Monday, 16 January 2017

MADHARA YA RUSHWA (UFISADI, CORRUPTION, BRIBERY) KWA TAIFA


Mithali 29:4 “Mfalme huithibitisha nchi kwa hukumu; Bali yeye apokeaye rushwa huipindua.”


Rushwa/Ufisadi (Corruption) – Ni kukosa uaminifu na kutumia vibaya mamlaka, au ni matumizi yasiyo halali ya ofisi kwa jili ya kujinufaisha mwenyewe. Mla rushwa (corrupt) ni mtu aliyeamua mwenyewe kutumia nafasi yake ya uongozi, au ofisi kwa manufaa binafsi. Rushwa huwa inatumika kama msukumo wa kupotosha hukumu na kuwatolea wenye haki, haki zao; kisha kuwapa wasiohaki nafasi. Tangu zamani watu maskini, wajane, mayatima walinyimwa haki zao kwa sababu ya rushwa; na jambo hili limekuwa likimuudhi sana Mungu.

Rushwa/ufisadi hubeba sura mbali mbali, inaweza ikawa kwa mfumo wa hongo yaani kutoa fedha au mali kwa ajili ya kushawishi maamuzi Fulani yasiyo halali au sahihih kufanyika. Katika nyakati hizi pia tuna aina nyingine ambayo imekuwa ikisemwa sana na mabinti wanaokwenda kuomba kazi maofisini – Rushwa ya ngono.

Mfumo mwingine ni ule wa kuchota hela kutoka kwenye serikalini kwa kutumia mgongo wa miradi na shughuli mbalimbali za serikali. Au kupunguza hela za matumizi ya serikali na kujiwekea kwa matumizi binafsi. Kutumia ofisi za uma kwa manufaa ya kibiashara binafsi, kujiwekea rasilimali ambazo zilipaswa ziwe za wengi mfano mashamba na viwanja.

Mara nyingi wanyonge na maskini wasio na uwezo wakutoa rushwa ndio huteseka na kuishi maisha magumu, huku wachache wenye fedha wakifanya wanavyotaka. Hali hii ni hatari sana kwa maisha ya watu na taifa kwa ujumla. Zipo sababu nyingi lakini katika makala hii nitataja sababu chache, ni kwa nini rushwa ni hatari kwa taifa:

1. Rushwa hulifarakanisha Taifa na Mungu kwani Mungu anachukizwa sana na Rushwa.
Katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati 10:17 tunasoma, “Kwa maana Bwana, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu wa miungu, na Bwana wa mabwana, Mungu mkuu, mwenye kuogofya, asiyependelea nyuso za watu, wala hakubali RUSHWA.” Kama Yeye mwenyewe hakubali, basi hawezi kukubaliana nayo. Watu wanapotoa na kupokea rushwa moja kwa moja wanakuwa kinyume cha Mungu asiyependa upendeleo. Maagizo ya Mungu kwa viongozi wote ni:
-        Kuhukumu kwa haki
-        Kuwa na usawa
-        Kutenda mema kwa watu wote


  •  Kusimamia watu kulingana na utaratibu uliowekwa na kukubalika mbele za Mungu.
  •   Kusimama kwa niaba ya Mungu kutoa maagizo yanayostahili kwa watu
  •     Kuyashika maagizo na sheria za Mungu, huku wakijua Mungu ndiye aliyewapa mamlaka.
  •   Anapotokea viongozi wakaenda kinyume na haya yote, wanakuwa wanajisababishia hatia mbele za Mungu. Na kwa sababu Mungu anachukizwa nao, mambo mabaya hayapungui kwao. Magonjwa, majaribu, shida, misiba, na majanga mengi yanaambatana nao. Taifa lenye viongozi kama hawa liko kwenye hatari kubwa kwani kuna uwezekano mkubwa mambo mengi yakaharibika kwa sababu viongozi wamejikita katika kutatua shida zao.
Kwa kinywa cha nabii Isaya Mungu anazungumza juu ya wakuu wa watu wake, Isaya 1:23 anasema, “Wakuu wako ni waasi, na rafiki za wevi; kila mtu hupenda rushwa, hufuata malipo; hawampatii yatima haki yake, wala maneno ya mjane hayawawasilii.” Mungu hapendezwi kabisa na hali hii.
     2. Rushwa hupofusha macho ya viongozi
Ili taifa liweze kuendelea katika eneo lolote ni lazima pawe na viongozi wanaoweza kuona ili kuwapa watu maelekezo ya kuwasaidia; na kufungua fursa kwa wenye uwezo kuzitumia. Viongozi wanapaswa kuziona fursa na changamoto zinazoweza kujitokeza huko tuendako. Mataifa mengi ya kiafrika yanataabika kwa sababu ya mambo ambayo hayakutazamwa ipasavyo na viongozi waliotangulia. Wengi walipopata nafasi walijitazama wenyewe, hawakuwa na wa kuangalia mbele kitakachotokea.

Viwanda vingi vilivyoachwa na wakoloni vilifungwa baada ya miaka michache kwa sababu walioachiwa hawakuweza kuona changamoto ambazo zingejitokeza, hivyo wakakwama baada ya muda mfupi. Na wengine wa sababu ya kujipenda wenyewe wakajilimbikizia vitu na kuua shughuli zote za kuufaidisha uma.

Katika kitabu cha kutoka Mungu anaongea na uongozi wa Israeli kusema, “Nawe usipokee rushwa; kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hao waonao, na kuyapotoa maneno ya wenye haki.” Kutoka 23:8. Hapa Mungu anatoa madhara makubwa mawili ya rushwa, yaani kupofusha macho ya waonao na kupotoa maneno ya wenye haki. Maneno ya wenye haki ndiyo huliinua taifa, kama wenye haki wakinyamaza taifa litakuwa kwenye hali ngumu.

Katika Kumbukumbu la Torati 16:19 Mungu anaagiza tena kwa kiongozi, “Usipotoe maamuzi; wala usipendelee uso wa mtu; WALA USITWAE RUSHWA; kwa kuwa rushwa hupofusha macho ya wenye akili, na kugeuza daawa ya wenye haki”.

Kwa hiyo, taifa lenye viongozi wala rushwa ni taifa lenye viongozi wasioona (vipofu) na kama viongozi ni vipofu basin a watu wao wanakuwa vipofu. Hii ni hatari sana kwa taifa, taifa lolote linahitaji viongozi wenye maono katika Nyanja mbalimbali ili liweze kuinuka.

     3. Rushwa husababisha laana
Vilio na manung’uniko ya waliyoonewa na kunyimwa haki zao sio Baraka kwa taifa. Viongozi wanapowaacha watu wakateseka na kuumia bila kuwajali huku uwezekano wa kuwasaidia ukiwepo ni laana. Laana hii huwakalia viongozi na uzao wake na taifa lote kwa ujumla. Baadhi ya viongozi wamewafanyia watu ukatili mgumu sana bila kujua, wakati mwingine kiongozi anaweza kuwaza kwamba ni akili kuwadhulumu watu na kutumia nafasi yake kuwakandamiza watu wa hali ya chini; kimsingi hii ni laana.

