Wapendwa Nawasalimu katika Jina la Yesu!
Nianze kwa kuuliza "Je! Kristo
amegawanyika?" (1Wakorintho 1:13) Je, Yesu wa CASFETA TAYOMI ni
yupi, na wa CASFETA ni yupi? Je, ni Yesu wawili tofauti? Kwa nini mgogoro kati
ya makundi haya mawili hauishi? Maswali haya yamenijia baada ya kushuhudia
visanga kadhaa kwenye shule za sekondari kwa miaka mingi sasa. Nakumbuka
mkuu mmoja wa shule alisema, “katika shule yangu sitaki kusikia mgogoro wowote
wa vikundi vya dini, hasa kwa walokole kwa sababu huwa hawapatani siku
zote”
Nimekuwa nikitafakari juu ya hatima ya tofauti kubwa zinazojitokeza katika makundi haya mawili yenye jina moja. Nilichogundua ni kwamba hatima yake si njema, zaidi ni kuendelea kuligawa na kulidhohofisha kanisa. Watoto na vijana wakijengwa katika misingi ya migogoro na kutoelewana hawataweza kusimama pamoja tena, labda ifanyike toba na matengenezo mapema. Kwa kipindi kirefu sasa, kumekuwa na migogoro mingi mashuleni na vyuoni ambayo badala ya kutafutiwa tiba ya kudumu, imekuwa ikifunikwa tu ili maisha yaendelee. Kuna mshangao mkubwa kwa wengi juu ya kutokuelewana kwa walokole. Wengi huuliza: "Kama wana Yesu kweli, mbona hawaelewani." Baadhi ya wakuu wa shule wamekuwa wakikosoa vikali hali ya uhasama iliyopo miongoni mwa CASFETA hizi mbili.
Sijataka kuamini kwamba mithali isema “Baba
za watu wamekula zabibu kali, na meno ya watoto wao yametiwa ganzi” itatimia
kwetu. Najua viongozi wengi wa kanisa huwa hawapendi mjadala katika swala hili.
Naamini hili haliwazuii watu kuendelea kusema kile wanachokiona juu ya kanisa
la Mungu. Ili kanisa la Mungu lijengeke katika utakatifu na umoja ni lazima
mambo yote yawe sawasawa. Migogoro miongoni mwa vijana waliookoka mashuleni na
vyuoni si ishara nzuri. Ni ishara kwamba kuna nyufa ambazo hazijazibwa.
Migogoro ikitawala kati ya ndugu, inakuwa rahisi wao kwa wao kuangamizana. Adui
pia anapata nafasi kwa urahisi.
Kuwa na vikundi viwili au hata zaidi ya viwili haina
tatizo, inaweza kuwa njia nzuri kabisa ya kupanua wigo wa huduma, lakini
vikundi hivi ni lazima viwe huru. Maana yake viwe na katiba isiyoingiliana na
vingine, vifanye kazi kwa kuheshimu uwepo wa vikundi vingine, kila kimoja kiwe
na misingi isiyoshawishi migogoro na vingine. Ni lazima inapotokea Mungu
ameamua kupanua huduma amani izidi kuwepo. Paulo na Barnaba walipopishana,
hawakuachana kwa ubaya. Kila mmoja alichukua njia yake kwa amani, na hakuna
mahali ambapo mmojawapo alisimama kuusema ubaya wa mwenzake.
Hali sivyo ilivyo kwa CASFETA Tayomi na CASFETA:
vimekuwa ni vikundi vya kuvunjiana heshima, kusemana vibaya hata kuitana waasi,
kushindania matawi, kunyanganyana wahiriki na hata kuvutana wazi wazi. Nina hakika jambo hili si jema, ni baya na
halimpendezi Mungu. Tunapokuwa na viongozi wa wanafunzi wenye uwezo wa kuwasema
wenzao vibaya au hata kuwatendea mabaya, hatujengi kanisa. Ujasiri wa
kushuhudia unapungua, uwezo wa kuishawishi dunia unapungua.
Maono ya CASFETA zote mbili ni mazuri, na yana nafasi ya kuleta mapinduzi makubwa kwa kanisa. Changamoto ni kwamba hakuna amani kati yao. Kunapokuwa na Kamba inayovutwa na makundi mawili, kila kundi kuvuta kuelekea upande wake. Mwisho wadhaifu wataangukia upande wa wale wenye nguvu. Kiroho hali haiku hivyo! Tuliookoka wote tunapaswa kukaa upande mmoja ili tuzidi kuivuta dunia ije kwa Yesu. Tunapovutana sisi kwa sisi ni rahisi kuangukia upande wa shetani. Kwa nini tuwaache Watoto wetu wazidi kuvutana? Bilas haka kuna ugumu Fulani katika kuamua. Katika kutafakari nimegundua mambo machache:
Kwa nini mgogoro huu ni mgumu?
