Thursday, 17 November 2016

JE, KUNA TOFAUTI GANI KATI YA ‘CASFETA’ NA ‘CASFETA (TAYOMI)’?


Bwana Yesu Asifiwe!
Napenda kukualika katika kulitazama swali hili ambalo najua baadhi ya watu hawapendi kabisa kulisikia kwa sababu linahusu swala ambalo liliwajeruhi sana watumishi wa Mungu. Nimelileta swali hili kwa sababu ya changamoto kubwa niliyoiona na ninayoendelea kuiona kwa kizazi hiki. Katika kipindi hiki ambapo elimu imepewa kipaumbele sana, watoto wetu wanatumia muda mwingi sana mashuleni. Hivyo, kama hapatakuwa na usimamizi wa kueleweka tutawaweka katika wakati mgumu sana.

Kwanza, napenda kumshukuru sana Mungu kwa kuwepo kwa makundi haya ambayo yamefayika msaada mkubwa sana kwa maisha ya watu wengi waliopata nafasi ya kupita katika mfumo wa elimu hapa nchini kwetu. Wapo wengi walioanza maisha ya wokovu kutokana na utendaji wa makundi haya (nikiwepo mimi mwenyewe) na wengine wengi wameweza kusimama katika huduma zao na wokovu kwa ujumla kwa sababu ya kulelewa katika makundi haya.

Pili, nieleze sasa lililomo moyoni mwangu, wapendwa, “Ni muda mrefu sana nimekuwa nikishuhudia changamoto wanazokutana nazo wanafunzi wa Kipentekoste mashuleni hasa wa vikundi hivi viwili vyenye jina moja la ‘CASFETA’. Sijui kama wewe msomaji wangu kama ulishashuhudia changamoto yoyote katika makundi haya?

Naamini kama hujashuhudia inawezekana umesikia kwa mwanao au viongozi wa makanisa au hata kwa watu maeneo mbalimbali.”  Kuna maeneo mengine wanafunzi hawapatani na baadhi ya wachungaji, wengine wanagombana wao kwa wao, yaani ni vurugu tupu. Kila mmoja anateta jina la kikundi chake. Wakati natafakari hili nikakumbuka Paulo alivyosema,

“…kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu? Maana hapo mtu mmoja asemapo, Mimi ni wa Paulo; na mwingine, Mimi ni wa Apolo, je! Ninyi si wanadamu? Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye.”

Bado nikawa ninawaza, kuna nini kinachowafanya hawa watoto wetu wasipatane na wakamtumikia Mungu kwa pamoja kwa amani. Nimepata baadhi ya mambo ya kihistoria lakini bado ninaamini huu ni wakati wetu wa kulitazama jambo hili kwa upya. Kizazi kijacho kinatuhitaji sana ili kiweze kusimamia yote yaliyowekwa mbele yake kuyafanya.

Baada ya  kulitazama swala hili kwa kina, ndipo nikabaki na swali kubwa moyoni mwangu juu ya utofauti uliopo kati ya makundi haya mawili yenye jina moja. Kwa nini swali hili likanijia na kunisumbua? Nitakueleza mambo kadhaa niliyoyatafakari ili nawe uyatafakari, niayangu sio kukosoa vikundi hivi ila ni kukutazamisha hali ambayo inaweza kuwakosesha wengi mbingu kama hatutaishughulikia mapema. 

JINA LA MAKUNDI HAYA
Kinachonishangaza hapa ni kwamba makundi haya yanayojihesabu kuwa makundi mawili yenye lengo la kuwalea wanafunzi wa Kipentekoste wawapo masomoni yanaitwa kwa jina moja yaani CASFETA (Christ’s Ambassadors Students’ Fellowship of Tanzania). Sasa inakuwaje makundi tofauti yakaitwa kwa jina moja? Najua majibu yapo kutokana na historia ya makundi haya, ila nakuuliza ili uweze kutafakari kwa upana zaidi. Je, ilikuwaje jina moja likasimamia maono ya aina mbili tofauti?