Mpango wa Mungu ni kwamba wale waliofanikiwa na wenye mamlaka wawasaidie watu wanyonge. Na huu ndio mfumo wa kiroho unaokubalika mbele za Mungu. Taifa linalowajali wanyonge halikosi kubarikiwa. Katika Yeremia 23:1 Mungu anatoa Ole kwa wachungaji ambao kwa tafsiri nyingine tunaweza kusema “kwa viongozi” , anasema “Ole wao wachungaji, wanaoharibu kondoo za malisho yangu na kuwatawanya! Asema Bwana. Kondoo hapa ni watu wanaoongozwa. Kwa hiyo, tunaweza kusema, “Ole wao viongozi wanaoharibu watu (kwa kupotosha hukumu) na kuwatawanya (kwa kuwakosesha amani).

Isaya 10:1 “Ole wao wawekao amri zisizo za haki, na waandishi waandikao maneno ya ushupavu” Hili nalo linawahusu viongozi kwa maana wao ndio waliopewa dhamana ya kuweka sheria. Kumbe ni lazima waweke sheria au amri za haki na wanaohusika na kuandika waandike vizuri kwa kuzingatia utaratibu aliouweka Mungu.

Neno ‘ole’, sio neno la Baraka. Ni neno linaloonyesha kutakuwa na madhara baada ya muda. Kwa hiyo ni lazima viongozi wajiepushe na rushwa ili kuliepusha taifa na laa (mabaya). Taifa lenye viongozi waliolaaniwa ni taifa ambalo halina mwelekeo mzuri, viongozi waliobarikiwa huinua taifa.

    4. Rushwa hupanda uchungu ndani ya watu, na kuwafanya watu kuchukia taifa lao wenyewe
Uchungu ni kitu kibaya sana kwa watu, uchungu huleta mateso, huchoche malumbano na migomo. Watu wenye uchungu ni rahisi kwenda kinyume na uongozi, na kuleta maafa makubwa.  Taifa lenye watu waliojaa uchungu liko kwenye hatari kubwa sana, kwani watu wengi wanakuwa hawako tayaya

Mungu anataka watu ambao watapenda watu wake wafanikiwe, kwenye Zaburi 15:5 anasema, “Hakutoa fedha yake apate kula riba, Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia. Mtu atendaye mambo hayo Hataondoshwa milele.” Hapa tunaona mtu ambaye anawekeza kwa haki, asiyetoa rushwa anakuwa na maisha marefu.

      5. Rushwa kufunga fursa za maendeleo
Taifa lolote lenye watu wanaopenda rushwa, haliwezi kuwa na fursa za kutosha kwa ajili ya watu wake. Sababu kubwa ni kwamba fursa huwa zinaambatana, kwa hiyo kama mtu amefunga fursa moja kwa sababu ya faida binafsi basi anakuwa amefunga fursa nyingine nyingi. Mfano mtu aliyepewa dhamana ya kusimamia shule au kiwanda kisha akakubali kutumia hiyo nafasi vibaya kwa kujiangalia binafsi, akapindua mambo na mwisho kiwanda kikafa. Mtu huyu atakuwa amezuia biashara zilizokuwa zinafanyika kupitia hicho kiwanda, amepunguza uzalishaji, amewafanya watu wakose ajira na kadhalika.

Ili fursa za maendeleo zifunguke ni lazima fursa zilizopo zitumiwe vizuri. Rasilimali watu, fedha pamoja na maliasili ni lazima zitumiwe kwa uaminifu kwa kuzingatia mipango ya maendeleo iliyowekwa vinginevyo baada ya muda kilio cha kukosekana kwa fursa kitaendelea kuwa kikubwa zaidi. Vijana wanapoinuka wakakutana na watu waliojeruhiwa, viwanda vilivyokufa, maduka yaliyofungwa, maliasili zilizotumiwa bila utartibu wanabaki kwenye wakati mgumu.

Siri iliyowafanya walioendelea wakaendelea ni kule kuwa makini na kila fursa iliyojitokeza, baada ya kuzitumia vema hizo fursa ikafika mahali kila siku fursa mpaya zinafunguka, vijana wakizaliwa wanakuta mazingira mazuri yanayowasaidia kuziona fursa mbalimbali. Serikali inahusika moja kwa moja katika kuhakikisha watu wanazitumia vema fursa zinazofunguka.

    6. Rushwa huleta mafarakano na visasi kati ya watu
Watu walioonewa na kunyimwa haki zao, hawawezi kuwa na mahusiano mazuri na wale waliosababisha wao wakapoteza haki zao. Kinachotokea ni roho ya kisasi kujengeka, na kwa sababu ile shida inaingia mpaka kwa watoto basi unakuta jamii nzima inakuwa na hali ya visasi. Wengine watatumia nguvu za uharibifu walizonazo, wengine migomo, wengine nguvu za giza na wengine kutafuta nafasi za uongozi ili kupata fursa ya kulipiza kisasi.

Kuna kauli nimeisikia ikisemwa sana na watu wa hali ya chini kwa watoto wao wanapowasisitiza juu ya swala la shule, utasikia wakisema, “Soma kwa bidii angalau ukifika huko na sisi tutaonekana kuwa watu, siku hizi kama huna mtu huwezi kufika popote”. Bila shaka  hii ni kauli ya mtu anayejiona katika hali ya kutengwa kutokana na umaskini wake. Rushwa ni mbaya sana mioyo ya watu wengi katika nchi zinazoendelea imeharibiwa na rushwa.


7. Rushwa huzuia marafiki na kuongeza maadui.
Taifa lililojaa rushwa haliwezi kuwa na marafiki wengi, kwani baada watu waliokuwa marafiki kugundua kwamba misaada waliyokuwa wanatoa iliwafaidisha wachache na haikuwafikia walengwa wanajeruhika na kuvunja mahusiano. Hili ni dhahiri kabisa mataifa mengi yaliyokuwa yanatoa misaada kwa nchi zinazoendelea yamevunjika moyo kwa sababu wakifuatilia wanakuta shida walitaka kutatua zko palepale.

Yaani barabara walizofadhili zimevunjika, majengo waliyojenga, watu waliiba hela wakajenga chini ya kiwango, masikini waliotumika kutafutia misaada bado hali zao ziko vilevile. Na mengine yanayovunja moyo hata kuliko haya. Mataifa mengi yaliyoendelea wanapenda sana ushirikiano na viongozi waaminifu na wenye uchungu na maisha ya watu.

