NDOA INAHITAJI USAFI WA ROHO NA MWILI
Uchafu ni kitu cha kuchukiza sana. Hakuna mtu yeyote
anayeweza kuchukuliana na mazingira machafu labda awe hana akili. Usafi ni
asili ya Mungu, Mungu hachangamani na uchafu wa aina yoyote. Usafi wa kiroho
kwa lugha nyingine ni utakatifu. Mungu wetu ni Mtakatifu, chochote
kinachotokana naye ni kitakatifu. Yeye alikusudia kila alichokifanya kidumu
katika utakatifu.
Ndiyo maana akakamilisha kazi yake yote ya uumbaji katika
utakatifu (dhambi ilikuwa haijaingia duniani). Ndoa ya kwanza ilifungwa na
Mungu mwenyewe, na ilifanyika katika usafi wote (Adamu na Eva walikuwa safi
walipounganishwa na Mungu) na Mungu akawaagiza waendelee kudumu katika usafi na
kuepuka kula atunda ya mti wa mema na mabaya.
Usafi (wa rohoni na mwilini) ni nguzo ya ndoa. Ikiwa
wanandoa hawajasimama katika huo, hakuna uwezekano wa kufika mbali. Uchafu
husababisha maradhi, harufu mbaya, na kudharauliwa. Heshima ya ndoa inategemea
jinsi ambavyo wanandoa watadumu katika usafi. Uchafu wa rohoni hudhihirika
kwenye matendo, maneno na mawazo; uchafu wa mwilini hudhihirika kwenye mwili,
malazi, mavazi na kwenye mazingira (ndani ya nyumba na nje). Mtu anaweza kuwa
na:
1.
Midomo michafu.
Hii ni ile hali ya kutoa maneno machafu ambayo
husababishwa na yale yalioyoko moyoni. Isaya aliuona uchafu huu alipomwambia
Mungu “mimi ni mtu mwenye midomo
michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu” (Isaya 6:5). Bila shaka utaelewa kwamba midomo michafu hapa haimaanishi midomo ambayo
haijasafishwa (hajapiga mswaki); maana yake ni kule kuwa na maneno machafu,
kunena mabaya (uovu, masengenyeo, matusi na mengine). Ili ndoa isimame
inahitaji maneno mazuri yenye kujenga, maneno ya kutia moyo, maneno matamu,
maneno ya staha, maneno yaliyojaa neema ya Mungu. Ndoa nyingi
zimeharibika kwa sababu ya midomo michafu.
Ukikuta mke ni
mtukanaji, au ni msengenyaji au ni mgomvi asubuhi, mchana na jioni, ujue hakuna
ndoa hapo. Hata kama ataishi na mume, yatakuwa maisha ya taabu sana. Mithali
inasema “Ni afadhali kukaa katika nchi ya nyika; Kuliko na
mwanamke mgomvi, mchokozi. (Mithali 21:19) Unaona, nchi ya
nyika ni mahali pa shida (hapana maji, jua kali, hapana chakula) ila mateso
yake hayafikii mateso ya kukaa ndani na mwanamke mgomvi na mchokozi. Je, mdomo
wako unautumiaje? Kusudi la Mungu ni kwamba wanandoa watiane moyo, wajadili
mambo yao kwa upendo, wapeane maneno yenye kujenga. Siyo kutukanana, kuitana
majina ya wanyama, kugombana, na kuchokozana.
Mwanaume anayeutumia mdomo wake kama silaha ya kumpiga mke wake naye
haijengi ndoa yake. Mwanaume ni mshauri wa familia, ni mwalimu, ni baba, ni
kiongozi na ni mlinzi wa mke na watoto. Maneno ya ukali na matusi au ugomvi,
hurarua mioyo ya watoto na mke. Ni muhimu mwanaume kujifunza Kwa Mungu, Baba.
Yeye ni Mungu wa Upendo, hata wanawe tukikosea
huturidi (hutuadhibu) kwa upendo. Kila wakati anatuwazia yaliyo mema,
hajawahi kuwaza kutuumiza au kutuangamiza. Hata tukimkosea atakasirika lakini
tukishuka na kumwomba msamaha yeye hutusamehe.
Hivyo ni muhimu tukahakikisha midomo yetu ni misafi, yaani tunaongea maneno
mema siku zote. Paulo anasema “Maneno yenu yawe na neema siku zote,
yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu.” (Wakolosai
4:6) Mke akijua jinsi ya kumjibu
mumewe na mume akajua jinsi ya kuongea na mkewe na wote wakaungana kuongea na
Mungu maisha yatakuwa mazuri sana. Hata mwenzi wako akikosea, ongea naye kwa
maneno ya kujenga. Maneno yana uwezo wa kubomoa kabisa mahusiano, kumbuka Mauti
na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.
