Friday, 18 October 2024

MWANAUME KWENYE NAFASI YA "MUME"

Mume ni mwanaume aliyeoa kwa kuzingatia vigezo na taratibu za kijamii, kishria na za kiroho. Mume si rafiki wa kiume (boyfriend), hawara, wala si mzazi mwenza (kwamba tu umezaa naye). Ili mtu awe mume ni lazima akamilishe taratibu za kijamii, za kisheria na za kiroho katika kuanzisha ndoa.

Ndoa kibiblia, ni muunganiko wa kudumu kati ya mtu mke na mtu mume; na mwanzilishi wa muunganiko huu ni Mungu mwenyewe. Katika Mithali 19:14 tunasoma, “Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana.” Hivyo, katika kuanzishwa kwa ndoa kibiblia ni lazima Mungu ahusike. Tangu Agano la kale hata sasa, tunaona Mungu akihusika kwa ukaribu sana kwenye ndoa. Ndoa ya kwanza aliifunga mwenyewe kati ya Adam una Eva.

Ibrahimu alipewa Sara kuwa mkewe, Isaka alipewa Rebeka kuwa mkewe, Yakobo alipewa Lea na Raheli kuwa wake zake. Hata kama walijihusisha na wanawake wengine, bado hawa walibaki kuwa na nafasi ya pekee kwao. Kwa hiyo, kuwa mume kwa mke si jambo rahisi na la kawaida, ni jambo lenye kusudi la Mungu ndani yake.

Ukifuatilia ndoa hizi niliziozitaja utagundua kwamba familia zilihusika kwa ukaribu sana katika kuianzisha ndoa. Mfano Rebeka aliulizwa na wazazi wake kama yuko tayari kuambatana na yule aliyetumwa kuja kumchukua. “Wakamwita Rebeka wakamwuliza, Je! Utakwenda na mtu huyu? Akasema, Nitakwenda.” (Mwanzo 24:58) Sheri ana kanuni za jamii zao nazo zilizingatiwa kwa karibu sana.

Maagizo ya Mungu kwa Mume

                                                                                      i.          Kuambatana na Mkewe

Makubaliano kati ya mwanaume na mwanamke katika mahusiano siku zote yamekuwa yakizingatiwa. Tangu zamani iliwalazimu, mwanaume na mwanamke kukubali kuambatana pamoja. Kibiblia, mume ni lazima aambatane na mkewe na kumpokea kama sehemu ya mwili wake (Mwanzo 2:24, Waefeso 5:31, Mathayo 19:5). Tangu uumbaji, mwanamke ni sehemu ya mwili wa mwanaume.

Mungu aliuchukua ubavu mmoja wa Adamu na kumuumba Eva. Naye Eva alipoletwa kwa Adamu, kwa furaha, na kwa kumkubali Adamu lisema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume.” Kule kutolewa katika mwanaume ndiko kulikomfanya Eva aitwe mwanamke.

Mwanaume akimwona mkewe katika mtazamo huu ni rahisi kuambatana naye. Kuambatana kunahusu mambo yote katika Maisha: yaani kimwili na kiroho. Mume hana maisha binafsi tena, kila kitu ni shirika. Kwa kukazia Zaidi Paulo anasema, “Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe.” (1 Wakorintho 7:4)

Kuambatana kati ya mume na mke, ni kwa lazima. Japo changamoto ni kubwa katika kizazi hiki, inawezekana kuliko vizazi vyote. Ile neno aliloambiwa Eva kusema “tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.” Limekuwa gumu kwa wanawake walio wengi. Hivyo mashindano, chuki, na kutendeana kwa hiyana kumetawala kati ya wanaume na wanawake.

Kuambatana ni jambo pana katika Maisha ya wanandoa.  Mume ni lazima akubali na ajitoe:

Kuambatana na mkewe katika kuhudumiana, huku kunahusisha kujitoa kwa kila mmoja kwa mwenzake. Huduma ya tendo la ndoa ni moja ya huduma za msingi katika ndoa. Paulo anasema, “msinyimane” (1 Wakorintho 7:5). Kuhudumiana kiroho na kimahitaji na mengineyo pia ni sehemu ya kuambatana kwa wanandoa.