8. Rushwa hupotosha hukumu na kuvunja utaratibu wa uongozi katika taifa (katiba).
Taifa lenye watu wanaotoa na kupokea rushwa, linakuwa na watu wengi ambao mioyo yao imeathirika na hawawezi tena kutoa hukumu inavyopasa. Wamesoma lakini wanakuwa hawana akili, unakuta kesi ambazo wanaweza kuamua hata watu wa kawaida kwa ufasaha zinawashinda waliosomea. Roho Rushwa inaharibu utaratibu wa uongozi katika taifa.

Kiujumla, Viongozi wanakosa uwezo wa kukaa kwenye nafasi zao, kuna wakati wanapaswa wasema ila wanakaa kimya; kuna wakati wanapaswa wakatae ila wanakubali tu; kuna wakati wanafanya yasiyowapasa. Hili liko dhahiri, kuna mahali ukipita unaweza kusema hivi hapa palikuwa na kiongozi? Swali hili hujitokeza kwa sababu kiongozi hutambulika kwa utendaji wake. Kwa kifupi, Kiongozi aliyekuwepo alikuwa ameuza nafasi yake ya uongozi, akabaki kama pambo tu.

Kwa sababu ya rushwa wakuu wanakosa ujasiri wa kuwakemea wa chini yao, kwanini? Kwa sababu kuna siri wamefichiana. Anaogopa kukemea ili mambo yake yasiwekwe wazi. Kwa hiyo, kwa jinsi hii mfumo mzima wa uongozi unakuwa umevurugika, watu wachache wenye madaraka wanakuwa ndio waamuzi wa kila kitu. Katima inabaki kuwa pambo tu. Taifa lililojaa rushwa ni gumu sana, linakuwa na sheria zisizofuatwa, wanapanga bajeti isiyosimamiwa, wanaweka mipango ambayo haitekelezwi ipasavyo.


9. Husababisha kuinuka kwa viongozi wasio na sifa.
Taifa linaweza kuwa na watu wengi sana wasio na sifa, walioingia kwenye nafasi kwa kuteuliwa au kwa kuchaguliwa kutoana na rushwa. Mwanya huu unapojitokeza unakuwa ndio mlango wa rushwa zaidi na zaidi. Kwa nini? Sababu kubwa ni kwamba watu wasio na uwezo wa kufanya mambo watafuta namna ya kuwafunga vinywa wafuatiliaji, na njia rahisi ni kutoa rushwa/hongo. Kwa jinsi hii taifa linadorora kiuchumi.

Rushwa huwafanya watu wafanye maamuzi yasiyofaa wakati wa uchaguzi, rushwa huwafanya wenye uwezo kukata tamaa hasa walio katika mazingira magumu/walio chini kiuchumi. Taifa linakosa watu wabunifu; wanabaki walewale waliozaliwa katika kambi ya wala rushwa ambao rushwa imeanza kuingia kwenye damu zao tangu mimba ilipotungwa.

Mataifa mengi ya ki-Afrika yamekuwa kwenye wakati mgumu kwa sababu ya baadhi ya viongozi waliopenya nakuingia kwenye nafasi zao kwa njia isiyo halali. Ninaposema viongozi simaanishi maraisi tu namaanisha kila mtu mwenye nafasi kwenye eneo Fulani, iwe ni serikalini au sekta binafsi.


10. Hupindua kweli, hivyo kulipindua taifa na kuliletea aibu.
Katika Mithali 29:4 tunasoma jambo la ajabu sana. Neno linasema “Mfalme (kiongozi) huithibitisha nchi kwa hukumu; Bali yeye apokeaye rushwa huipindua.” Kumbe mapinduzi hayafanywi na wanasiasa tu, hata wala rushwa nao wana uwezo wa kuipindua nchi. Wanaipinduaje? Nafikiri ni kwa njia ya kufanya mambo yaende ndivyo sivyo:


  •   Kutoka kwenye kuwa nchi ya amani na kuwa nchi ya vita na migogoro
  •    Kutoka kwenye kuwa nchi ya kupendana kwenda kwenye nchi ya chuki na visasi
  •     Kutoka kwenye nchi inayoendelea kuwa nchi anayodaiwa
  •   Kutoka kwenye nchi inayojitegemea kwenda kwenye nchi tegemezi na mapinduzi mengine
  •         Kutoka kwenye nchi inayoheshimiwa kwenda kwenye nchi inayodharauliwa
Kumbuka dhambi ni aibu ya taifa. Katika Mithali 14:34 tunasoma, “Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote.” Kwenye mstari huu tunapata pande mbili za taifa:

-        Upande wa Haki, pale ambapo watu wanafanyiwa mambo kwa haki, hakuna anayemwonea mwingine, rasilimali zinatumika kwa usawa na watu wapewa wanayostahili. Hapa tunaambiwa taifa huinuka (Mafanikio hutokea)
-        Upande wa pili tunakuta dhambi (ikiwepo dhambi ya rushwa ambayo ni dhambi ya karibu sana kwa viongozi na wenye mamlaka). Hapa tunaambi ni aibu ya taifa. Mataifa mengi ya Afrika yanasemwa vibaya kwa sababu ya Rushwa.

        11. Viongozi wanakosa nguvu ya ushawishi kwa watu wao.
Mara nyingi maswala ya rushwa au ufisadi hufanyika kwa siri, ila inapotokea hiyo roho ikaendelea kudumu kwa muda mrefu, uovu wote uliofanyika kwa siri hufichuka na mambo yote huwa wazi kwa watu. Hapo ndipo tafsiri na sura ya viongozi hubadilika kabisa ndani ya watu. Watu huanza kuwaona viongozi kama wabinafsi na watu wasio na uwezo wa kujizuia. Hapo inakuwa kila watalolisema linahusishwa moja kwa moja na tabia yao ya kupenda rushwa/ufisadi.

Viongozi waaminifu wanakuwa wanapendwa sana na watu, wanaweza kuwaambia watu mambo na wakawaelewa. Watu wanawaona ni watu wenye uwezo mkubwa wa kuweza kutatua matatizo yao, sio kuongeza matatizo. Viongo kama Mwalimu Julius K. Nyerere raisi wa Kwanza wa Jamhuru ya Muungano wa Tanzania walikuwa na ushawishi mkubwa kwa sababu ya kuchukia rushwa.

Taifa lenye viongozi mafisadi/wala rushwa linakuwa na viongozi wasioweza kusikilizwa na watu wao. Wanaweza kuitisha mikutano watu wasihudhurie. Ila kama viongozi ni wema, waaminifu, waadilifu na wanaofanya mambo kwa haki, wanaoongozwa wanakuwa na upendo wa dhati kabisa kwao. Na hivi ndivyo Mungu ameweka, kwamba wenye mamlaka wapewe heshima.

Waebrania 13:17 inasema, “Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi.” Heshima hii ni kwa watu wale wanaotoa muda wao kwa ajili ya watu wanaowaongoza. Kwa hiyo kama kiongozi ni fisadi hawezi kuheshimiwa na watu wake, nguvu yake ya ushawishi inapungua na hapo taifa liko hatarini.