(Mithali 18:21). Maneno yanaweza kuua au kuhuisha ndoa yako, Mwombe Mungu
akitakase kinywa chako kama ukiona kina shida.
2.
Moyo uliojaa
uchafu.
Maandiko
yanasema, “Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji,
uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano” (Mathayo 15:19). Moyoni mwa mtu ndimo mlimo hisia, mawazo, na maamuzi, hivyo ili maisha ya
mtu yawe salama ni lazima moyo uwe salama. Kwenye mithali tunasoma, “Linda
moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.
(Mithali 4:23. Moyo uliochafuka ni makao ya shetani, kila aina ya uharibifu
utatoka ndani yake. Kama mwanadoa mmoja wapo ataacha moyo wake wazi na shetani
akaujaza uchaffu wake (chuki, husuda, matukano, uzinzi, uasherati, uongo na
mengine) ndoa haitaweza kusimama.
Upendo wa kweli huletwa na Roho Mtakatifu ndani ya
mtu, hivyo kama moyo ni mchafu Roho Mtakatifu hawezi kukaa na upendo wa kweli
hauna nafasi. Suluhisho ni kurudi msalabani na kumtwika Yesu mizigo ili kupata
raha moyoni (nafsini) – Mathayo 11:28. Moyo wa mtu hujazwa kwa vile
anavyovisikia, anavyovisoma na kuviona.
Je, huwa unasoma nini? Huwa unasikiliza
nini? Huwa unatazama nini kwenye runinga au ‘smartphone’ au
kipakatilishi chako? Moyo wako ndio uliobeba ndoa yako, na ukilemewa na uchafu
hakika utaiharibu ndoa. Dhambi ilipowalemea Adamu na Eva, walianza kulaumiana
mbele za Mungu. Linda moyo wako, linda ndoa yako.
Dunia hufanya kazi katika mfumo hatari ambao hauwezi kutusaidia kudumu
katika mahusiano. Kimsingi, dunia huhamasisha ubinfsi, chuki, kiburi na tamaa
ambavyo ni hatari sana kwa ndoa. Yohana anasema, “Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na
kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. (1Yohana 2:16). Mambo haya yaani “taama ya mwili, tama, na kiburi” kazi yake ni
kuvuta uharibifu na kututenga na Mungu.
Uasherati ni uchafu mbaya, unaua
roho na kuharibu mwili; ni lazima kujiepusha nao kama
kijana unayempenda Mungu. Mabinti wanaojua thamani ya ubinti wao na vijana
wanaojitambua hujilinda kabisa na uchafu huu. Ndoa nyingi zimevurugika kwa
sababu ya uasherati ambao wanandoa waliufanya kabla ya ndoa. Wengine katika uasherati
wao wakapata watoto ambao wamekuwa chanzo cha vurugu na chuki katika ndoa.
Uchafu wa uasherati huchochea uzinzi katika ndoa, japo si mara zote. Ila mara
nyingi watu ambao hawakuwa waaminifu kabla ya ndoa hushindwa kuwa waaminifu
kwenye ndoa.
Usifanye
tendo la ndoa kabla ya ndoa, na baada ya ndoa baki na mume wako kama Mungu
alivyoamuru; ndoa yako haitatikisika.
|
Ni muhimu sana wanandoa wakadumisha usafi mioyo
yao, na wasijichafue kabisa kwa uzinzi au picha za ngono. Kuaminiana huletwwa
na usafi. Kila mmoja akikubali na kuamua kwa moyo wa dhati kumtii Mungu na kuwa
wasafi na waaminifu kwa ndoa yake, maisha ya ndoa yatakuwa ya Baraka sana.
Usafi ni msingi wa muhimu sana katika ndoa.
3.
Mikono (michafu)
iliyojaa damu.
Unaitumiaje mikono yako? Wengine wameitumia kuwapiga
wenzi wao. Wengine wameitumia kubeba vitu ambavyo ni hatarishi kwa wenzi wao.
Je, mikono yako ni salama? Mungu ametupa mikono ili kwamba tuweze kujipatia
kipato kwayo, tena tuitumie kuwasaidia wengine sio kuwaumiza. Mume au mke
ambaye mikono yake ni myepesi kuleta madhara hawezi kuishi na ndoa yake kwa
usalama. Mtume Yakobo akasema, “Mkaribieni Mungu, naye
atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha
mioyo yenu, enyi wenye nia mbili.” Hapa anazunggumza juu ya
kuitakasa mikono na mioyo ili kuweza kuwa karibu na Mungu. Usafi huu ni wa
muhimu sana.