1.
WANAOGOMBANA WAMETOKA
KWENYE FAMILIA MOJA.
Mgogoro kati ya CASFETA (Tayomi) na CASFETA) hauna
tofauti na ule wa ndani ya familia. Watoto wanaweza kugombana lakini mwisho
wanakutana kwa baba na mama mmoja. Wazazi na walezi wa vijana waliookoka wote
walioko mashuleni na vyuoni ni makanisa yetu ya kipentekoste. Wakitoka shuleni
wanakutana kanisani pamoja, na mchungaji wao ni mmoja. Kinachoshangaza ni vita
na malumbano yanayoendelea kushamiri kati ya watoto hawa. Ile hali ya
kugombana shuleni kwa sababu ya vyama na kurudi kanisani kuabudu pamoja inaonyesha
udhaifu katika kanisa.
Baadhi ya watu niliowauliza juu ya jambo hili
gumu, wamenipa majibu mepesi. Mmoja aliniambia, “Hili jambo limeshindikana huko
tulipotokea sidhani kama linawezekana, wanaolisimamia ndio wanaojua zaidi” Nilipotafakari
kauli hii nikagundia kwamba hakuna anayetaka kukubali lawama. Kila mmoja
anataka aonekane ni mwema huku ukweli akiujua. Kinacholeta shida ni hali ya
kutokuelewana ambayo haijapatiwa ufumbuzi. Ninafikiri kuna haja ya kuwapa
vijana na watoto wetu mashuleni na vyuoni ufafanuzi wa kina ili wasije
wakajikwaa.
Hatari kubwa zaidi inajitokeza pale ambapo Watoto wanakataliwa wanakwenda kwa wazazi kutaka msaada au uwezesho kwa ajili ya huduma. Nimeshuhudia baadhi ya wachungaji wakiwakataa wanafunzi waziwazi kwa sababu wanatoka CASFETA Fulani tofauti na ile anayoitaka yeye. Jambo hili limaleta majeraha kwa vijana wengi. Nilikutana na binti mmoja aliyekwenda kuomba mchango wa Injili kwenye kanisa alilokuwa anaabudu, akajibiwa vibaya akaumia. Watoto wa familia moja wanapokosa upendo wa walezi, au wakabaguliwa kwa namna yoyote ile huleta maumivu.
2. SABABU YA KUTOFAUTIANA HAIKO WAZI IPASAVYO
Wengi hawaoni umuhimu wa kuwepo kwa mamkundi
haya mawili kwa pamoja. Swali rahisi ambalo huuliza ni “Ni kwa nini msiwe
pamoja” Ni kweli si lazima kuwa pamoja ikiwa Mungu hajakusudia hivyo, lakini ni
lazima tutofautiane kwa amani. Kuna kanuni moja ya kibiashara ambayo
nimejifunza kwa wafanyabiashara katika masoko makubwa. Mara nyingi maduka
yanayouza vitu vinavyofanana hujikusanya pamoja. Nia yao ni kuwavitua wateja
wengi zaidi ili kila mmoja apate. Huwezi kukuta wakigombana, kila mmoja
hujitahidi kufanya ubunifu wake kuimarisha biashara yake.
Kwa CASFETA (Tayomi) na CASFETA hali sivyo
ilivyo: mvutano ni mkubwa, hakuna anayetaka kumwona mwenzake. Kwenye tawi la
CASFETA, CASFETA (Tayomi) akijitokeza ni shida, na vivyo hivyo kwa CASFETA
(Tayomi). Kila mmoja anataka atawale yeye. Nilipata mgogoro mmoja wa tawi
lililoanzishwa na CASFETA ila hawakujishughulisha kulihudumia, Tayomi
walipokuja wakawahudumia na mwisho wakaligeuza tawi. Baadaye CASFETA walipojua,
walikuja kwa hasira na kusababisha mgogoro mkubwa. Mambo hay ani chukizo kwa
Mungu.
Fundisho linapokuwa moja inakuwa rahisi kwa
washirika kuhama kutoka kundi moja kwenda jingine. Wengi waliokuwa katika moja
ya makundi haya wakiwa sekondari (O-Level) waliingia kwenye kundi jingine
wakiwa A-Level na hawakuona tofauti yoyote. Vijana wengi hawaoni sababu ya kutofautiana
japo wameambiwa mengi. Hali ya kutokuwa na sababu za msingi za kutofautiana
imeleta ugumu katika kulitangua fumbo hili. Nafikiri ni vizuri sababu
zingeangaliwa kwa undani Zaidi ili kuona kama bado zinaweza kueleweka kwa
kizazi hiki na kile kinachokuja. Yapo mambo yanayoweza kueleweka kwenye kizazi Fulani
na yasiweze kueleweka kwenye kizazi kingine.