12. Rushwa huuharibu ufahamu
Katika kitabu cha Mhubiri 7:7 tunasoma, “Kweli jeuri humpumbaza mwenye hekima, Na rushwa huuharibu ufahamu.” Hapa neno hili linazungumza moja kwa moja kwamba rushwa huuharibu ufahamu. Ni kweli kabisa, kuna wakati ukifuatilia baadhi ya maamuzi yaliyofanywa na viongozi wala rushwa (Corrupt leaders) unaweza kushangaa sana. Baadhi ya maamuzi wanafanya bila ufahamu kabisa.

Ufahamu ulioharibika ni ule ambao haufanyi kazi ipasavyo, ni kama mtu anajua ila hajui. Ufahamu ulioharibika kwa tafsiri nyingine ni upumbavu. Akili zinakuwa zimepumbazwa kwa rushwa, ufahamu umepoteza mwelekeo. Utakuta kiongozi anajua kabisa ujenzi wa miundimbinu Fulani ni kwa ajili ya faida ya sasa nay a baadaye, lakini atathubutu kutumia fedha za miundombinu kwaajili ya mambo yake binafsi. Hii ni kwa sababu ya ufahamu ulioharibika.

Hitimisho
Naamini kupitia makala hii utakuwa umepata kitu cha kukusaidia katika lile unaloweza kufanya katika kupiga vita rushwa katika bara letu la Africa. Ili nchi zetu za kiafrika zipige hatua kiuchumi, kisiasa na kijamii ni lazima iwe na watu wanaoichukia rushwa ili kuepukana na madhara yote yaliyotajwa hapo juu. Najua kwa msingi huu wa maneno kutoka kwenye Biblia Takatifu ambacho ni kitabu kinachotumiwa na wengi duniani kote, kuna mambo ambayo yamekuwa wazi kuliko ilivyokuwa mwanzo.

Ikiwa wewe ni kiongozi uliyeteuliwa au kuchaguliwa, au unasimamia kampuni binafsi au vyovyote ulivyo, nina hakika kila mtu ni kiongozi katika eneo lake; au wewe na raia mwema wa taifa Fulani, nakusii usimame katika nafasi yako kuhakikisha mbegu ya rushwa haiendelei kumea na kuifunika nchi yako.

Kila mtu ana nafasi katika kutokomeza adui huyu anayejulikana kwa majina mengi. Wengine humwita Corruption/bribe, wengine rushwa, wengine hongo, wengine takrima, wengine kitu kidogo na mengine mengi. Kimsingi hawa wote ni watoto wa baba mmoja na kazi yao na kuleta umaskini wa wengi huku wachache wakinufaika.

Mungu ibariki Tanzania! Mungu ibariki Afrika!

Na Mwl. S.S.Michael
Simu: 0713511544 (Whatsapp)




Thursday, 17 November 2016

JE, KUNA TOFAUTI GANI KATI YA ‘CASFETA’ NA ‘CASFETA (TAYOMI)’?


Bwana Yesu Asifiwe!
Napenda kukualika katika kulitazama swali hili ambalo najua baadhi ya watu hawapendi kabisa kulisikia kwa sababu linahusu swala ambalo liliwajeruhi sana watumishi wa Mungu. Nimelileta swali hili kwa sababu ya changamoto kubwa niliyoiona na ninayoendelea kuiona kwa kizazi hiki. Katika kipindi hiki ambapo elimu imepewa kipaumbele sana, watoto wetu wanatumia muda mwingi sana mashuleni. Hivyo, kama hapatakuwa na usimamizi wa kueleweka tutawaweka katika wakati mgumu sana.

Kwanza, napenda kumshukuru sana Mungu kwa kuwepo kwa makundi haya ambayo yamefayika msaada mkubwa sana kwa maisha ya watu wengi waliopata nafasi ya kupita katika mfumo wa elimu hapa nchini kwetu. Wapo wengi walioanza maisha ya wokovu kutokana na utendaji wa makundi haya (nikiwepo mimi mwenyewe) na wengine wengi wameweza kusimama katika huduma zao na wokovu kwa ujumla kwa sababu ya kulelewa katika makundi haya.

Pili, nieleze sasa lililomo moyoni mwangu, wapendwa, “Ni muda mrefu sana nimekuwa nikishuhudia changamoto wanazokutana nazo wanafunzi wa Kipentekoste mashuleni hasa wa vikundi hivi viwili vyenye jina moja la ‘CASFETA’. Sijui kama wewe msomaji wangu kama ulishashuhudia changamoto yoyote katika makundi haya?

Naamini kama hujashuhudia inawezekana umesikia kwa mwanao au viongozi wa makanisa au hata kwa watu maeneo mbalimbali.”  Kuna maeneo mengine wanafunzi hawapatani na baadhi ya wachungaji, wengine wanagombana wao kwa wao, yaani ni vurugu tupu. Kila mmoja anateta jina la kikundi chake. Wakati natafakari hili nikakumbuka Paulo alivyosema,

“…kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu? Maana hapo mtu mmoja asemapo, Mimi ni wa Paulo; na mwingine, Mimi ni wa Apolo, je! Ninyi si wanadamu? Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye.”

Bado nikawa ninawaza, kuna nini kinachowafanya hawa watoto wetu wasipatane na wakamtumikia Mungu kwa pamoja kwa amani. Nimepata baadhi ya mambo ya kihistoria lakini bado ninaamini huu ni wakati wetu wa kulitazama jambo hili kwa upya. Kizazi kijacho kinatuhitaji sana ili kiweze kusimamia yote yaliyowekwa mbele yake kuyafanya.

Baada ya  kulitazama swala hili kwa kina, ndipo nikabaki na swali kubwa moyoni mwangu juu ya utofauti uliopo kati ya makundi haya mawili yenye jina moja. Kwa nini swali hili likanijia na kunisumbua? Nitakueleza mambo kadhaa niliyoyatafakari ili nawe uyatafakari, niayangu sio kukosoa vikundi hivi ila ni kukutazamisha hali ambayo inaweza kuwakosesha wengi mbingu kama hatutaishughulikia mapema. 

JINA LA MAKUNDI HAYA
Kinachonishangaza hapa ni kwamba makundi haya yanayojihesabu kuwa makundi mawili yenye lengo la kuwalea wanafunzi wa Kipentekoste wawapo masomoni yanaitwa kwa jina moja yaani CASFETA (Christ’s Ambassadors Students’ Fellowship of Tanzania). Sasa inakuwaje makundi tofauti yakaitwa kwa jina moja? Najua majibu yapo kutokana na historia ya makundi haya, ila nakuuliza ili uweze kutafakari kwa upana zaidi. Je, ilikuwaje jina moja likasimamia maono ya aina mbili tofauti?


