“Ingawa
Bwana yuko juu, amwona mnyenyekevu, Naye amjua mwenye kujivuna tokea mbali” (Zaburi 138:6)
Unyenyekevu ni ile hali ya kukubali
kuwa chini hata kama una sababu nzuri za kukaa juu. Ni kukubali kukaa chini ya
mamlaka au kanuni au sheria au mfumo Fulani kwa nia ya kujenga. Mtu akikubali
kukaa kwenye mamlaka ya Mungu, maana yake ni mnyenyekevu kwa Mungu. Katika hali
ya ubinadamu, unyenyekevu umahusishwa sana na umaskini kwani mara nyingi mtu
mwenye shida analazimika kujishusha kwa wale wenye navyo ili watoke kwenye
shida. Kwenye mazingira ya kazi, wafanyakazi hulazimika kunyenyekea kwa mabosi
wao ili waendelee kuwa na kazi; kwenye maswala ya kijeshi pia, wakuu
hunyenyekewa na wale walio chini yao.
Unyenyekevu tunaojifunza hapa si huu
unaosababishwa na mazingira; hapa tunaangalia unyenyekevu kama tabia ya mwamini
inayosababishwa na usafi wa moyo. Hakuna mtu anayeweza kukaa na Mungu bila kuwa
na tabia hii. Isaya 57:15 inasema, “Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye
milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali
palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu
na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao
waliotubu.”
Mtu mwenye kiburi na kujiinua hawezi kukaa na Mungu au kuwa juu au
kufanikiwa. Mithali 29:23 inasema “Kiburi cha mtu kitamshusha; Bali mwenye roho
ya unyenyekevu ataheshimiwe” Nimeona watu wengi wanyenyekevu wakipata heshima
sana. Jifunze kwa watumishi wote waliofanikiwa katika Biblia utagundua kwamba
hakuna hata mmoja aliyekuwa na kiburi, wote walikuwa wanyenyekevu Mungu
akawainua. Hivyo ni lazima sisi kama waamini tujifunze unyenyekevu. Tuwe
wanyenyekevu kwa Mungu na kwa watu wanaotuzunguka. Kimsingi, tuwe na maisha ya
unyenyekevu.
Unyenyekevu una mambo mengi unafanya
katika maisha yetu kama tulivyoona, yaani:
a. Unatupa nafasi ya kupewa neema na Mungu. Mithali 3: 34 inasema, “Hakika yake huwadharau wenye dharau, Bali
huwapa wanyenyekevu neema”
b.
Unatupa kuwa na
uhusiano mzuri na wengine: Watu watakuheshimu, utakuwa na ujasiri kwa watu, Watu
watakupenda Mithali 15:33 inatuambia, “Kumcha Bwana ni maonyo ya hekima; Na
kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu.” Kumbe hakuna heshima bila unyenyekevu
kwanza.
c.
Faida kubwa
zaidi ni kutupa kukaa na Mungu
Unyenyekevu
unatupa kuhudumiana: Mtumishi wa
Mungu Petro anatuambia, “…Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate
kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa
wanyenyekevu neema. Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili
awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye
hujishughulisha sana kwa mambo yenu.” (1Petro 5:5-7) Unyenyekevu ndio chanzo
cha kuinuka au kuinuliwa kwa mtu wa Mungu. Yeyote asiye mnyenyekevu hakika atapingwa
na Mungu hata kushushwa chini.
Kunyenyekea chini ya mkono wa Mungu
utasababisha Mungu atuinue kwa wakati wake. Neema ya Mungu ipo pamoja na wote
wanaonyenyekea. Katika Mathayo 23:12 Yesu anasema, “Na ye yote atakayejikweza,
atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa.” Maisha ya kujinyenyekesha
ndiyo maisha ya Mkristo. Yesu mwenyewe kama kielelezo chetu alijinyenyekesha
hata mauti ya msalaba ndipo sisi tukainuliwa pamoja naye (Wafilipi 2:6-8) Neno
linasema, “ingawa
ni Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata” (Waebrania 5:8) Baada
ya kunyenyekea alikirimiwa jina lipitalo majina yote (Wafilipi 2:9), tena
ametufanyia wokovu wa milele hata akatajwa na Mungu kama kuhani mkuu kwa mfano
wa Melikizedeki. (Waebrania 5:9)
Hebu tuuangazie macho mfano huu
tunaoupata katika Luka 18:10 – 14: “Watu
wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza
ushuru.Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru
kwa kuwa mimi si kama watu wengine,
wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga
mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza
ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali
alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie
radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake
amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila
ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”
Hapa tunaona jinsi ambavyo Farisayo alipata hasara kwa sababu ya
kiburi, kujihesabia haki kwa kutimiza taratibu za dini. Yeye alijiona “si kama wengine” ni kweli hakuwa kama wengine lakini haikupasa
iwe sababu ya kujihesabia haki. Tunapofanya vizuri au kutimiza majukumu Fulani
katika kanisa Mungu anategemea tuendelee kunyenyekea na kuwathamini wengine.