Kuambatana na mkewe katika kazi; huku ni kuunganisha mikono pamoja katika kuzalisha. Kazi za nyumbani, za kiuchumi, za kanisa na nyinginezo ni lazima zifanyike katika ushirika wa mume na mke katika ndoa. Mke n msaidizi, mume ni mwongoza njia. Wote wawili ni wasafiri katika chombo kimoja kiitwacho ndoa au familia. Kutiana moyo, kusaidiana, kuwezeshana, na kupeana nafasi katika kazi katika kuambatana hakuepukiki.

Kuambatana na mkewe katika mapato na matumizi; hili ni eneo linalohusu uchumi katika ndoa. Kimsingi uchumi wa ndoa hujengwa na mume na mke, hivyo wote ni lazima wahusike vilivyo katika kupata na kutumia mali zinazozalishwa. Japo jukumu la kuzalisha amepewa Adamu, Eva hawezi kujiweka pembeni kwani naye ni msaidizi. Na Zaidi ni mwili mmoja na Adamu.

Kuambatana na mkewe katika huduma na maisha ya kiroho (kiimani): Imani hubeba hatima ya mwanadamu. Tena huathiri maamuzi ya mtu moja kwa moja. Ikitokea mke na mume hawako pamoja kiimani au kihuduma, kuambatana huwa kugumu. Mume ni lazima akubali kuambatana na mkewe katika mambo ya kiroho ili wawe na hatima njema, vivyo hivyo na mke. Maombi, kusoma neno, utoaji, kutumika, na kumtafuta Mungu kwa pamoja ni msingi wa Maisha ya kiroho katika ndoa.

Kuambatana na mkewe katika malezi ya watoto (kabla na baada ya kuzaliwa): huku kunahusisha kupanga idadi ya watoto, aina ya malezi ya kuwapa watoto, jinsi ya kukidhi mahitaji ya Watoto, na jinsi ya kutunza maadili ya familia.  Mambo haya hayawezi kufanyika kwa ufanisi bila maridhiano na maamuzi ya pamoja. Mume bora ni yule anayeweza kusafiri salama akiwa bega kwa bega na mkewe pamoja na Watoto.

Kuambatana na mkewe katika mipango (iweni na nia moja) na kukuza uchumi wa ndoa na familia: katika ndoa ni lazima kupanga pamoja. Mume atoe mawazo yake, mke naye atoe yak wake. Ndoa iliyogawanyika mara nyingi, huanzia kwenye mipango. Mipango ikishatofautiana, matumizi hayawezi kwenda sawa. Kushirikishana mipango ni njia muhimu katika kudumisha kuambatana. Mume ni lazima amshirikishe mkewe mipango yote aliyonayo.

Mume pia ana jukumu kuambatana na mkewe katika matatizo mfano magonjwa, misiba na mengineyo. Mwanaume anayekimbia matatizo, hana sifa ya kuwa mume. Kuoa ni kukubali kuchukua madhaifu ya mke, na kumshirikisha mke udhaifu wako. Kutafuta suluhu ya matatizo ni moja ya jukumu la msingi la mume katika ndoa.

Mungu ni lazima aambatane na mkewe katika kusaidia ndugu na kuwatunza wazazi. Japo hili linakwenda kwa pande zote mbili, ni lazima mume awe mstari wa mbele kuwasaidia ndugu wa mkewe. Kuambatana kunadai kubebeana mizigo. Katika familia zetu za kiafrika tuna majukumu Fulani ambayo hatwezi kuyaepuka, hivyo kusaidiana ni kwa lazima.

Haya ni baadhi ya maeneo ya msingi, yanaweza kuwepo mengine zaidi. Jambo la msingi hap ani kujua kwamba kuwa ‘mume’ ni kuwa mshirika wa karibu na wa pekee kwa mkeo. Mke ameumbwa kufurahia ushirika na kujaliana katika mahusiano. Hajaumbwa kupambana peke yake, hivyo kuambatana naye ni njia muhimu katika kujenga amani ya ndoa. Mume naye hawezi peke yake, hata  Adamu yalimshinda, hivyo ni lazima mke akubali kuambatana na mumewe.