4.
Mwili na
mavazi.
Usafi wa mwili na mavazi una uzito sana kwenye
mahusiano. Tuliyoyaona hapo juu ni mambo ya rohoni, hivyo matokeo yake huja
taratibu na ni ya ndani. Swala la mwili na mavazi ni la wazi na halifichiki.
Watu wengi wamevuruga mahusiano yao ya ndoa kwa sababu ya uchafu. Baadhi ya maeneo
ya kutilia mkazo zaidi ni:
-
Nguo za ndani
yani brazia, chupi, boksa, soksi, vesti n.k. hakuna kitu
chenye kero kama harufu mbaya. Na kwenye ndoa ule ukaribu wa wanandoa huweza
kuathirika sana kama kutakuwa na harufu mbaya inayotoka kwa mmoja wapo.
Kukimbiana na kutokufurahiana huanzia hapo, mwisho michepuko hubisha hodi.
Usafi wa mavazi ni kivutio kikubwa sana kwa mwenzi wako, usikubali kuwa mchafu
bila sababu za msingi.
-
Mwili: Sehemu
za siri, kinywa, kwapa nk; Haya nayo yamevuruga ndoa nyingi. Mume au mke ni mtu
wa karibu sana na mara nyingi meneo haya kwake ni ya msingi, hasa kwenye eneo
la tendo la ndoa. Hivyo yakiwa machafu yanamsababisha anapata haaki yake kwwa
mateso badala ya furaha. Mwisho anaweza kupoteza kiu kabisa au akafanya kama
wajibu tu bila kuonyeha furaha na kuridhika. Hii ni hatari kwa ndoa.
5.
Mazingira ya
ndani na nje.
Haya nayo yana umuhimu wake, kimsingi nyumba yenye
mandhari masafi ni bustani yenye kuvutia kwa wanandoa. Usafi huleta unadhifu na
hamasa kwa wanandoa wenyewe na wageni. Maeneo ya msingi ya kuangalia kwenye
eneo la usafi wa ndani na nje ni:
-
Usafi wa nyumba
na mpangilio wake. Nyumba ikisafishwa na kupangiliwa vizuri huwavutia
sana wanaume, wanawake nao hufurahia kuona wanakaa na waume zao nyumbani ili
kujenga ndoa. Usafi na mpangilio mzuri wa nyumba ndiyo siri ya mafanikio katika
hili.
-
Chumba na
malazi; Chumba cha wanandoa ni cha muhimu sana, yaani ni
mahali ambapo wanashikiana katika tendo la ndoa. Hivyo ni mahali wanapafurahia
kuliko pahali pengine pote. Ni bustani ya amani na furaha kwa wandoa.
Usafi wa
chumbani ni wa msingi sana. Na hili linawahusu wanandoa wote japo mke ndiye
msimamizi mkuu wa jukumu hili. Mashuka yafuliwe kwa wakati, chumba kisafishwe,
neti ifuliwe, vitu vipangiliwe vizuri, pawepo na kapafyumu kazuri, yaani mambo
yatakuwa mazuri sana. Mke usikubali mumeo atamani kukaa chini ya miti kwa
sababu chumbani hapakaliki. Jitahidi kwa uwezo ulionao ufanye usafi.
-
Maandalizi ya
chakula na vyombo: Chakula kilichoandaliwa katika mazingira safi na
kutengwa kweye vyombo visafi, ni kivutio kikubwa. Hata hamu ya kula huja ghafla
kwa ule usafi tu. Ndoa inaguswa na eneo hili pia, ili mume au mke ale na
afurahie chakula usafi unahitajika.
-
Chooni na
bafuni na Mazingira ya nje, nayo pia yanahitaji usafi ili kuifanya nyumba iwe ya
kuvutia zaidi. Watoto hujifunza sana kwa wazazi, hivyo usafi ukitiliwa mkazo
utawajengea watoto tabia njema na utajenga sifa njema kwa ndoa.
Kumbuka uchafu wa aina yoyote ile huleta dharau,
hakuna mwanandoa yeyote anayependa kudharauliwa kwa sababu ya mwenzake. Mume
hupenda kusifiwa kwa sababu ya mkw wake na mke vivyo hivyo. Kiujumla, usafi ni
msingi wa muhimu sana kwa wanandoa. Ona mstari huu unavyosema “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati
na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.” Waebrania 13:4. Katika
mafundisho ya Paulo kwa Timotheo, Paulo alikazia sana kuhusu usafi pia (1Timotheo
4:12), hivyo usafi ni lazima utiliwe mkazo kwa vijana, ili wakafanye vizuri
kwenye ndoa zao pia.