Mtoza ushuru yeye alijishusha, akakaa mbali kwa unyenyekevu (alipiga magoti) na
kumwomba Mungu akimwambia “uniwie radhi mimi ni mwenye dhambi” Hii ndiyo siri
ya kufanikiwa kwake. Mimi na wewe leo tunakwendaje mbele za Mungu? Tunawaonaje
wengine ambao hawafanyi kwa viwango kama sisi?
Katika kitabu cha 1Samwel 2:3 tunakutana
na maneno haya, “Msizidi kunena kwa
kutakabari hivyo; Majivuno yasitoke vinywani mwenu; Kwa kuwa Bwana ni Mungu wa
maarifa, Na matendo hupimwa na yeye kwa mizani.” Kumbe Mungu ndiye hupima
matendo yetu, hatuna haja ya kujisifia kwayo. Tukiyabeba matendo yetu kama
sababu ya kujihesabia haki tutajikuta tumebaki wenyewe, kwani hakuna hata tendo
moja linalotosha kulipa gharama ya uhai wetu. Ni vema tukamwishia Mungu kwa
unyenyekevu, na shukrani kwa yale aliyotuwezesha kufanya.
Mungu hawezi kumwacha mnyenyekevu: “Naye mnyenyekevu Mungu atamwokoa.” (Ayubu
22: 29). Hata kama unapita katika magumu kiasi gani, ukiendelea kunyenyekea
mbele za Mungu kwa moyo uliopondeka hakika Mungu hatakuacha. Daudi alipoona
ameanguka, hakuanza kujitetea. Alishuka akamlilia Mungu kwa kuyararua mavazi
yake (ishara ya unyenyekevu), na Mungu akamsamehe. Kutenda dhambi kisha
ukaficha na kujifanya mtakatifu si Ukristo huo, ni unafiki mbaya, ni kiburi. Ni
vema ukajinyenyekesha ukaomba Mungu akusamehe, utakuwa salama.
Angalia mafanikio yasiufanye moyo wako ukainuka ukamsahau Mungu
aliyekutoa kwenye utupu na kukubariki (Kumb. 8:11-14). Watu wengi huwa
wanyenyekevu wakiwa hawana kitu ila wakifanikiwa wanapoteza heshima kwa Mungu
na watumishi wake. Maisha yetu kama waamini hayapaswi kuwa hivi. Tunapaswa
kuendelea kunyenyekea hata kama tutabarikiwa kwa kiasi gani. Mungu anataka
tutafute pamoja naye, tumiliki pamoja naye, tutumie pamoja naye na tuendelee
kuishi pamoja naye hata tukipoteza. Maisha ya Ayubu yanatufundisha somo la
unyenyekevu mbele za Mungu.
Maisha baada ya kuokoka ni maisha ya unyenyekevu kwa Mungu, kwa
viongozi wa kanisa, kwa watu wanaotuzunguka kulingana na Neno la Mungu. Ndani
ya maisha ya wokovu tunapaswa kuwa na mioyo ya toba na unyenyekevu. Kila wakati
tuhitaji rehema za Mungu, na kumtii Mungu kutoka moyoni. Tuwape heshima
viongozi na kuwasikiliza katika mapenzi ya Mungu. Petro anaagiza na kusema, “ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate
kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa
wanyenyekevu neema.”
Unyenyekevu unatupa kuweza kuhudumiana: Katika kanisa sisi ni viungo, kila mmoja na
mwenzake; hivyo hatuwezi kuepuka kuhudumiana. Katika unyenyekevu kila mmoja
wetu akiwatanguliza wengine, tutahudumiana. Paulo anaeleza jinsi ambavyo
amekuwa “akimtumikia Bwana kwa
unyenyekevu wote” (Matendo 20:19) Je, sisi tunatumika kwa jinsi gani? Nabii
Sefania anasema, “Utafuteni unyenyekevu” (Sefania 2:3) Huwezi kuwa mhudumu
ndani ya nyumba ya Mungu, na ukatumika kwa mafanikio, bila kuwa mnyenyekevu.
Jifunze unyenyekevu. Paulo anahitimisha kwa kusema, “Msitende neno lo lote kwa
kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu
mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.” Wafilipi 2:3