Bwana
Yesu Asifiwe!
Napenda
kukualika katika kulitazama swali hili ambalo najua baadhi ya watu hawapendi
kabisa kulisikia kwa sababu linahusu swala ambalo liliwajeruhi sana watumishi
wa Mungu. Nimelileta swali hili kwa sababu ya changamoto kubwa niliyoiona na
ninayoendelea kuiona kwa kizazi hiki. Katika kipindi hiki ambapo elimu imepewa
kipaumbele sana, watoto wetu wanatumia muda mwingi sana mashuleni. Hivyo, kama
hapatakuwa na usimamizi wa kueleweka tutawaweka katika wakati mgumu sana.
Kwanza,
napenda kumshukuru sana Mungu kwa kuwepo kwa makundi haya ambayo yamefayika
msaada mkubwa sana kwa maisha ya watu wengi waliopata nafasi ya kupita katika mfumo
wa elimu hapa nchini kwetu. Wapo wengi walioanza maisha ya wokovu kutokana na
utendaji wa makundi haya (nikiwepo mimi mwenyewe) na wengine wengi wameweza
kusimama katika huduma zao na wokovu kwa ujumla kwa sababu ya kulelewa katika
makundi haya.
Pili,
nieleze sasa lililomo moyoni mwangu, wapendwa, “Ni muda mrefu sana nimekuwa
nikishuhudia changamoto wanazokutana nazo wanafunzi wa Kipentekoste mashuleni
hasa wa vikundi hivi viwili vyenye jina moja la ‘CASFETA’. Sijui kama wewe msomaji wangu kama ulishashuhudia
changamoto yoyote katika makundi haya?
Naamini kama hujashuhudia inawezekana
umesikia kwa mwanao au viongozi wa makanisa au hata kwa watu maeneo mbalimbali.”
Kuna maeneo mengine wanafunzi hawapatani
na baadhi ya wachungaji, wengine wanagombana wao kwa wao, yaani ni vurugu tupu.
Kila mmoja anateta jina la kikundi chake. Wakati natafakari hili nikakumbuka
Paulo alivyosema,
“…kwa
maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna
husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa
jinsi ya kibinadamu? Maana hapo mtu mmoja asemapo, Mimi ni wa Paulo; na
mwingine, Mimi ni wa Apolo, je! Ninyi si wanadamu? Basi Apolo ni nani? Na Paulo
ni nani? Ni wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi
nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si
kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye.”
Bado
nikawa ninawaza, kuna nini kinachowafanya hawa watoto wetu wasipatane na
wakamtumikia Mungu kwa pamoja kwa amani. Nimepata baadhi ya mambo ya kihistoria
lakini bado ninaamini huu ni wakati wetu wa kulitazama jambo hili kwa upya.
Kizazi kijacho kinatuhitaji sana ili kiweze kusimamia yote yaliyowekwa mbele
yake kuyafanya.
Baada
ya kulitazama swala hili kwa kina, ndipo
nikabaki na swali kubwa moyoni mwangu juu ya utofauti uliopo kati ya makundi
haya mawili yenye jina moja. Kwa nini swali hili likanijia na kunisumbua?
Nitakueleza mambo kadhaa niliyoyatafakari ili nawe uyatafakari, niayangu sio kukosoa vikundi hivi ila ni kukutazamisha hali ambayo inaweza kuwakosesha wengi mbingu kama hatutaishughulikia mapema.
JINA LA MAKUNDI HAYA
JINA LA MAKUNDI HAYA
Kinachonishangaza
hapa ni kwamba makundi haya yanayojihesabu kuwa makundi mawili yenye lengo la
kuwalea wanafunzi wa Kipentekoste wawapo masomoni yanaitwa kwa jina moja yaani
CASFETA (Christ’s Ambassadors Students’ Fellowship of Tanzania). Sasa inakuwaje
makundi tofauti yakaitwa kwa jina moja? Najua majibu yapo kutokana na historia
ya makundi haya, ila nakuuliza ili uweze kutafakari kwa upana zaidi. Je,
ilikuwaje jina moja likasimamia maono ya aina mbili tofauti?
2. MAONO NA UTENDAJIKAZI
Katika
uzoefu wangu wa miaka zaidi ya 10 masomoni yakiwepo yale ya Kidato cha kwanza
hadi cha nne (O-Level), ya kidato cha tano na sita (A-Level) pamoja nay ale ya
Chuo kikuu miaka mitatu (UDSM) nimekuwa nikijifunza sana mambo mengi katika
makundi yote mawili. Mwisho nikagundua kwamba haya makundi yana maono
yanayofanana na yanafanya kazi katika msingi mmoja huku wakitumia mbinu
zinazofanana katika usiamamizi na uendeshaji wa ibada.