       2.  MAONO NA UTENDAJIKAZI
Katika uzoefu wangu wa miaka zaidi ya 10 masomoni yakiwepo yale ya Kidato cha kwanza hadi cha nne (O-Level), ya kidato cha tano na sita (A-Level) pamoja nay ale ya Chuo kikuu miaka mitatu (UDSM) nimekuwa nikijifunza sana mambo mengi katika makundi yote mawili. Mwisho nikagundua kwamba haya makundi yana maono yanayofanana na yanafanya kazi katika msingi mmoja huku wakitumia mbinu zinazofanana katika usiamamizi na uendeshaji wa ibada.

       3. WASHIRIKI WA KILA KUNDI
Kila kundi linadai kwamba linafanya kazi na wanafunzi wa makanisa yote ya Kipentekoste yaani EAGT, TAG, FPCT, KLPT, PENTEKOSTE PEFA, PENTEKOSTE HOLINESS NA MENGINE MENGI, kwa kifupi ni yale makanisa ambayo yapo kwenye umoja wa makanisa ya Kipentekoste (PCT). Kwa hiyo mshiriki ni lazima awe amebatizwa kwa maji tele, na awe anaabudu katika moja ya makanisa ya Kipentekoste. Kwa hiyo katika makundi yote mawili utakuta mchanganyiko wa wanafunzi wa madhehebu mbalimbali ya Kipentekoste.

         4. MSIMAMO WA KIIMANI
Kama nilivyosema kwenye swala la washiriki kwamba wote ni wa Imani ya Kipentekoste, yaani wanasimamia misingi ya Kipentekoste wakisistiza hasa ile yenye utata kwa baadhi ya watu mfano Ujazo wa Roho Mtakatifu na kunena kwa lugha mpya, Ubatizo wa maji tele na ule wa kuukiri wokovu wazi wazi. Viongozi na washiriki wote katika makundi haya ni lazima asimamie misingi hii kuhakikisha inakuwa hai kwenye maisha yao ya kila siku yaani, wajazwe nguvu za Roho Mtakatifu, wanene kwa lugha mpya na ni lazima wawe wamebatizwa kwa maji tele kama maandiko yasemavyo.

      5.  MISISTIZO YA MSINGI (Mambo ya muhimu)
Makundi yote mawili yameweka msisitizo mkubwa kwenye swala Utakatifu, Neno la Mungu, Maombi, Utumishi wa mtu mmoja mmoja na wa kikundi kama viungo katika mwili wa Kristo, Mafanikio ya kimasomo kama sehemu ya kumtangaza Kristo, Malezi ya kiroho makanisani (Kila mshiriki ni lazima awe na kanisa linalomlea kiroho), Utoaji wa kibiblia (Hasa Fungu la 10) na mengine.

Baada ya kuyaangalia mambo haya pamoja na mimi japo kwa ufupi naamini na wewe umeanza kujiuliza swali nilililojiuliza, “Kwani kuna tofauti gani?” Je, unayo majibu ya Swali hili? Kama unazo hebu zipime na kuziangalia tena mara mbili mara tatu.

Hebu nikushirikishe changamoto chache nilizoziona kwa kuwepo kwa makundi haya mawili yenye jina moja.
                 i.          Migogoro kati ya viongozi
Nimeshuhudia migogoro ya maneno na ile ya kimya kimya kati ya viongozi wengi wa makundi haya, hasa kwa yale yanayofanya kazi kwenye taasisi moja (Shule au Chuo). Migogoro hii imekuwa ikiibuka hasa kwenye maeneo mbalimbali likiwemo eneo la washiriki ambapo baadhi ya viongozi wamekuwa wakinyang’anyana washiriki na wengine kujitahidi kuwajengea washiriki wake maneno mabaya kuhusu kundi la pili ili wahame (kuwalinda). Kila kundi linajitahidi kuonyesha utofauti wake ambao kiuhalisia hauonekani au hauna nguvu kubwa.
               ii.          Kutangatanga kwa vijana waliookoka mashuleni na vyuoni
Kwa sababu wengi huwa hawaoni tofauti kati ya makundi haya mawili, wengi huwa na uhuru wa kwenda kundi lolote kati ya haya mawili. Mwingine utakuta ameshiriki kwenye makundi haya kwa nyakati tofautitofauti kutokana na anavyoona mwenyewe.
              iii.          Mwonekano kwa wasiomjua Mungu na waongofu wapya
Wengi huwa katika maswali mengi wakijiuliza juu ya tofauti iliyopo kati ya makundi haya, wakati mwingine viongozi wa makundi hutumia muda mwingi kuwaelimisha juu ya utofauti huo ili kuweza kuwajengea msimamo badala ya kuwalea katika misingi ya kibiblia.
              iv.          Walezi na wadau mbalimbali wa Injili kwa wanafunzi na vijana
Changamoto hii hutokea pale ambapo utakuta mtumishi wa Mungu amepata maono ya kuwafikia wanafunzi wa kipentekoste kwa umoja wao. Hapa ni lazima aulizwe unawatafuta wa CASFETA ipi? Na hili huleta ugumu pia katika kuwaunganisha na kuwaleta pamoja.
               v.          Changamoto kwenye uanzishwaji wa matawi mashuleni
Tumeshuhudia migongano mingi kwenye hili eneo, ambapo utakuta CASFETA iliyotangulia inajitahidi kuipiga vita inayoingia ili isiwavuruge washiriki wake. Japo kwenye baadhi ya maeneo kuna makubaliano yanayofanyika bado hakupo kutazamana vizuri kwa makundi haya.
Katika kutafakari nikasema, “Sasa ni nini sababu ya utofauti huu? Au ni nini Tatizo?
Baadhi ya watu wakasema “tatizo ni waanzilishi wake”, nami nikasema “kwani hawa waanzilishi sio Wapentekoste? Hawajatoka kwenye makanisa haya ya kipentekoste?” nikagundua kwamba wote ni wapentekoste wazuri.

