Maarifa ni uwezo wa kutumia ufahamu ili kusababisha
mabadiliko au matokeo mazuri au mafanikio. Unaweza ukawa ni ufahamu wa
kiroho au ufahamu wa kawaida wa kibinadamu. Kuwa na ufahamu tu hakutoshi, bali
ni lazima mtu aweze kuutumia huo ufahamu vizuri kwa ajili ya maisha ya kila
siku. Chanzo cha maarifa yote ni uchaji mbele za Mungu (Mithali 1:7) Yaani kuwa
na hofu ya Mungu kunakodhihirika katika ibada na utii katika neno lake. Katika maisha
yetu yapo mengi yanayohitaji maarifa na hekima ya Mungu. Maarifa huleta hekima
na hekima hutuwezesha kuishi vizuri na watu, hivyo kuwa na maisha ya furaha na
amani.
Katika Muhubiri 11:8-9 Maandiko
yanasema,
“Naam, mtu akiishi
miaka mingi, na aifurahie yote; lakini na azikumbuke siku zijazo za giza, kwa
maana zitakuwa nyingi…..Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako
ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono
ya macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote Mungu
atakuleta hukumuni.”
Katika mistari hii
tunajifunza kwamba ni mpango wa Mungu tuifurahie miaka yote ya maisha yetu,
ikiwepo miaka ya utoto, ujana, utu uzima na uzee. Swali langu ni kwamba, “Ni kwa nini vijana
na watoto wengi wanaishi maisha ya huzuni, majuto, maumivu makali moyoni,
migogoro, chuki, dhiki nk? Katika kutafakari nikagundua kwamba ipo
shida kubwa kwenye mahusiano kati ya watoto/vijana na wazazi/walezi. Watoto
wengi wamewaumiza wazazi/walezi wao kwa tabia zao mbaya za dharau na dhambi,
kwa upande mwingine nao wazazi/walezi wamewaumiza watoto/vijana kwa kutotimiza
wajibu wao na kuwatendea mabaya.
Tena katika Hosea
4:6 Mungu anasema, “Watu
wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa
maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa
umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako.” Kukosa
maarifa ya Mungu katika kujenga mahusiano ya kifamilia imekuwa ni tatizo kubwa
kwa dunia, katika kizazi hiki. Kwa sababu hiyo shetani anazidi kuangamiza
kizazi hiki kwa kasi sana.
Kwenye isaya Isaya 5:13
tunasoma matokeo mengine mabaya sana yanayoletwa na kukosa maarifa ya ki-Mungu,
hapo tunasoma, “Kwa
sababu hiyo watu wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa;
na watu wao wenye cheo wana njaa, na wengi wao waona kiu sana.” Kumbe
kwa kukosa maarifa ndipo tunaweza kuona jinsi ambavyo kizazi hiki kimeingia
katika uteka wa Ibilisi kupitia mifumo ya kisasa ya maisha. Maeneo mengi watu
wanalia kuhusu tabia za watoto wa kizazi hiki.
Wazazi/walezi wamekuwa
na wakati mgumu sana katika malezi ya watoto wao. Hapa dawa ni Mungu aingilie
kati, maombi na sala pamoja na kuwekeza kwenye kuwajaza maarifa ya Mungu ndilo
suluhisho la kudumu. Uteka hauvunjiki kwa vikao na adhabu, au kutishiwa
kufungwa gerezani; Mungu ndiye mwenye uwezo wa kuwaweka huru waliosetwa katika
mateka ya Ibilisi.
Katika Luka 4:18 Yesu
anasema, “Roho wa
Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini
habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu
kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa” Watoto/vijana wetu wengi
wanahitaji mguso wa Mungu watoke katika vifungo vilivyowafunga. Nimeshuhudia
matukio mengi katika shule ambazo nimepita, watoto wengi watukutu wanakuwa wana
uvamizi wa kipepo ndani yao, si wao katika hali ya kawaida.
Kwa maombi yetu na jitihada zetu za kuwafundisha ili wajae maarifa ya kiMungu,
ndivyo vitakavyoleta mapinduzi.
Shetani anashughulika
kuwazuilia watoto/vijana maarifa ya Mungu ili apate kuwachota kwa urahisi kila
siku. Katika Mithali 1:7, tunasoma, “Kumcha Bwana ni
chanzo cha maarifa” Ukiangalia katika kizazi hiki watoto na
vijana wengi wamejaa mambo machafu sana, haya mambo ndiyo yanayochafua kabisa
mahusiano na wazazi na kuwafanya watoto/vijana waingie kwenye uteka wa Ibilisi.
Maswala ya mitandao yamechochea sana uasherati kwa kizazi hiki, siku hizi ni
kawaida kukuta binti mdogo waa shule ya msingi ameshaanza maswala ya mapenzi.
Kwenye Mithali 1:28-29 tunaona
matokeo mengine mabaya YA kuyakataa maarifa ya Mungu, Neno linasema, “Ndipo watakaponiita,
lakini sitaitika; Watanitafuta kwa bidii, wasinione. Kwa kuwa walichukia
maarifa, Wala hawakuchagua kumcha Bwana.” Hakuna mwanadamu
asiyemwitaji Mungu katika mambo mbalimbali ya maisha yake. Hapa tunaona hali ya
hatari inayojitokeza kizazi kinapokuwa na watu walioyakataa maarifa ya Mungu.
Kwanza maombi hayatasikiwa na Mungu, pili, Mungu hawezi kuonekana wakati anahitajika.
Hivyo ni lazima kila mtu akajua ana wajibu wa kutafuta maarifa ya Mungu ili kwa
hayo tuweze kufanya mambo kwa hekima na ufahamu mzuri.
Wito wangu kwa wazazi,
waalimu, viongozi, mitume, wachungaji, manabii, jamii na serikali ni kwamba
kila mmoja aiangalie nafasi yake. Tuna jukumu la kuhakikisha kwamba watoto na
vijana wetu wanazidi kupata maarifa ya Mungu,wanapoendelea kusoma katika elimu
mbalimbali. Tusipuuze mambo ya Mungu; vipindi vya dini mashuleni vipewe nafasi
yake. Watoto na vijana wasisitizwe kwenda kwenye nyumba za ibada. Vifaa vya
kujifunzia elimu ya kiroho navyo vipatikane kwa wingi. Tena kila mmoja wetu awe
mfano bora kwa watoto na vijana wetu. Vijana nao wawe tayari, na waamue
kuwekeza muda wao katika kujifunza. Wawaheshimu viongozi na waalimu wa kiroho
kama inavyowapasa. Hili litadumisha mahusiano kati yao na Mungu, kisha kati yao
na wazazi/walezi.
Mungu awabariki,
Mwl. Stephen Swai
Simu: +255713511544