       2.  MAONO NA UTENDAJIKAZI
Katika uzoefu wangu wa miaka zaidi ya 10 masomoni yakiwepo yale ya Kidato cha kwanza hadi cha nne (O-Level), ya kidato cha tano na sita (A-Level) pamoja nay ale ya Chuo kikuu miaka mitatu (UDSM) nimekuwa nikijifunza sana mambo mengi katika makundi yote mawili. Mwisho nikagundua kwamba haya makundi yana maono yanayofanana na yanafanya kazi katika msingi mmoja huku wakitumia mbinu zinazofanana katika usiamamizi na uendeshaji wa ibada.

       3. WASHIRIKI WA KILA KUNDI
Kila kundi linadai kwamba linafanya kazi na wanafunzi wa makanisa yote ya Kipentekoste yaani EAGT, TAG, FPCT, KLPT, PENTEKOSTE PEFA, PENTEKOSTE HOLINESS NA MENGINE MENGI, kwa kifupi ni yale makanisa ambayo yapo kwenye umoja wa makanisa ya Kipentekoste (PCT). Kwa hiyo mshiriki ni lazima awe amebatizwa kwa maji tele, na awe anaabudu katika moja ya makanisa ya Kipentekoste. Kwa hiyo katika makundi yote mawili utakuta mchanganyiko wa wanafunzi wa madhehebu mbalimbali ya Kipentekoste.

         4. MSIMAMO WA KIIMANI
Kama nilivyosema kwenye swala la washiriki kwamba wote ni wa Imani ya Kipentekoste, yaani wanasimamia misingi ya Kipentekoste wakisistiza hasa ile yenye utata kwa baadhi ya watu mfano Ujazo wa Roho Mtakatifu na kunena kwa lugha mpya, Ubatizo wa maji tele na ule wa kuukiri wokovu wazi wazi. Viongozi na washiriki wote katika makundi haya ni lazima asimamie misingi hii kuhakikisha inakuwa hai kwenye maisha yao ya kila siku yaani, wajazwe nguvu za Roho Mtakatifu, wanene kwa lugha mpya na ni lazima wawe wamebatizwa kwa maji tele kama maandiko yasemavyo.

      5.  MISISTIZO YA MSINGI (Mambo ya muhimu)
Makundi yote mawili yameweka msisitizo mkubwa kwenye swala Utakatifu, Neno la Mungu, Maombi, Utumishi wa mtu mmoja mmoja na wa kikundi kama viungo katika mwili wa Kristo, Mafanikio ya kimasomo kama sehemu ya kumtangaza Kristo, Malezi ya kiroho makanisani (Kila mshiriki ni lazima awe na kanisa linalomlea kiroho), Utoaji wa kibiblia (Hasa Fungu la 10) na mengine.

Baada ya kuyaangalia mambo haya pamoja na mimi japo kwa ufupi naamini na wewe umeanza kujiuliza swali nilililojiuliza, “Kwani kuna tofauti gani?” Je, unayo majibu ya Swali hili? Kama unazo hebu zipime na kuziangalia tena mara mbili mara tatu.

Hebu nikushirikishe changamoto chache nilizoziona kwa kuwepo kwa makundi haya mawili yenye jina moja.
                 i.          Migogoro kati ya viongozi
Nimeshuhudia migogoro ya maneno na ile ya kimya kimya kati ya viongozi wengi wa makundi haya, hasa kwa yale yanayofanya kazi kwenye taasisi moja (Shule au Chuo). Migogoro hii imekuwa ikiibuka hasa kwenye maeneo mbalimbali likiwemo eneo la washiriki ambapo baadhi ya viongozi wamekuwa wakinyang’anyana washiriki na wengine kujitahidi kuwajengea washiriki wake maneno mabaya kuhusu kundi la pili ili wahame (kuwalinda). Kila kundi linajitahidi kuonyesha utofauti wake ambao kiuhalisia hauonekani au hauna nguvu kubwa.
               ii.          Kutangatanga kwa vijana waliookoka mashuleni na vyuoni
Kwa sababu wengi huwa hawaoni tofauti kati ya makundi haya mawili, wengi huwa na uhuru wa kwenda kundi lolote kati ya haya mawili. Mwingine utakuta ameshiriki kwenye makundi haya kwa nyakati tofautitofauti kutokana na anavyoona mwenyewe.
              iii.          Mwonekano kwa wasiomjua Mungu na waongofu wapya
Wengi huwa katika maswali mengi wakijiuliza juu ya tofauti iliyopo kati ya makundi haya, wakati mwingine viongozi wa makundi hutumia muda mwingi kuwaelimisha juu ya utofauti huo ili kuweza kuwajengea msimamo badala ya kuwalea katika misingi ya kibiblia.
              iv.          Walezi na wadau mbalimbali wa Injili kwa wanafunzi na vijana
Changamoto hii hutokea pale ambapo utakuta mtumishi wa Mungu amepata maono ya kuwafikia wanafunzi wa kipentekoste kwa umoja wao. Hapa ni lazima aulizwe unawatafuta wa CASFETA ipi? Na hili huleta ugumu pia katika kuwaunganisha na kuwaleta pamoja.
               v.          Changamoto kwenye uanzishwaji wa matawi mashuleni
Tumeshuhudia migongano mingi kwenye hili eneo, ambapo utakuta CASFETA iliyotangulia inajitahidi kuipiga vita inayoingia ili isiwavuruge washiriki wake. Japo kwenye baadhi ya maeneo kuna makubaliano yanayofanyika bado hakupo kutazamana vizuri kwa makundi haya.
Katika kutafakari nikasema, “Sasa ni nini sababu ya utofauti huu? Au ni nini Tatizo?
Baadhi ya watu wakasema “tatizo ni waanzilishi wake”, nami nikasema “kwani hawa waanzilishi sio Wapentekoste? Hawajatoka kwenye makanisa haya ya kipentekoste?” nikagundua kwamba wote ni wapentekoste wazuri.

      Wengine wakasema “labda ni Madhehebu wanayotoka hao washiriki”, hapa napo nikajiuliza “kwani makundi haya hayana watu kutoka madhehebu mbali mbali?” (Nikagundua wala hakuna ubaguzi wa kidhehebu kwenye makundi haya)

Wengine wakasema tofauti inatokana na walezi wa makundi haya: yaani CASFETA inalelewa na Kanisa la TAG (Tanzania Assemblies of God) na CASFETA (TAYOMI) inalelewa na Tanzania Youth Ministries (TAYOMI). Kwa upande wangu nikajiuliza kuna tofauti gani ya malezi kati ya walezi hawa? Je, Wanafunzi hawa si wa makanisa yote ya Kipentekoste? Japo baadhi ya makanisa nayo yameshaanzisha vyombo vyao. Je, hii roho ya kuwabagua watoto huku tukiwaita jina moja ilitoka wapi? Je, wokovu wetu si mmoja (imani moja, ubatizo mmoja, Roho mmoja) au kuna nini kimefichika?