      Wengine wakasema “labda ni Madhehebu wanayotoka hao washiriki”, hapa napo nikajiuliza “kwani makundi haya hayana watu kutoka madhehebu mbali mbali?” (Nikagundua wala hakuna ubaguzi wa kidhehebu kwenye makundi haya)

Wengine wakasema tofauti inatokana na walezi wa makundi haya: yaani CASFETA inalelewa na Kanisa la TAG (Tanzania Assemblies of God) na CASFETA (TAYOMI) inalelewa na Tanzania Youth Ministries (TAYOMI). Kwa upande wangu nikajiuliza kuna tofauti gani ya malezi kati ya walezi hawa? Je, Wanafunzi hawa si wa makanisa yote ya Kipentekoste? Japo baadhi ya makanisa nayo yameshaanzisha vyombo vyao. Je, hii roho ya kuwabagua watoto huku tukiwaita jina moja ilitoka wapi? Je, wokovu wetu si mmoja (imani moja, ubatizo mmoja, Roho mmoja) au kuna nini kimefichika?

     Wengine wakasema ni matunda ya ule mgogoro uliokuwepo kati TAG na EAGT kwenye miaka ya 1980 na 90, bado hapa nikajiuliza kwa hiyo ile roho ya matengano hakufa bado? Ni kweli kwamba ndiyo inayoendelea kukitafuna hata kizazi hiki ambacho hakina hatia (Hakikuwepo wakati wa mgogoro)? Bado sikuweza kukubaliana nao asilimia mia moja.

    Hebu sasa nikuulize na wewe mpendwa, ikiwa ni mchungaji, Askofu, mwimbaji, kiongozi wa CASFETA mstaafu, Mwana-CASFETA, mshirika wa kanisa la Kipentekoste na mdau mwingine yeyote unayejishughulisha na malezi ya wanafunzi mashuleni. Je, Kuna tofauti gani kati ya CASFETA na CASFETA (TAYOMI)? 

Mimi ninawalilia watoto wanaopigana vita isiyowahusu. Au niseme, "baba za watu wamekula zabibu kali, na meno ya watoto wao yametiwa ganzi." Matengano haya yanawatesa watoto wetu. Chuki ya CASFETA na CASFETA (TAYOMI) haina Mungu ndani yake. Sumu hii ni lazima itafutiwe dawa, ili kuokoa maisha ya vijana mashuleni. Wachungaji wengi wanawapiga vita wanafunzi kwa sababu ya chuki kati ya makundi haya mawili. Kanisa la Kristo Yesu liko wapi katika mashindano na malumbano. 

Hakunatofauti kati ya CASFETA na CASFETA (TAYOMI), ni lazima watoto wetu wajue Kristo hajagawanyika. Wote ni wa Kristo, Kristo ni mmoja. Tutumike katika upendo, na wazazi wa kiroho (Maaskofu na Wachungaji) msaidie kusimamia jambo hili. Huduma nyingi zinazimwa kwa sababu ya mitazamo hasi iliyojengeka katika makundi haya.

