Sunday, 8 July 2018

SOTE TUPIGE KELELE


 "ZIMWI HILI HALIJAFA"


Ama kweli rushwa zimwi, tena zimwi kwelikweli
Lazidi hata ukimwi, upungufu kinga za mwili
Kama moto halizimwi, kila kona watu chali
Zimwi linatutafuna, sote tupige kelele

Halichomwi Kwa mkuki , kwa risasi halitoki
Chunguni halipikiki, ni gumu halikatiki
Adui wa kila haki, kuchafua halichoki
Zimwi linatutafuna, sote tupige kelele

Tena halijabagua, kwa yeyote linapita
Rangi yake yavutia, kila mtu kumvuta
Mjini kijiji pia, kotekote talipata
Zimwi linatutafuna, sote tupige kelele

Wengi walio kitini, wamekwisha kuvamiwa
Ni wema sana machoni, moyoni ni kama chawa
Aingiapo mwilini, hataki kuondolewa
Zimwi linatutafuna, sote tupige kelele

Nyangumi pia dagaa, wote limewafikia
Mashilingi wayazoa, nyumba zao kujengea
Hoja wanazozitoa, uongo tamu kolea
Zimwi linatutafuna, sote tupige kelele

Wako kama hayawani, hawataki makatazo
Kila kitu mfukoni, wanazidisha ujazo
Utu kwao ndio nini, Rushwa kwao ndiyo chanzo
Zimwi linatutafuna, sote tupige kelele

Wangine kiomboleza, wao kwao ni tulizo
Hukumu kuigeuza, hilo kwao si tatizo
Haki nazo kuziuza, kila kona ni uozo
Zimwi linatutafuna, sote tupige kelele

Yatima hata wajane, wamekuwa kama ngazi
Wanapopanda  wengine, kukanyagwa ndiyo kazi
Wakisema wayanene, mwisho wake ni machozi
Zimwi linatutafuna, sote tupige kelele

Huko nako barabara, nao wamo mtegoni
Wamebaki na mkwara, nacho kidogo pembeni
Japo wana mshahara, wataka na mkononi
Zimwi linatutafuna, sote tupige kelele

Kanisani ‘sikitini, zimwi linajipenyeza
Tuulize kulikoni, nako tume kuchunguza
Hawa watu wa Imani, Mola hajawatuliza?
Zimwi linatutafuna, sote tupige kelele

Masikini hatiani, matatani kibindoni
Makosani hukumuni, mtieni gerezani
Nguvuni afanye nini, mhaini wa kitini?
Zimwi linatutafuna, sote tupige kelele

Hili zimwi tangu kale, halina wa kulitaka
Sio hawa wala wale, kauli ni toka toka
Kwa hatua na kelele, zimwi hili tatimka
Zimwi linatutafuna, sote tupige kelele

Zimwi hili ni laana, lachafua nchi yote
Tena halina maana, adui wa watu wote
Linaleta kuumana, na vilio kotekote
Zimwi linatutafuna, sote tupige kelele

Hongera kwa wateule, wapigao makelele
Maisha yasiwe yale, ya hadithi tangu kale
Uzalendo utawale, tamaa tutupe kule
Zimwi linatutafuna, sote tupige kelele

Tusitazame usoni, tukitaka ua nyani
Wahuni na waumini, vitini uraiani
Bungeni nako chamani, mkoani wilayani
Zimwi linatutafuna, sote tupige kelele

Majumbani mashuleni, televisheni redioni
Barabani mtaani, mjini na vijijini
Jijini mtandaoni, Gazetini  vitabuni
Zimwi linatutafuna, sote tupige kelele

Mahakamani barazani, Jeshini sipitalini
Ofisini mashambani, makampuni sokoni
Mashuleni na vyuoni, kusini kaskazini
Zimwi linatutafuna, sote tupige kelele

Hata nako vitabuni, zimwi hili ni chukizo
Chukizo kwa Maanani, kwalo hataki mchezo
Hasa wale wa enzini, wasiotaka katazo
Zimwi linatutafuna, sote tupige kelele

Chonde chonde wanakwetu, tusimmunye maneno
Sote tubebe mtutu, tuanzishe fungamano
Nchi yetu haki zetu, tusongeshe mpambano
Zimwi linatutafuna, sote tupige kelele

No comments:

Post a Comment

MWANAUME KWENYE NAFASI YA "MUME"

Mume ni mwanaume aliyeoa kwa kuzingatia vigezo na taratibu za kijamii, kishria na za kiroho. Mume si rafiki wa kiume (boyfriend), hawara, wa...

Powered By Blogger