     Wengine wakasema ni matunda ya ule mgogoro uliokuwepo kati TAG na EAGT kwenye miaka ya 1980 na 90, bado hapa nikajiuliza kwa hiyo ile roho ya matengano hakufa bado? Ni kweli kwamba ndiyo inayoendelea kukitafuna hata kizazi hiki ambacho hakina hatia (Hakikuwepo wakati wa mgogoro)? Bado sikuweza kukubaliana nao asilimia mia moja.

    Hebu sasa nikuulize na wewe mpendwa, ikiwa ni mchungaji, Askofu, mwimbaji, kiongozi wa CASFETA mstaafu, Mwana-CASFETA, mshirika wa kanisa la Kipentekoste na mdau mwingine yeyote unayejishughulisha na malezi ya wanafunzi mashuleni. Je, Kuna tofauti gani kati ya CASFETA na CASFETA (TAYOMI)? 

Mimi ninawalilia watoto wanaopigana vita isiyowahusu. Au niseme, "baba za watu wamekula zabibu kali, na meno ya watoto wao yametiwa ganzi." Matengano haya yanawatesa watoto wetu. Chuki ya CASFETA na CASFETA (TAYOMI) haina Mungu ndani yake. Sumu hii ni lazima itafutiwe dawa, ili kuokoa maisha ya vijana mashuleni. Wachungaji wengi wanawapiga vita wanafunzi kwa sababu ya chuki kati ya makundi haya mawili. Kanisa la Kristo Yesu liko wapi katika mashindano na malumbano. 

Hakunatofauti kati ya CASFETA na CASFETA (TAYOMI), ni lazima watoto wetu wajue Kristo hajagawanyika. Wote ni wa Kristo, Kristo ni mmoja. Tutumike katika upendo, na wazazi wa kiroho (Maaskofu na Wachungaji) msaidie kusimamia jambo hili. Huduma nyingi zinazimwa kwa sababu ya mitazamo hasi iliyojengeka katika makundi haya.

"Eee Mungu likumbuke kanisa la Tanzania, Wakumbuke wanafunzi wetu mashuleni, na wasaidie viongozi wetu walione kusudi lako kwa watoto na vijana walio mashuleni."

Na Mwl. S.S.Michael
Simu: 0713511544 (Whatsapp)
AGM - International.