"Eee Mungu likumbuke kanisa la Tanzania, Wakumbuke wanafunzi wetu mashuleni, na wasaidie viongozi wetu walione kusudi lako kwa watoto na vijana walio mashuleni."

Na Mwl. S.S.Michael
Simu: 0713511544 (Whatsapp)
AGM - International.


8 comments:

  1. Swali hili ukitaka kujibu ni rahisi sana kwanza lazima ujiulize je? Mwanzilishi wa casfeta ni nani? Na wa casfeta tayomi ni yupi? Na je tayomi chimbuko lake lilitoka wapi?

    ReplyDelete
  2. Tofauti Kati ya casfeta na casfeta Tayomi n nyingi Sana
    1: casfeta ( IPO chini ya utawala WA TAG na inasadikika kwamba ni chama cha vjana ndani ya kanisa LA TAG yaan Kwa maana nyingn N (C.A)

    Lakini Casfeta Tayomi Chama kilicho chini ya uongozi WA Tayomi ambapo Tayomi n viongozi wanaosimamia Casfeta, vlevle Casfeta Tayomi n mkusanyiko WA WA wanafunzi /wanachuo wote wa makanisa yote ya kpentecoste yaani PAG, FPCT, KLPA,EAGT n. K, wenye lengo LA kukuza huduma na vpaji vya vjana ambao wapo shuleni na vyuoni, mm n mwanaTayomi.

    ReplyDelete
  3. Binafsi sioni umuhimu wa kuwepo tofauti tunazolazimishwa kuziona kuwa zipo, mimi nachofikiri ni viongozi wetu wa makanisa haya PAG, TAG, EAGT, KLPTA, n.k kukaa chini na kutafakari kwa upya waone wanakowapeleka watoto na vijana wa kizazi kijacho. Haya ya CASFETA na CASFETA TAYOMI ndo yameleta migogoro mikubwa hadi kugawanyika kwa makanisa, utakuta makanisa ya kilokole ni ni utitili na yote ukichunguza yanalengo moja, sema hawaweki bayana tu, utofauti ni kutaka sadaka tu hakuna kingine, na suala la sadaka ndo lililosababisha maana kila mmoja anatizama ananufaikaje, akiona haimnufaishi anabuni njia ya kumnufaisha, wachungaji wengi wamebaki kutizama sadaka, sasa sijui ndo zinawapeleka mbinguni?

    ReplyDelete
  4. Tofauti ipo jamani. Casfeta ndo ilianza ikiwa chini ya kanisa la TAG. Lakini kiongozi mmoja wapo wa TAG alijitenga na ushirika huu (Joseph Justine)akaanzisha Casfeta Tayomi. Hivyo akaacha kuhudumu Casfeta iliyochini ya TAg akaanzisha Casfeta Tayomi. Japo lengo ni lile lile la kumwabudu Mungu na malengo mengine lakini Wabeba maono ya Casfteta bado ni viongozi wa TAG. Ipo chini ya idara ya CA's.

    ReplyDelete
    Replies
    1. SASA KAMA IPO CHINI YA CAs ya kanisa la TAG,KWA MASHULENI HUONI INALETA MKANGANYIKO?JE!WALE WATOKAO MADHEHEBU TOFAUTI NA TAG UTAWAWEKA WAPI?

      Delete
  5. Hapo mkurugenzi wa Tayomi na askofu wa T.A.G wakae meza moja wazungumze mtoa post naomba kama utaweza kufanya hivyo ndo utakuwa umesaidia T.A.G askofu mkuu kabisa na Katibu wake na TAYOMI nao mkurugenzi mtendaji na Katibu Mkuu wake wakae meza moja tuone shida ipo wapi

    ReplyDelete
  6. Enter your comment...
    Niliwahi kukutana na hii changamoto lakini sikuitilia maanani yan ndo nimekuja kuifatilia ukubwani.

    ReplyDelete

MWANAUME KWENYE NAFASI YA "MUME"

Mume ni mwanaume aliyeoa kwa kuzingatia vigezo na taratibu za kijamii, kishria na za kiroho. Mume si rafiki wa kiume (boyfriend), hawara, wa...

Powered By Blogger