                                                                                          ii.          Kumpenda Mkewe 

Paulo anasema, “Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. (Waefeso 5:28-29)

Hapa Paulo anasema juu ya kuwapenda wake zetu kama miili yetu, hili ni fumbo zito kwa mume. Waume wote tungeweza jambo hili, ndoa zetu zingekuwa paradiso. Kizazi chetu kinashangaza sana, kwani kesi za waume kuwapiga, kuwaumiza, kuwaacha, wakati mwingine hata kuwaua wake zao zimekuwa nyingi sana. Paulo amatuambia “haiwezekani mtu akauchukia mwili wake. Bali huchukua jukumu la Kuulisha na kuutunza.

Kutokea kwa matukio haya mabaya kunadhihirisha kwamba wanaume wengi hawajawapokea wake zao kama miili yao wenyewe au hawana upendo wa kweli kwa wake zao. Mume aliyempokea mkewe kama mwili wake na kumpenda ni lazima awe na upendo ulio hai. Yaani:

v    Upendo kwa mkewe huambatana na kuhakikisha kwamba anakula na anapata mahitaji yake yote (matunzo). Hata kama ana kazi yake usikubali mkeo akajigharamikia kila kitu, tumia fedha yako kumlisha na kumnunulia mahitaji yake. Kumjali mke kimahitaji ni jukumu la msingi la manaume. Mume ni lazima awe na macho ya kuona mahitaji ya mkewe.

Si lazima mke aombe kila kitu. Vitu vingine ukiona anavihitaji mnunulie naye atajisikia kupendwa kila wakati. Kama mume unayempenda mkeo, hupaswi kuishia kwenye maneno tu, ni lazima upendo wako uambatane na kujali mahitaji. Ukumbuke kabla ya kumwoa mkeo alikuwa anapewa mahitaji na wazazi wake na pengine wanaume wengine, au kujihangaikia mwenyewe. Hakikisha unazipa mapengo yote kwa kufanya Zaidi ya wote.

 

v    Upendo unadai kujitoa: Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake. (Waefeso 5:25). Kujitoa ni kwenda Zaidi ya ile hali ya kawaida ya kutimiza majukumu. Unapofika mahali kama mume ukatafuta muda wa ziada, ukafanya zaidi, ukakubali kuumia kwa sababu ya mkeo basi unakuwa unautimiza upendo.

Linapotokea jambo gumu kwa mkeo, hakikisha unakuwa mstari wa mbele kama mume kutafuta utatuzi. Hata kama litakugharimu kupoteza baadhi ya vitu, Mungu atawajalia neema mtapata vingine baada ya jambo hilo kupita. Kazi zipo tu, ila kujitoa kumsaidia mwenzako wakati wa taabu au hata mazuri yenye gharama ni muhimu.

NiIisikia habari za kijana mmoja (mume) ambaye alimwacha mkewe hospitalini akiwa mahututi kwa sababu ya kuogopa hasara ya kazi aliyokuwa anaifuatilia. Mkewe alipotoka hospitalini, alikuwa na uchungu mwingi sana kwa kuona mumewe amethamini kazi kuliko Maisha yake. Kurekebisha kosa kama hilo, ni gharama kubwa kuliko kuacha faida ikapita.

v Upendo unadai kusamehe na kusahau: Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao. (Wakolosai 3:19) Wanaume wasio na moyo wa kusamehe mara nyingi huwatendea wake zao mabaya. Upendo hauhesabu mabaya (1 Wakorintho 13:4 “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya”

Hivyo, mume mwenye upendo ni lazima ajifunze kumsemehe mkewe. Ni muhimu kukumbuka wamba, wanawake ni watu wa mahusiano zaidi kuliko kazi, hali wanaume ni watu wa kazi zaidi. Kupishana katika mazingira kama haya ni kawaida. Wanawake huwa hawapendi kukosea, hivyo kusamehewa wakikosea ni lenye nafasi kubwa kwenye maisha yao.

v    Upendo unadai heshima: Paulo anafundisha  na kusema, “Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe. (1 Petro 3:7). Mume ana jukumu la kuitunza heshima ya mkewe kwa kumvisha vizuri, kumpamba, kumwendeleza, kumpa nafasi na kumsikiliza.