Wednesday, 16 November 2016

USISHINDANE NA MUNGU

YA NINI KUSHINDANA NA MUNGU?
Isaya 45:9 “Ole wake ashindanaye na Muumba wake! Kigae kimoja katika vigae vya dunia! Je! Udongo umwambie yeye aufinyangaye; Unafanya nini? Au kazi yako, Hana mikono?”
Kabla ya kumwangalia mwanadamu labda nikukumbushe kwamba Shetani (Lucifer) ndiye aliyekuwa wa kwanza kuinua kiburi na kushindana na  Mungu. Kumbuka alikuwa Isaya 14:13 Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini.” Hiki ni kiburi cha hali ya juu sana, ndiyo maana Mungu akakasirika akamtupa chini kuzimu na kumhukumu milele. 
Shetani yeye kwa sababu alikuwa Kerubi wa sifa kwa Mungu, tunaweza kusema hizo sifa ndizo zlizompa kiburi hata akashindana na Mungu. Je, wewe mwanadamu wa leo ni nini kinakupa kiburi? Je, ni mali! Kumbuka nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Mungu. Je, ni uwezo ulionao kitaaluma? Kumbuka Mungu ndiye aliyekuumba na kukupa huo uwezo. Je, ni sura (urembo)! Kumbuka sisi sote ni mavumbi.
Ukisoma biblia utagundua kwamba mwanadamu amekuwa katika hali ya kutaka kushindana na Mungu hasa kwa sababu Mungu haonekani kwa macho ya damu na nyama. Tangu Adamu na Eva walipofanya uasi katika bustani ya Edeni, hali ya uasi iliendelea kukaa katika moyo wa mwanadamu hata kufikia mahali pa kupata kiburi na kutaka kushindana na Mungu.
Katika Mwanzo 6:3, Bwana (Mungu) akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini.
Ukisoma kuanzia mstari wa kwanza utaona kwamba wanadamu waliongezeka sana, na wakazidi kufanya maasi mengi hata kuvuruga kabisa ile mipaka ambayo Mungu amewawekea. Mstari wa 5 unasema “Bwana akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote.”
Mashindano haya hayakuisha, yamekuwa yakiendelea hata katika kizazi hiki.
Tunashindana na Mungu kwa njia gani?
  1. Kuukosoa uumbaji wake.
Kusudi la Mungu ni kila kitu kiende kwa utaratibu aliouweka kulingana na kusudi lake. Ila katika kizazi cha leo kuna watu ambao wamekuwa wagumu wa kuelewa na wamekuwa wakipindua mambo. Mtume Paulo akisema na warumi aliwazungumzia watu wa jinsi hii.
Warumi 1:26 – 27 “Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili; wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao.” Unaona mapinduzi haya? Huku ni kushindana na Mungu.
Hapa anazungumzia maswala ya “Ushoga”  ndoa za jinsia moja na kufanya mapenzi kinyume na maumbile. Huku ni kwenda kinyume na utaratibu wa Mungu na kwa lugha rahisi ni kushindana na Mungu. Matokeo yake ni magumu sana. Hapo juu tuliposoma panatuweka wazi kwamba “Kuna kuachwa na Mungu” na hii ndiyo sababu ya ugumu wa maisha duniani.
2.  Kwa kupingana na neno  lake.
Wako watu wengi siku hizi wanaojaribu kulipindua neno la Mungu na kuleta mafundisho yao kulingana na matakwa yao. Hii ni kushindana na Mungu. Lile neno alilolisema Mungu ni AMINI na KWELI, sisi kazi yetu ni kutii tu. Tukimchukua Farao kama mfano tunaweza kuona ni jinsi gani Mungu anavyoweza kulisimamia neno lake. Mungu anamwambia “WAPE WATU WAANGU RUHUSA WAENDE WAKANITUMIKIE” (Kutoka 5:1, 8:1)
Ona majibu ya Farao Kutoka 5:2 “Farao akasema, Bwana ni nani, hata niisikilize sauti yake, na kuwapa Israeli ruhusa waende zao? Mimi simjui Bwana, wala sitawapa Israeli ruhusa waende zao.” Hiki ni kiburi cha hali ya juu sana, na ni hali ambayo inaweza kuonekana kwa watu wengi wenye madaraka au utajiri. Wako watu wenye mioyo kama Farao, hawako tayari kulitii neno la Mungu. Huku ni kushindana na Mungu!
3. Kwa kutenda dhambi (Uasi)
Katika 1Yohana 3:4 tunasoma, “Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi.” Kwa hiyo kutenda dhambi mbali na kumtenga mtu na Mungu, huinua pia roho ya mtu kuwa na kiburi na wakati mwingine hata kumsema Mungu vibaya.
Roho ya kuasi ni roho mbaya sana, katika mwanzo 6 tumeona maovu wa wanadamu yaliongezeka sana na Mungu akatangaza wazi kwamba Roho yake haitashindana na mwanadamu.
4. Kupigana au kuwapiga vita watumishi wake.
 Hili ni jambo ambalo watu katika nyakati za leo wameliona la kawaida tu. Kumbe sio jambo la kawaida, uscheze na mpakwa mafuta wa Mungu.
Mfalme Daudi alijua swala na Mashihi wa Bwana kabla hata ya kuwa Mfalme. 1 Samweli 26:9 “Lakini Daudi akamwambia Abishai, Usimwangamize; kwani ni nani awezaye kuunyosha mkono wake juu ya masihi”
Ukisoma tena, Zaburi 20:6 Daudi anaimba Zaburi na kusema “Sasa najua kuwa Bwana amwokoa masihi wake;Atamjibu kutoka mbingu zake takatifu.” Nakatika  Zaburi 28:8 anasema “Bwana ni nguvu za watu wake, Naye ni ngome ya wokovu kwa masihi wake.”
Tunachijifunza hasa kwenye mistari hii ya Zaburi ni kwamba, unaposhindana na masihi au mpakwa mafuta wa Bwana unashindana naye (Mungu) mwenyewe. Tunaliona pale Miriamu alipojaribu kumsema vibaya Musa mtumishi wa Mungu. (Hesabu 12) Mungu alimpa adhabu kali sana, hakutaka kusikia hata maombi ya Musa na Haruni. Miriamu alipata Ukoma na alifungwa  nje ya kambi kwa muda wa siku saba.
Tukumbuke pia wakati wa akina Daniel kule Babeli vile ambavyo Mungu alishughulika na watu walioshindana na watumishi wake. Kipindi cha Akina Petro Mungu alimshughulikia. Matendo 12:22 “Watu wakapiga kelele, wakisema, Ni sauti ya Mungu, si sauti ya mwanadamu. Mara malaika wa Bwana akampiga, kwa sababu hakumpa Mungu utukufu; akaliwa na chango, akatokwa na roho.”
Ni muhimu pia tukamkumbuka Paulo wakati anajulikana kama Sauli,aliyekuwa mkatili, akuia watu waliokuwa wanamtaja Yesu na kuamini. Ukiso Matendo 9 utaona taarifa za Sauli. Mstari wa kwanza tunasoma, “Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana”
Aliua wengi lakini mwisho akakutana na Mungu akamshikisha adabu, Mstari wa 8 na 9 tunasoma, “ Sauli akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski. Akawa siku tatu haoni; hali, wala hanywi.”
5. Kuabudu miungu (Kumfananisha Mungu na vitu au watu)
Katika Warumi 1: 21-23 “kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza.Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika; wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo.”
Kumbuka pia wakati Musa amekwenda mlimai akawaacha Wana wa Israeli Jangwani wakiongozwa na Haruni; kisha Haruni akawatengenezea Sanamu ya ndama ili waiabudu, Mungu alighadhibika sana akataka kuwaangamiza wote.
Kutoka 32, ukisoma huu mlango utaona madhara makubwa yaliyotokea kwa sababu ya jambo hili.
Waamuzi 2:12 Tunausoma wakati ambapo Israeli nao walimwacha Mungu wakaabudu sanamu, “Wakamwacha Bwana, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha Bwana, akaghadhibika. Napo matokeo yake hayakuwa mazuri, mambo yaliwaharibikia kabisa.
6.  Maneno ya Kiburi na kuingilia kazi za madhabahu.
Jinsi nyingine ya kushindana na Mungu ni kwa kuzungumza maneno ya kiburi, na kujiinua juu ya Mungu.  Maneno kama haya yalimgharimu Herode, alipoongea watu wakamsifu basi ikawa ndio mwisho wake.
Mfalme Uzia naye alifanya vizuri sana mbele za Mungu, kisha akawa na kiburi akaenda akaingilia kazi ya makuhani; kazi ya kuvukiza uvumba madhabahuni pa Bwana. Hata alipoelekezwa na makuhani hakutaka kusikia kabisa. Alijiona mwenye haki mahali ambapo Mungu hakumweka. Lililomtokea mwenyewe alishika adabu.
2Nyakati 26:19-21 “ ukamtokea ukoma katika paji la uso wake mbele ya makuhani nyumbani mwa Bwana karibu na madhabahu ya kufukizia na …. angalia, alikuwa na ukoma pajini mwa uso, wakamtoa humo upesi; hata na yeye mwenyewe akafanya haraka kutoka, kwa sababu Bwana amempiga. Uzia mfalme akawa na ukoma hata siku ya kufa kwake, akakaa katika nyumba ya pekee, kwa kuwa ni mwenye ukoma; maana alitengwa na nyumba ya Bwana”
          Katika dunia hii tuna watu wengi sana ambao wamejaa maneno ya kiburi, wengine ni kwa sababu ya nafasi zao za uongozi, wengine ni utajiri, wengine ni umaarufu, wengine ni sura na vile walivyo kwa nje. Watu hawa wanashindana na Mungu bila kujua nap engine kwa kujua. Ni muhimu tukajifunza kwa hawa waliojaribu kuongea maneno ya kiburi Mungu akashughulika nao.
Nirudie tena swali langu la Msingi “U nani wewe unayeshindana na Mungu?” Katika mstari wetu wa msingi tumesoma, “Ole wake ashindanaye na Muumba wake! Kigae kimoja katika vigae vya dunia! Je! Udongo umwambie yeye aufinyangaye; Unafanya nini? Au kazi yako, Hana mikono?”
Unapojaribu kushindana na Mungu kumbuka mambo haya:
  1.       Hakuna aliyewahi kushindana na Mungu akashinda
  2.     Sisi sote kwa jinsi ya mwili ni mavumbi,tuliumbwa kwa mavumbi na huko tutarudi (mwanzo 3:16)
  3.      Uko hivyo ulivyo kwa neema ya Mungu tu Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Mungu
  4.        Ukigusa utukufu wa Mungu huwezi kuendele kuishi
  5.     Tulikuja uchi na bila kitu na hatutaondoka na kitu. 1 Timotheo 6:7 “Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu”


JE, UNAISHI KULINGANA NA KUSUDI LA MUNGU JUU YA MAISHA YAKO?

TAFUTA KUTIMIZA KUSUDI LA MUNGU
KATIKA KILA UNALOLIFANYA.

