UNYENYEKEVU (HUMBLENESS/HUMILITY)
Dunia imejaa watu wanaotamani ukuu, utajiri na umaarufu; huzuni ni kwamba wengi hawajaelewa siri iliyopo kwenye kuinuliwa kwa mtu. Jitihada za kuonekana (kuwa maarufu), kuwa na fedha au mengine zimewakaa sana wanadamu. Na hii ni kawaida ya wanadamu, tumeumbwa lili tuishi kwa utukufu wa Mungu. Mafanikio yetu, hasa yanayotokana na Mungu yanaonesha utukufu wa Mungu.
Mambo ya msingi ya kujua:
A. Utajiri na heshima ya kweli hutokana na Mungu: Maandiko katika 1 Samweli 2:7 yanasema, "Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu." Tena katika Mithali 8:18 tunasoma, "Utajiri na heshima ziko kwangu, Naam, utajiri udumuo, na haki pia."
Hivyo bila Mungu mtu akipata utajiri, hauwezi kuwa wa kudumu. Tena utajiri unaoambatana na heshima ni ule unaotoka kwa Mungu.
Kwenye Mithali 22:4 inatuweka sawa zaidi "Thawabu ya unyenyekevu ambao ni kumcha Bwana Ni utajiri, na heshima, nayo ni uzima."
Kunyenyekea (Kumcha Mungu), kumeelezwa kuwa na matokeo makubwa matatu:
Utajiri: kumiliki au kuwa na mali nyingi
Heshima: kuwa na thamani kwa watu wanaokuzunguka
Uzima: kuwa na uhai au maisha.
Jumla ya mambo haya ni maisha bora (Maisha ya mafanikio). Mtu yeyote ambaye ni mnyenyekevu mbele za Mungu ana nafasi kubwa ya kuweza kufanikiwa katika Mungu.
Utajiri wa kweli hutokana na baraka za Mungu. Mithali 10:22 "Baraka ya Bwana hutajirisha, Wala hachanganyi huzuni nayo." Tukinyenyekea kwake atatuinua. 1 Petro 5:6 Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;
B. Kufanya kazi kwa bidii na uaminifu ni sehemu ya unyenyekevu. Mtu aliyejaa kiburi, mbinafsi hawezi kufanya kazi kwa mafanikio. Mtu mwenye bidii katika kazi ana nafasi kuwa sana ya kufanikiwa (wakati mwingine hata kama hana uhusiano mzuri na Mungu).
Shida ya kufanikiwa nje ya Mungu, ni maisha kuwa katika hatari. Haiwezekani kudumu katika utajiri, heshima na uzima bila kuwa na Mungu. Labda mtu aamue kuyauza maisha yake kwa shetani, napo shetani ni mwivi, aibaye na kuharibu na kuchinja (Yohana 10:10)
C. Kunyenyekea na kuwaheshimu wazazi kunaleta mafanikio na maisha marefu. Kumb. 5:16 Waheshimu baba yako na mama yako; kama Bwana, Mungu wako, alivyokuamuru, siku zako zipate kuzidi, nawe upate kufanikiwa katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako.
Watu wengi wamekwama kwa sababu ya kuonyesha kiburi kwa wazazi wao. Ni kweli unaweza kuwa umesoma kuliko wao, au una imani kuliko wao au umewazidi kiuchumi; bado ni haki yao kupata heshima kutoka kwako. Uwasikilize na utii katika yale yanayompendeza Mungu. Kushindana na wazazi hakuna baraka, ni laana.
D. Wazazi wa kiroho nao ni watu wa muhimu sana (Paulo anawaita wazee au watu waliotutangulia katika Imani). Mchungaji au mtu yeyote ambaye Mungu amemweka mbele yako akusaidie katika maisha yako ya kiroho, huwezi kuishi naye bila unyenyekevu.
Yohana 13:14 "Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi." Hapa Yesu anatufundisha somo kubwa la kunyenyekeana sisi kwa sisi. Hii ndiyo njia ya kuwa wakuu kuliko wengine. Yesu anasema mkuu lazima awe mtumwa wa wengine. Marko 10:44 na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote.
E. Kunyenyekea kwa viongozi ni njia ya kumweshimu Mungu aliyewaweka katika hiyo mamlaka. Kama umeajiriwa au unaishi katika nchi au eneo fulani. Unyenyekevu ndiyo njia ya kupata kibali kwa wakuu. Ajikwezaye hushushwa. Uwe mnyenyekevu huku ukitimiza majukumu yako kwa moyo. Ukiona watu wananyenyekea kwa raisi usiwashangae, wameng'amua siri ya kufanikiwa. Kunyenyekea si kujipendekeza. Ni kumpa heshima anayestahili heshima.
Mwisho Petro anasema"Waheshimuni watu wote. Wapendeni ndugu. Mcheni Mungu. Mpeni heshima mfalme."1 Petro 2:17
JE, UNATAKA KUFANIKIWA KATIKA MUNGU? JIFUNZE KUNYENYEKEA. UTAFANIKIWA.
Na. Mwl. S.S.Michael
Simu: 0713511544 (Whatsapp)