"Wanaomtegemea Mwenyenzi - Mungu, wako kama mlima Siyoni, ambao hautikisiki bali wabaki imara Daima" (Zaburi 125 BHN)
Kila aliyeamua kuishi maisha ya kumwamini Mungu ni lazima aidhihirishe Imani yake katika tumaini kwa Mungu siku zote. Mtu asiye na Tumaini ni mtu ambaye hana imani thabiti kwa Mungu. Biblia aintufundisha mengi kuhusu tumaini au tegemeo:
Mfano "Usizitegemee akili zako mwenyewe" (Mithali 3:5), usiwatumainie wanadamu (Yeremia 17:5), usiwatumainie wakuu (viongozi) (Zaburi 146:3), usizitumainie mali (1Timotheo 6:17) na mengine kama hayo. Mungu anataka tumtumaini Yeye peke yake, hili ni la muhimu sana katika maisha ya wokovu. Ni kweli wanadamu wanaweza kukusaidia lakini haikupaswi kuwatumainia. Acha Mungu awatumie kwa wakati wake ili kama ikitokea hawapo wewe uzidi kusonga mbele. Kila siku useme “Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini.” (Zaburi 91:2)
Hakika “VITA NI VYA BWANA” baada ya kuokoka, wewe ni sehemu ya ufalme wa Mungu duniani (tueingizwa kwenye ufalme wa Mwana wa pendo la Mungu (Wakolosai 1:13) . Hivyo tunalindwa na jeshi la ufalme wa Mungu (Zaburi 34:7), tena tunalindwa na nguvu za Mungu (1Petro 1:5). Ukilielewa hili utakuwa na maisha ya wokovu yenye mafanikio makubwa kiroho na kimwili.
Mara nyingi watu hukwama kwa sababu ya kukosa maarifa (Hosea 4:6). Shetani akijua hatujui haki zetu katika Bwana, atatumia mwanya huo kutuyumbisha kiimani. Nafurahi kwa sababu leo umeshajua kwamba ni haki yako kulindwa na Mungu, usimpe ibilisi nafasi. (Waefeso 4: 27). Mtumaini Mungu hata wakati wa vita. Usilie kama waliavyo wasio na Mungu. Wewe ni mteule wa Mungu, simama imara katika kusudi la Mungu. Watu wanaweza kukuacha lakini Mungu hawezi kukuacha. Yeye anasema, "Nimekuchora katika viganja vyangu; kuta zako naziona daima mbele yangu" Hakuna asiloliweza Mungu.
No comments:
Post a Comment