Utangulizi:

Kila jambo litakalokujia wewe kama mtumishi wa Mungu jua kwamba lina muunganiko na kusudi unalolitumikia kwa wakati huo au unaloelekea kulitumikia. Jambo lolote liwe baya au jema, liwe gumu au jepesi, uwe unalijua au haulijui, liwe la kawaida au lisiwe la kawaida.

Nafasi au fursa zote anazofungua au alizofungua Mungu kwako , vita anavyoleta shetani, hali ya mwili wako binafsi-usumbufu, umbo, sura nk; hali ya kiuchumi, familia uliyotoka, maeneo uliyopita na yote uliyofanya katika maisha uliyoishi ni lazima yawe na matokeo ya namna moja au nyingine katika kusudi unalotumikia au utakalotumikia.
🔃🔃
Kila mahali Mungu anapokupeleka ni lazima pawe na kusudi lake, wakati mwingie kusudi lake ni kukuandaa kwaajili ya kusudi jingine. Kila unalofanya likikufanya utimize kusudi la Mungu  rahisi kuona mafanikio makubwa yakiandamana nawe kila wakati.

Muhubiri 3:1-8
Kwa kila jambo kuna majira yake, Na WAKATI kwa kila kusudi chini ya mbingu. WAKATI wa kuzaliwa, na WAKATI wa kufa; WAKATI wa kupanda, na WAKATI wa kung'oa yaliyopandwa; WAKATI wa kuua, na WAKATI wa kupoza; WAKATI wa kubomoa, na WAKATI wa kujenga; WAKATI wa kulia, na WAKATI wa kucheka; WAKATI wa kuomboleza, na WAKATI wa kucheza; WAKATI wa kutupa mawe, na WAKATI wa kukusanya mawe; WAKATI wa kukumbatia, na WAKATI wa kutokumbatia; WAKATI wa kutafuta, na WAKATI wa kupoteza; WAKATI wa kuweka, na WAKATI wa kutupa; WAKATI wa kurarua, na WAKATI wa kushona; WAKATI wa kunyamaza, na WAKATI wa kunena; WAKATI wa kupenda, na WAKATI wa kuchukia; WAKATI WA VITA, NA WAKATI WA AMANI.

MSINGI WA SOMO
1Tim. 4:8 -10
Kwa maana kujizoeza kupata nguvu za mwili kwafaa kidogo, lakini utauwa hufaa kwa mambo yote; yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye. Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa; kwa maana twajitaabisha na kujitahidi KWA KUSUDI HILI, kwa sababu tunamtumaini Mungu aliye hai, aliye Mwokozi wa watu wote, hasa wa waaminio.
Wafilipi 2:13
Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.
Yeremia 29:11-14
Maana nayajua MAWAZO NINAYOWAWAZIA ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.NANYI MTANIITA, mtakwenda na KUNIOMBA, nami NITAWASIKILIZA. NANYI MTANITAFUTA na KUNIONA, mtakaponitafuta KWA MOYO wenu wote. NAMI NITAONEKANA KWENU, asema Bwana, NAMI NITAWARUDISHA watu wenu waliofungwa, nami nitawakusanya ninyi, nikiwatoa katika mataifa yote, na katika mahali pote, nilikowafukuza, asema Bwana; nami nitawaleta tena, hata mahali ambapo kutoka hapo naliwafanya mchukuliwe mateka.

MAMBO MATATU
*     Yajue mawazo ya Mungu juu ya kusudi unalolitumikia au unalojiandaa kulitumikia. (Mawazo Mungu anayokuwazia)
-       1kor. 2:12 Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, MAKUSUDI tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu.
-       Zaburi 92:5 Ee Bwana, jinsi yalivyo makuu matendo yako! Mawazo yako ni mafumbo makubwa.
-       Mika 4:12 Lakini wao hawayajui mawazo ya Bwana, wala hawafahamu shauri lake; kwa maana amewakusanya kama miganda sakafuni.
-       Zaburi 139:17-18 Mungu, fikira zako zina thamani nyingi kwangu; Jinsi livyo kubwa jumla yake! Kama ningezihesabu ni nyingi kuliko mchanga; Niamkapo nikali pamoja nawe.
*     Hakikisha unamuona Mungu kabla hujaondoka kupiga hatua/ wewe binafsi uhakikishwe katika hilo unaloliendea.
-       Kutoka 33:15 Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa.
-       Mathayo 12:30 Mtu asiye pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya.
-       KUTOKA 3:7 – 14
Bwana akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi. Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa. Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri. Musa akamwambia Mungu, Mimi ni nani, hata niende kwa Farao, nikawatoe wana wa Israeli watoke Misri? Akasema, Bila shaka mimi nitakuwa pamoja nawe; na dalili ya kuwa nimekutuma ndiyo hii; utakapokuwa umekwisha kuwatoa hao watu katika Misri, mtamwabudu Mungu katika mlima huu. Musa akamwambia Mungu, Tazama, nitakapofika kwa wana wa Israeli, na kuwaambia, Mungu wa baba zenu amenituma kwenu; nao wakaniuliza, Jina lake n'nani? Niwaambie nini? Mungu akamwambia Musa, MIMI NIKO AMBAYE NIKO;akasema,Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli; MIMI NIKO amenituma kwenu.

-       Mdo. 9: 3-16
Hata alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni. Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi? Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe. Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda. ……………… Basi palikuwapo Dameski mwanafunzi jina lake Anania. Bwana akamwambia katika maono, Anania.
Akasema, Mimi hapa, Bwana. Bwana akamwambia, Simama, enenda zako katika njia iitwayo Nyofu, ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu aitwaye Sauli, wa Tarso; maana, angalia, anaomba; naye amemwona mtu, jina lake Anania, akiingia, na kumwekea mikono juu yake, apate kuona tena.
Lakini Anania akajibu, Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya mengi aliyowatenda watakatifu wako Yerusalemu; hata hapa ana amri itokayo kwa wakuu wa makuhani awafunge wote wakuitiao Jina lako. Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli. Maana nitamwonyesha yalivyo mengi yatakayompasa kuteswa kwa ajili ya Jina langu.

*     Mwandalie Mungu mazingira ya kuonekana unapoendelea. –“nami nitaonekana kwenu...”
-       Mfanyie Mungu nafasi katika kutimiza kwako hayo ambayo una uhakika ni makusudi ya Mungu.
-       Ambatana na madhabahu ya Mungu
-       Mungu aone nafasi yake katika kufanikiwa kwako.
-       Tunza Ibada

Ili Mungu aonekane kwenye jambo lolote ni lazima aione heshima yake kwanza, na apewe nafasi ya kuweza kuonekana. Mwanadamu peke yake ndiye mwenye nafasi ya kumfanya Mungu ajidhihirishe katika eneo lolote. 

A Strong Marriage vs. A Good Family: Understanding God's Order

In many Christian homes, there is a deep desire to build a good family. Parents work hard to provide for their children, maintain a peaceful...

Powered By Blogger