YA NINI
KUSHINDANA NA MUNGU?
Kabla
ya kumwangalia mwanadamu labda nikukumbushe kwamba Shetani (Lucifer) ndiye
aliyekuwa wa kwanza kuinua kiburi na kushindana na Mungu. Kumbuka alikuwa Isaya 14:13 Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka
mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya
mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini.” Hiki ni kiburi cha hali ya juu sana, ndiyo maana Mungu
akakasirika akamtupa chini kuzimu na kumhukumu milele.
Shetani yeye kwa sababu
alikuwa Kerubi wa sifa kwa Mungu, tunaweza kusema hizo sifa ndizo zlizompa
kiburi hata akashindana na Mungu. Je, wewe mwanadamu wa leo ni nini kinakupa
kiburi? Je, ni mali! Kumbuka nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Mungu. Je, ni
uwezo ulionao kitaaluma? Kumbuka Mungu ndiye aliyekuumba na kukupa huo uwezo.
Je, ni sura (urembo)! Kumbuka sisi sote ni mavumbi.
Ukisoma
biblia utagundua kwamba mwanadamu amekuwa katika hali ya kutaka kushindana na
Mungu hasa kwa sababu Mungu haonekani kwa macho ya damu na nyama. Tangu Adamu
na Eva walipofanya uasi katika bustani ya Edeni, hali ya uasi iliendelea kukaa
katika moyo wa mwanadamu hata kufikia mahali pa kupata kiburi na kutaka
kushindana na Mungu.
Katika
Mwanzo 6:3, Bwana (Mungu) akasema, Roho
yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku
zake zitakuwa miaka mia na ishirini.
Ukisoma kuanzia mstari wa
kwanza utaona kwamba wanadamu waliongezeka sana, na wakazidi kufanya maasi
mengi hata kuvuruga kabisa ile mipaka ambayo Mungu amewawekea. Mstari wa 5 unasema “Bwana akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni
makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu
sikuzote.”
Mashindano haya hayakuisha, yamekuwa
yakiendelea hata katika kizazi hiki.
Tunashindana na Mungu kwa njia gani?
- Kuukosoa uumbaji wake.
Kusudi la Mungu ni kila kitu kiende kwa utaratibu aliouweka
kulingana na kusudi lake. Ila katika kizazi cha leo kuna watu ambao wamekuwa
wagumu wa kuelewa na wamekuwa wakipindua mambo. Mtume Paulo akisema na warumi
aliwazungumzia watu wa jinsi hii.
Warumi 1:26 – 27 “Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu,
hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili; wanaume
nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa,
wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao
yaliyo haki yao.” Unaona mapinduzi haya? Huku ni kushindana na Mungu.
Hapa anazungumzia maswala ya “Ushoga” ndoa za jinsia moja na kufanya mapenzi
kinyume na maumbile. Huku ni kwenda kinyume na utaratibu wa Mungu na kwa lugha
rahisi ni kushindana na Mungu. Matokeo yake ni magumu sana. Hapo juu tuliposoma
panatuweka wazi kwamba “Kuna kuachwa na Mungu” na hii ndiyo sababu ya ugumu wa
maisha duniani.
2. Kwa kupingana na neno lake.
Wako watu wengi siku hizi wanaojaribu
kulipindua neno la Mungu na kuleta mafundisho yao kulingana na matakwa yao. Hii
ni kushindana na Mungu. Lile neno alilolisema Mungu ni AMINI na KWELI, sisi
kazi yetu ni kutii tu. Tukimchukua Farao kama mfano tunaweza kuona ni jinsi
gani Mungu anavyoweza kulisimamia neno lake. Mungu anamwambia “WAPE WATU WAANGU
RUHUSA WAENDE WAKANITUMIKIE” (Kutoka 5:1, 8:1)
Ona
majibu ya Farao Kutoka 5:2 “Farao akasema, Bwana ni
nani, hata niisikilize sauti yake, na kuwapa Israeli ruhusa waende zao? Mimi
simjui Bwana, wala sitawapa Israeli ruhusa waende zao.” Hiki ni kiburi cha hali
ya juu sana, na ni hali ambayo inaweza kuonekana kwa watu wengi wenye madaraka
au utajiri. Wako watu wenye mioyo kama Farao, hawako tayari kulitii neno la Mungu.
Huku ni kushindana na Mungu!
3. Kwa kutenda dhambi (Uasi)
Katika 1Yohana 3:4 tunasoma, “Kila atendaye dhambi, afanya
uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi.” Kwa
hiyo kutenda dhambi mbali na kumtenga mtu na Mungu,
huinua pia roho ya mtu kuwa na kiburi na wakati mwingine hata kumsema Mungu
vibaya.
Roho ya kuasi ni roho mbaya sana, katika mwanzo 6 tumeona maovu wa
wanadamu yaliongezeka sana na Mungu akatangaza wazi kwamba Roho yake
haitashindana na mwanadamu.
4. Kupigana au kuwapiga vita watumishi wake.
Hili ni jambo ambalo watu katika nyakati za
leo wameliona la kawaida tu. Kumbe sio jambo la kawaida, uscheze na mpakwa
mafuta wa Mungu.
Mfalme Daudi alijua swala
na Mashihi wa Bwana kabla hata ya kuwa Mfalme. 1 Samweli 26:9 “Lakini Daudi akamwambia Abishai, Usimwangamize; kwani ni nani awezaye
kuunyosha mkono wake juu ya masihi”
Ukisoma tena, Zaburi 20:6
Daudi anaimba Zaburi na kusema “Sasa
najua kuwa Bwana amwokoa masihi wake;Atamjibu kutoka mbingu zake takatifu.”