Kwa sababu ya maumbile yao au hali ya maisha au historia wakati mwingine mke anaweza kuonekana kama hana heshima. Kwa mume, mke ni lazima awe malikia katika hali zote. Mume hatakiwi kumvunjia mkewe heshima, kwa kwenda nje ya ndoa, vivyo hivyo mke. Kama mume, ni muni kuyaheshimu mawazo ya mkeo, hisia zake, na nafasi yake kwa ujumla.

v    Upendo unaambatana na kumlinda mkeo: Kwa hiyo jihadharini roho zenu; mtu awaye yote asimtende mke wa ujana wake mambo ya hiana. (Malaki 2:14-15) Wanapoinuka watu kumshambulia mkeo usinyamaze, usiwape ndugu (wazazi, wadogo zako, dada zako au marafiki) kumshambulia mkeo. Katika changamoto zote, tunza heshima ya mkeo (chukua aibu yake, na Mungu atakubariki). Zaidi sana usimgeuke na kumtendea mambo ya hiana. Mweke mkeo kwenye mzingira salama, na hakikisha anakuwa salama wakati wote.

Kila mwanamume au mwanamke anapaswa kutunza heshima ya ndoa: Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu. (Waebrania 13:4) Usafi wa ndani na wa nje ni muhimu katika ndoa. Usafi wa tabia ni wa muhimu zaidi sana. Tabia za uzinzi na uasherati zimeharibu mahusiano ya wanadoa wengi, na yameleta aibu isiyofutika.

Mambo ya kufanya kama mume ili mkeo akufurahie

Pamojana maagizo haya makubwa mawili tuliyokwisha kuyaona, kuna mambo kadhaa ya kiutendaji yatakayomfanya mume awe mtu wa kutamanika kwa mkewe kila wakati.

1.               Fanya kazi kwa bidi ili kukidhi mahitaji ya familia, kwa kiwango chako. Mke hujisikia salama akiwa na mume mpambanaji na anayezalisha.

2.               Timiza wajibu wako kwa jamii, mfano kanisani au kazini au pale unapoishi. Mke hujisikia vizuri sana akiona mumewe anaheshimiwa na kusemwa vizuri na watu.

3.               Jifunze kumpongeza mkeo akifanya vizuri, na kumkosoa kwa upendo akifanya vibaya. Hili litampa uhakika wa wewe kuambatana naye, hivyo kuvutiwa na wewe zaidi.

4.               Jifunze kumsikiliza na kuongea na mkeo. Hili ni la muhimu sana, mwanamke hujisikia kama malkia akiona mumewe ametulia akimsikiliza. Mume mwema humsikiliza mkewe kwa uvumilivu na busara. Wanawake wengi hupenda kuongea kuliko kusikiliza. Japo wapo ambao hupenda kusikiliza pia, hivyo msome mkeo na kuhakikisha unakwenda naye alivyo.

5.               Msifie mkeo kwa kumpa majina mazuri, sifia umbile lake na kumtia moyo kila wakati. Mwite mkeo “mpenzi, laazizi, malikia, mke; ikiwezekana weka na kiingereza kidogo kama “honey”, “sweetie” “baby” “sweetheart” na mengine. Haya humpa mke ujasiri na kujikubali zaidi, hivyo kila wakati atatamani uwe naye ili umsifie zaidi.

6.               Mnunulie mkeo zawadi za hap ana pale. Hili litampa kukuamini zaidi, na kuona kumbe unamwaza kila wakati.

7.               Jitahidi kumtosheleza mkeo katika tendo la ndoa. Hapa niongee kwa herufi kubwa “kilichomtoa mkeo kwao pamoja na mengine yote, nit endo la ndoa. Hakikisha kama mume unaongeza ufanisi kila siku. Mkeo atakufurahia sana ukimpa kile anachokihitaji chumbani mwako.