3. WASHIRIKI WA KILA KUNDI
Kila
kundi linadai kwamba linafanya kazi na wanafunzi wa makanisa yote ya
Kipentekoste yaani EAGT, TAG, FPCT, KLPT, PENTEKOSTE PEFA, PENTEKOSTE HOLINESS
NA MENGINE MENGI, kwa kifupi ni yale makanisa ambayo yapo kwenye umoja wa
makanisa ya Kipentekoste (PCT). Kwa hiyo mshiriki ni lazima awe amebatizwa kwa
maji tele, na awe anaabudu katika moja ya makanisa ya Kipentekoste. Kwa hiyo
katika makundi yote mawili utakuta mchanganyiko wa wanafunzi wa madhehebu
mbalimbali ya Kipentekoste.
4. MSIMAMO WA KIIMANI
Kama
nilivyosema kwenye swala la washiriki kwamba wote ni wa Imani ya Kipentekoste,
yaani wanasimamia misingi ya Kipentekoste wakisistiza hasa ile yenye utata kwa
baadhi ya watu mfano Ujazo wa Roho Mtakatifu na kunena kwa lugha mpya, Ubatizo
wa maji tele na ule wa kuukiri wokovu wazi wazi. Viongozi na washiriki wote
katika makundi haya ni lazima asimamie misingi hii kuhakikisha inakuwa hai
kwenye maisha yao ya kila siku yaani, wajazwe nguvu za Roho Mtakatifu, wanene
kwa lugha mpya na ni lazima wawe wamebatizwa kwa maji tele kama maandiko
yasemavyo.
5. MISISTIZO YA MSINGI (Mambo ya muhimu)
Makundi
yote mawili yameweka msisitizo mkubwa kwenye swala Utakatifu, Neno la Mungu,
Maombi, Utumishi wa mtu mmoja mmoja na wa kikundi kama viungo katika mwili wa
Kristo, Mafanikio ya kimasomo kama sehemu ya kumtangaza Kristo, Malezi ya
kiroho makanisani (Kila mshiriki ni lazima awe na kanisa linalomlea kiroho),
Utoaji wa kibiblia (Hasa Fungu la 10) na mengine.
Baada
ya kuyaangalia mambo haya pamoja na mimi japo kwa ufupi naamini na wewe umeanza
kujiuliza swali nilililojiuliza, “Kwani kuna tofauti gani?” Je, unayo majibu ya
Swali hili? Kama unazo hebu zipime na kuziangalia tena mara mbili mara tatu.
Hebu
nikushirikishe changamoto chache nilizoziona kwa kuwepo kwa makundi haya mawili
yenye jina moja.
i.
Migogoro kati ya viongozi
Nimeshuhudia
migogoro ya maneno na ile ya kimya kimya kati ya viongozi wengi wa makundi
haya, hasa kwa yale yanayofanya kazi kwenye taasisi moja (Shule au Chuo).
Migogoro hii imekuwa ikiibuka hasa kwenye maeneo mbalimbali likiwemo eneo la
washiriki ambapo baadhi ya viongozi wamekuwa wakinyang’anyana washiriki na
wengine kujitahidi kuwajengea washiriki wake maneno mabaya kuhusu kundi la pili
ili wahame (kuwalinda). Kila kundi linajitahidi kuonyesha utofauti wake ambao
kiuhalisia hauonekani au hauna nguvu kubwa.
ii.
Kutangatanga kwa vijana waliookoka mashuleni na
vyuoni
Kwa
sababu wengi huwa hawaoni tofauti kati ya makundi haya mawili, wengi huwa na
uhuru wa kwenda kundi lolote kati ya haya mawili. Mwingine utakuta ameshiriki
kwenye makundi haya kwa nyakati tofautitofauti kutokana na anavyoona mwenyewe.
iii.
Mwonekano kwa wasiomjua Mungu na waongofu wapya
Wengi
huwa katika maswali mengi wakijiuliza juu ya tofauti iliyopo kati ya makundi
haya, wakati mwingine viongozi wa makundi hutumia muda mwingi kuwaelimisha juu
ya utofauti huo ili kuweza kuwajengea msimamo badala ya kuwalea katika misingi
ya kibiblia.
iv.
Walezi na wadau mbalimbali wa Injili kwa wanafunzi
na vijana
Changamoto
hii hutokea pale ambapo utakuta mtumishi wa Mungu amepata maono ya kuwafikia
wanafunzi wa kipentekoste kwa umoja wao. Hapa ni lazima aulizwe unawatafuta wa
CASFETA ipi? Na hili huleta ugumu pia katika kuwaunganisha na kuwaleta pamoja.
v.
Changamoto kwenye uanzishwaji wa matawi mashuleni
Tumeshuhudia
migongano mingi kwenye hili eneo, ambapo utakuta CASFETA iliyotangulia
inajitahidi kuipiga vita inayoingia ili isiwavuruge washiriki wake. Japo kwenye
baadhi ya maeneo kuna makubaliano yanayofanyika bado hakupo kutazamana vizuri
kwa makundi haya.
Katika
kutafakari nikasema, “Sasa ni nini sababu ya utofauti huu? Au ni nini Tatizo?