Katika mazingira hay ani lazima matengenezo
yafanyike ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kwa kizazi kisichojua
chimbuko la jambo. Alipoinuka Farao asiyemjua Yusufu Wana wa Yakobo waliingia
kwenye utumwa. Kama sababu zikiwa ni za mtu binafsi, mtu huyo akishaondoka ni
lazima aache mateso. Akiwepo anaweza kujirudi na kusema tofauti, asipokuwepo waliopo
ni lazima wasimame kuziba nafasi yake.
3.
NI JAMBO LA KIHISTORIA
Kizazi kilichokuwepo
wakati makundi haya yanaanza haikosi wanajua mambo mengi kuhusu makundi haya.
Kizazi kinachoibuka na vitakavyokuja vitaathiriwa na umbali wa muda, hivyo
tafsiri yao juu ya tofauti zilizopo ni lazima iwe tofauti na ya wale
walioshuhudia mambo yote yakitendeka. Nilichogundua katika utafiti wangu ni
kwamba mgawanyiko juu ya makundi haya uliimarishwa Zaidi na mpasuko uliokuwepo
ndani ya kanisa kwa kipindi hicho. Majeraha ya mgogoro mkubwa wa kanisa
yaliendelea kuchokonolewa na uwepo wa makundi haya mawili.
Si jambo rahisi kurekebisha jambo la kihistoria.
Inagharimu kizazi cha mashuhuda kukaa na kizazi kinachoibuka ili kuweka mambo
sawa. Kizazi cha mashuhuda kikiondoka bila kusuluhisha au kuandika ushuhuda wao
katika kile kilichotokea ni rahisi kuleta shida kwa kizazi kinachofuata. Ninafikiri
kuna haja ya kizazi cha mashuhuda kulitazama jambo hili kwa kina na kupata
muafaka wake. Migogoro ikishazoeleka mara nyingi huwa kawaida lakini kiroho ni chanzo
cha anguko.
Kila upande katika migongano inayoendelea,
hujihesabia haki kihistoria. Hili haliondoi ukweli kwamba mgogoro wowote husababishwa
na mambo kutokwenda sawa. Hivyo ni lazima kuna mahali mambo hayako sawa. Mabaya
mangi yaliyomkuta Esau katika Maisha yake yalisababishwa na kule kuuza uzaliwa
wake wa kwanza. Kwa hiyo watu wasiojua kwamba Esau alishauza uzaliwa wake wa
kwanza, ni rahisi kumlaumu Yakobo. Ni muhimu mambo yaliyotokea yakawekwa sawa.
Suluhu ya kudumu ikapatikana.
Kanisa kama mzazi na mlezi wa vijana ni lazima
linie mamoja, na kuhakikisha linaondoa tofauti zote zinazoleta changamoto miongoni
mwa vijana. Ipo sumu mbaya ya matengano na uhasama inaendelea kutafuta njia ya
kuvuka kwenda kwenye kizazi kinachofuata. Ninaamini kwa msaada wa Mung una kwa kuunganisha
maombi na jitihada za pamoja hatutaruhusu Watoto wetu wakaingia kwenye magumu
tuliyopitia. Ni wito wangu kwa maaskofu
wote, wachungaji wote na kila aliye na nafasi katika kanisa la Mungu lililo
hai, kwamba tujitoe kuangalia mstakabali wa kanisa la kesho.
Haitoshi kujaza makanisa leo, na kupata sadaka
za kutosha leo, na kufurahia mafanikio leo; yatupasa kuiangalia kesho. Uamsho
endelevu ni lazima ujengewe misingi itayorithishwa kizazi hadi kizazi. Wasomi
wengi wanajikuta hawana mizizi katika Imani kwa sababu hawakupata watu wa
kuwalelea walipokuwa mashuleni. Wengi wamejikuta wakijeruhika kwa sababu ya
mambo wanayokutana nayo mashuleni na vyuoni. Kama kanisa tukiamua kuiangalia
kesho, migogoro kama hii ya CASFETA haitaachwa tu. Ni lazima iangaliwe kwa
ukaribu ili kuwapa Watoto wetu fursa ya kupendana, kutumikiana, na kupendwa na
wachungaji wote bila ubaguzi.
Mungu akubariki!