa haki, wanaoongozwa wanakuwa
na upendo wa dhati kabisa kwao. Na hivi ndivyo Mungu ameweka, kwamba wenye
mamlaka wapewe heshima.
Waebrania 13:17 inasema, “Watiini wenye kuwaongoza, na
kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa
hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana
isingewafaa ninyi.” Heshima hii ni kwa watu wale wanaotoa muda wao kwa
ajili ya watu wanaowaongoza. Kwa hiyo kama kiongozi ni fisadi hawezi
kuheshimiwa na watu wake, nguvu yake ya ushawishi inapungua na hapo taifa liko
hatarini.
12. Rushwa huuharibu ufahamu
12. Rushwa huuharibu ufahamu
Katika kitabu cha Mhubiri 7:7 tunasoma, “Kweli jeuri humpumbaza mwenye hekima, Na
rushwa huuharibu ufahamu.” Hapa neno hili linazungumza moja kwa moja kwamba
rushwa huuharibu ufahamu. Ni kweli kabisa, kuna wakati ukifuatilia baadhi ya
maamuzi yaliyofanywa na viongozi wala rushwa (Corrupt leaders) unaweza
kushangaa sana. Baadhi ya maamuzi wanafanya bila ufahamu kabisa.
Ufahamu ulioharibika ni ule ambao
haufanyi kazi ipasavyo, ni kama mtu anajua ila hajui. Ufahamu ulioharibika kwa
tafsiri nyingine ni upumbavu. Akili zinakuwa zimepumbazwa kwa rushwa, ufahamu
umepoteza mwelekeo. Utakuta kiongozi anajua kabisa ujenzi wa miundimbinu Fulani
ni kwa ajili ya faida ya sasa nay a baadaye, lakini atathubutu kutumia fedha za
miundombinu kwaajili ya mambo yake binafsi. Hii ni kwa sababu ya ufahamu
ulioharibika.
Hitimisho
Naamini
kupitia makala hii utakuwa umepata kitu cha kukusaidia katika lile unaloweza
kufanya katika kupiga vita rushwa katika bara letu la Africa. Ili nchi zetu za
kiafrika zipige hatua kiuchumi, kisiasa na kijamii ni lazima iwe na watu
wanaoichukia rushwa ili kuepukana na madhara yote yaliyotajwa hapo juu. Najua
kwa msingi huu wa maneno kutoka kwenye Biblia Takatifu ambacho ni kitabu
kinachotumiwa na wengi duniani kote, kuna mambo ambayo yamekuwa wazi kuliko
ilivyokuwa mwanzo.
Ikiwa wewe
ni kiongozi uliyeteuliwa au kuchaguliwa, au unasimamia kampuni binafsi au
vyovyote ulivyo, nina hakika kila mtu ni kiongozi katika eneo lake; au wewe na
raia mwema wa taifa Fulani, nakusii usimame katika nafasi yako kuhakikisha
mbegu ya rushwa haiendelei kumea na kuifunika nchi yako.
Kila mtu ana nafasi katika kutokomeza
adui huyu anayejulikana kwa majina mengi. Wengine humwita Corruption/bribe,
wengine rushwa, wengine hongo, wengine takrima, wengine kitu kidogo na mengine
mengi. Kimsingi hawa wote ni watoto wa baba mmoja na kazi yao na kuleta
umaskini wa wengi huku wachache wakinufaika.
Mungu ibariki Tanzania!
Mungu ibariki Afrika!
Na Mwl. S.S.Michael
Simu: 0713511544 (Whatsapp)