Baadhi
ya watu wakasema “tatizo ni waanzilishi
wake”, nami nikasema “kwani hawa waanzilishi sio Wapentekoste? Hawajatoka
kwenye makanisa haya ya kipentekoste?” nikagundua kwamba wote ni
wapentekoste wazuri.
Wengine
wakasema “labda ni Madhehebu wanayotoka
hao washiriki”, hapa napo nikajiuliza “kwani makundi haya hayana watu kutoka
madhehebu mbali mbali?” (Nikagundua wala hakuna ubaguzi wa kidhehebu kwenye
makundi haya)
Wengine
wakasema tofauti inatokana na walezi wa makundi haya: yaani CASFETA inalelewa
na Kanisa la TAG (Tanzania Assemblies of God) na CASFETA (TAYOMI) inalelewa na
Tanzania Youth Ministries (TAYOMI). Kwa upande wangu nikajiuliza kuna tofauti
gani ya malezi kati ya walezi hawa? Je, Wanafunzi hawa si wa makanisa yote ya
Kipentekoste? Japo baadhi ya makanisa nayo yameshaanzisha vyombo vyao. Je, hii
roho ya kuwabagua watoto huku tukiwaita jina moja ilitoka wapi? Je, wokovu wetu si mmoja (imani moja, ubatizo mmoja, Roho mmoja) au kuna nini kimefichika?
Wengine
wakasema ni matunda ya ule mgogoro uliokuwepo kati TAG na EAGT kwenye miaka ya 1980
na 90, bado hapa nikajiuliza kwa hiyo ile roho ya matengano hakufa bado? Ni
kweli kwamba ndiyo inayoendelea kukitafuna hata kizazi hiki ambacho hakina
hatia (Hakikuwepo wakati wa mgogoro)? Bado sikuweza kukubaliana nao asilimia
mia moja.
Hebu
sasa nikuulize na wewe mpendwa, ikiwa ni mchungaji, Askofu, mwimbaji, kiongozi
wa CASFETA mstaafu, Mwana-CASFETA, mshirika wa kanisa la Kipentekoste na mdau
mwingine yeyote unayejishughulisha na malezi ya wanafunzi mashuleni. Je, Kuna tofauti gani kati ya CASFETA na
CASFETA (TAYOMI)?
Mimi ninawalilia watoto wanaopigana vita isiyowahusu. Au niseme, "baba za watu wamekula zabibu kali, na meno ya watoto wao yametiwa ganzi." Matengano haya yanawatesa watoto wetu. Chuki ya CASFETA na CASFETA (TAYOMI) haina Mungu ndani yake. Sumu hii ni lazima itafutiwe dawa, ili kuokoa maisha ya vijana mashuleni. Wachungaji wengi wanawapiga vita wanafunzi kwa sababu ya chuki kati ya makundi haya mawili. Kanisa la Kristo Yesu liko wapi katika mashindano na malumbano.
Hakunatofauti kati ya CASFETA na CASFETA (TAYOMI), ni lazima watoto wetu wajue Kristo hajagawanyika. Wote ni wa Kristo, Kristo ni mmoja. Tutumike katika upendo, na wazazi wa kiroho (Maaskofu na Wachungaji) msaidie kusimamia jambo hili. Huduma nyingi zinazimwa kwa sababu ya mitazamo hasi iliyojengeka katika makundi haya.
"Eee Mungu likumbuke kanisa la Tanzania, Wakumbuke wanafunzi wetu mashuleni, na wasaidie viongozi wetu walione kusudi lako kwa watoto na vijana walio mashuleni."
Na Mwl. S.S.Michael
Simu: 0713511544 (Whatsapp)
AGM - International.
Mimi ninawalilia watoto wanaopigana vita isiyowahusu. Au niseme, "baba za watu wamekula zabibu kali, na meno ya watoto wao yametiwa ganzi." Matengano haya yanawatesa watoto wetu. Chuki ya CASFETA na CASFETA (TAYOMI) haina Mungu ndani yake. Sumu hii ni lazima itafutiwe dawa, ili kuokoa maisha ya vijana mashuleni. Wachungaji wengi wanawapiga vita wanafunzi kwa sababu ya chuki kati ya makundi haya mawili. Kanisa la Kristo Yesu liko wapi katika mashindano na malumbano.
Hakunatofauti kati ya CASFETA na CASFETA (TAYOMI), ni lazima watoto wetu wajue Kristo hajagawanyika. Wote ni wa Kristo, Kristo ni mmoja. Tutumike katika upendo, na wazazi wa kiroho (Maaskofu na Wachungaji) msaidie kusimamia jambo hili. Huduma nyingi zinazimwa kwa sababu ya mitazamo hasi iliyojengeka katika makundi haya.
"Eee Mungu likumbuke kanisa la Tanzania, Wakumbuke wanafunzi wetu mashuleni, na wasaidie viongozi wetu walione kusudi lako kwa watoto na vijana walio mashuleni."
Na Mwl. S.S.Michael
Simu: 0713511544 (Whatsapp)
AGM - International.