Nakatika Zaburi 28:8 anasema “Bwana ni nguvu za watu wake, Naye ni ngome
ya wokovu kwa masihi wake.”
Tunachijifunza
hasa kwenye mistari hii ya Zaburi ni kwamba, unaposhindana na masihi au mpakwa
mafuta wa Bwana unashindana naye (Mungu) mwenyewe. Tunaliona pale Miriamu
alipojaribu kumsema vibaya Musa mtumishi wa Mungu. (Hesabu 12) Mungu alimpa
adhabu kali sana, hakutaka kusikia hata maombi ya Musa na Haruni. Miriamu
alipata Ukoma na alifungwa nje ya kambi
kwa muda wa siku saba.
Tukumbuke
pia wakati wa akina Daniel kule Babeli vile ambavyo Mungu alishughulika na watu
walioshindana na watumishi wake. Kipindi cha Akina Petro Mungu alimshughulikia.
Matendo 12:22 “Watu
wakapiga kelele, wakisema, Ni sauti ya Mungu, si sauti ya mwanadamu. Mara
malaika wa Bwana akampiga, kwa sababu hakumpa Mungu utukufu; akaliwa na chango,
akatokwa na roho.”
Ni muhimu pia tukamkumbuka Paulo wakati anajulikana kama
Sauli,aliyekuwa mkatili, akuia watu waliokuwa wanamtaja Yesu na kuamini. Ukiso
Matendo 9 utaona taarifa za Sauli. Mstari wa kwanza tunasoma, “Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza
kuwaua wanafunzi wa Bwana”
Aliua wengi lakini mwisho akakutana na Mungu akamshikisha adabu,
Mstari wa 8 na 9 tunasoma, “ Sauli
akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika
mkono wakamleta mpaka Dameski. Akawa siku tatu haoni; hali, wala hanywi.”
5. Kuabudu miungu (Kumfananisha Mungu na vitu
au watu)
Katika Warumi 1:
21-23 “kwa sababu, walipomjua Mungu
hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi
wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza.Wakijinena kuwa wenye hekima
walipumbazika; wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa
sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya
vitambaavyo.”
Kumbuka pia wakati Musa
amekwenda mlimai akawaacha Wana wa Israeli Jangwani wakiongozwa na Haruni;
kisha Haruni akawatengenezea Sanamu ya ndama ili waiabudu, Mungu alighadhibika
sana akataka kuwaangamiza wote.
Kutoka 32, ukisoma huu mlango utaona madhara
makubwa yaliyotokea kwa sababu ya jambo hili.
Waamuzi
2:12 Tunausoma wakati ambapo Israeli nao walimwacha Mungu wakaabudu sanamu, “Wakamwacha Bwana, Mungu wa baba zao,
aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya
miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao;
wakamkasirisha Bwana, akaghadhibika.
Napo
matokeo yake hayakuwa mazuri, mambo yaliwaharibikia kabisa.
6. Maneno ya Kiburi na kuingilia kazi za
madhabahu.
Jinsi
nyingine ya kushindana na Mungu ni kwa kuzungumza maneno ya kiburi, na kujiinua
juu ya Mungu. Maneno kama haya
yalimgharimu Herode, alipoongea watu wakamsifu basi ikawa ndio mwisho wake.
Mfalme Uzia naye alifanya
vizuri sana mbele za Mungu, kisha akawa na kiburi akaenda akaingilia kazi ya
makuhani; kazi ya kuvukiza uvumba madhabahuni pa Bwana. Hata alipoelekezwa na
makuhani hakutaka kusikia kabisa. Alijiona mwenye haki mahali ambapo Mungu
hakumweka. Lililomtokea mwenyewe alishika adabu.
2Nyakati 26:19-21 “ ukamtokea
ukoma katika paji la uso wake mbele ya makuhani nyumbani mwa Bwana karibu na
madhabahu ya kufukizia na …. angalia, alikuwa na ukoma pajini mwa uso, wakamtoa
humo upesi; hata na yeye mwenyewe akafanya haraka kutoka, kwa sababu Bwana
amempiga. Uzia mfalme akawa na ukoma hata siku ya kufa kwake, akakaa katika
nyumba ya pekee, kwa kuwa ni mwenye ukoma; maana alitengwa na nyumba ya Bwana”
Katika dunia
hii tuna watu wengi sana ambao wamejaa maneno ya kiburi, wengine ni kwa sababu
ya nafasi zao za uongozi, wengine ni utajiri, wengine ni umaarufu, wengine ni
sura na vile walivyo kwa nje. Watu hawa wanashindana na Mungu bila kujua nap
engine kwa kujua. Ni muhimu tukajifunza kwa hawa waliojaribu kuongea maneno ya
kiburi Mungu akashughulika nao.
Nirudie
tena swali langu la Msingi “U nani wewe unayeshindana na Mungu?” Katika mstari
wetu wa msingi tumesoma, “Ole wake ashindanaye na
Muumba wake! Kigae kimoja katika vigae vya dunia! Je! Udongo umwambie yeye
aufinyangaye; Unafanya nini? Au kazi yako, Hana mikono?”
Unapojaribu kushindana
na Mungu kumbuka mambo haya:
- Hakuna aliyewahi kushindana na Mungu akashinda
- Sisi sote kwa jinsi ya mwili ni mavumbi,tuliumbwa kwa mavumbi na huko tutarudi (mwanzo 3:16)
- Uko hivyo ulivyo kwa neema ya Mungu tu Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Mungu
- Ukigusa utukufu wa Mungu huwezi kuendele kuishi
- Tulikuja uchi na bila kitu na hatutaondoka na kitu. 1 Timotheo 6:7 “Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu”
No comments:
Post a Comment