8.               Mwamini mkeo, japo wapo wanawake wasioaminika, tunajua aliyetoka kwa Mungu ni wa kuaminika. Mke akiaminiwa kuna asilimia nyingi za kufanya vizuri kuliko asipoaminiwa. Mpe uhuru, akikuambia jambo likubali bila kuona shaka. Kama una shaka na jambo mwambie wazi ili akupe maelezo. Wanawake ni wasiri lakini wapewa uaminifu, ni lazima walipe uaminifu.

9.               Jenga urafiki wa karibu na mkeo, wakati mwingine muwe na muda wa kucheza, kutaniana kidogo, kukumbushana mambo mbalimbali na mengineyo.

10.            Jifunze kumshukuru mkeo kwa huduma anazokupa mfano tendo la ndoa, chakula, kukufulia, kusafisha ndani, kukutunzia vitu, kulea Watoto na mengineyo.

11.            Pale inapowezekana jiepushe na yale asiyoyapenda, na kuweka muda kwa yale anayoyapenda.

12.            Usimtanie kwenye madhaifu aliyo nayo. Ukifanya hivyo unaweza kumuumiza moyo na kuleta hisia tofauti.

13.            Usimlinganishe mkeo na wanawake wengine, mkubali kama alivyo na mzungumzie yeye zaidi ukiwa naye. Epuka kuwasifia wanawake wengine ukiwa na mkeo.

14.            Ipende familia, ikiwa ni pamoja na kuwahudumia watoto na ndugu. Mke hufurahishwa sana na mume anayeipenda familia. Niliongea na binti mmoja akaniambia moja vitu vinavyomuumiza duniani ni kuona baba yake hajali familia yake. Usilete maumivu kama haya kwenye ndoa yako.

15.            Jiamini na simamia maamuzi yako. Mke huwa hapendi kuona mumewe anatawaliwa na watu wengine. Uthabiti na ujasiri wa kuamua humtia moyo mke.

16.            Uwe mkweli kwa mkeo. Hakuna ukweli ambao mkeo anayekupenda kwa dhati atashindwa kuchukuliana nao. Uongo ni sumu mbaya sana, ukimdanganya kisha akaja kuujua ukweli itakuwa mbaya mara mbili ya kumwambia ukweli.

17.            Usikae mbali na mkeo kwa muda mrefu bila sababu za msingi na makubaliano ya pamoja; ikitokea inakulazimu, hakikisha unakuwa na mawasiliano ya mara kwa mara.

18.            Msaidie mkeo kazi za nyumbani, hasa akiwa amelemewa Na majukumu, amechoka, au anaumwa. Hii itmfanya akuone kama rafiki yake wa karibu sana.

19.            Pale inapowezekana, uwe na mtoko na mkeo; mara kwa mara uwe na faragha naye. Huyo ndiye make wa ujana wako. Kuambatana naye, kutembea pamoja naye, kwenda kanisani pamoja naye, kula pamoja naye, na mengine kama hayo, huongeza sana ladha ya mahusiano.

20.            Usiogope kuwa uchi mbele ya mkeo. Kuoga pamoja ni dsturi nzuri kwa wanandoa. Kuwa huru kwa mkeo Ni ishara ya wazi kwamba unamwamini, na umejitoa kwa ajili yake. Hii inaongeza furaha na mahaba kwenye ndoa.

21.            Dumisha ukaribu na mkeo. Usipende kukaa mbali naye muwapo pamoja. Mkumbatie, mbusu, ongea naye kwa kamnong’oneza. Hili litampa kuona kwamba unamkubali Na hatimaye naye atajibu mapigo.

22.            Heshimu hisia zake - usiwe mtu wa kulazimisha mambo bila sababu. Kama Kuna ulazima kwenye jambo Fulani tumia lugha nzuri kulizungumza, mweleweshe. Usitake kusikilizwa wewe tu. Wakati mwingine mwenzako naye ana namna anatamani mambo yaende. Akikuhitaji pia Ni vizuri ukapatikana.

MWANAUME KWENYE NAFASI YA "MUME"

Mume ni mwanaume aliyeoa kwa kuzingatia vigezo na taratibu za kijamii, kishria na za kiroho. Mume si rafiki wa kiume (boyfriend), hawara, wa...

Powered By Blogger