YAPO MENGI HUTOKEA.
“Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe
kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya” 2 Wakorintho 5:17
Ni vema mtu
unapoamua kuokoka ukatambua mabadiliko ya msingi ambayo hutoe pao kwa papo
ambayo, yanakufanya kuwa mtu wa tofauti na ulivyokuwa mwanzoni. Mtu anapokubali
kuokoka, hutokea mabadiliko katika maeneo makuu manne.
A.
Mbinguni (Kwenye Ufalme wa Mungu).
Katika kitabu
cha Luka15:10 Nawaambia, Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa
ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye” Kwa hiyo kunakuwa na furaha mbinguni juu ya kurejea kwako katika Ufalme wa Mungu
(ulikuwa mwana aliyepotea) Neno linasema
“malaika wa mbinguni anafurahia” mtu anapoamua kutubu na kumrudia Mungu.
Jambo
jingine ambalo hutokea mbinguni ni, jina kuandikwa katika kitabu cha uzima. Luka
10:20 “Lakini, msifurahi kwa vile pepo
wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.”
Wanafunzi walipokuwa wanafurahia utendaji kazi wa nguvu za Mungu; Yesu
anawakumbusha kwamba jambo la kufurahia zaidi ni kule majina yao kuandikwa
mbinguni na sio mapepo kutii. Kumbuka Yesu alikuja ili aturejeshe kwa Mungu, na
majina yetu yatambulike tena mbinguni.
Ufunuo 21:27 “Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote
kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa
katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo. Hapa tunaona wenye fursa ya
kuingia mbinguni ni wale tu ambao majina yao yameandikwa kwenye Kitabu cha
uzima.
Wafilipi 4:3 “…. na wale wengine waliotenda kazi pamoja nami, ambao majina yao yamo
katika kitabu cha uzima.” Mtume Paulo anaongea kwa uhakika kabisa akijua ya
kwamba mtu anapoamua kuokoka moja kwa moja jina lake linaandikwa katika kitabu
cha Uzima.
Revelation
20:15 “Na iwapo mtu ye yote hakuonekana
ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.”
Hapa tunaona adhabu ya mtu ambaye jina lake halitaonekana kwenye kitabu cha
uzima, kwamba atatupwa kwenye ziwa la moto (Jehanamu). Jambo hili linatupa
kujipeleleza na kuona kama majina yetu kweli yameandikwa mbinguni.
Je,
utajuaje jina langu limeandikwa mbinguni? Ni rahisi tu kujua, kama umetubu
kweli na kumkiri Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako na kusimama katika
utakatifu basi jina lako litakuwepo kwenye kitabu cha Uzima. Hiki ni kitabu cha
watakatifu, yaani wale waliokubali kusafishwa kwa Damu ya Yesu kama tulivyoona
kwamba Yesu alijisafishia watu ili wawe milki yake. Tena Roho Mtakatifu wa
Mungu atakushuhudi ndani yako.
Tatu, unapata kibali cha kupokea siri na Baraka
za rohoni ndani yake Kristo. Mtu
anapokuwa hajaokoka anakuwa amefungwa na katika utu wa kale ambao hauna
ushirika na Mungu. Hivyo anakuwa hana uwezo wa kurithi Baraka pamoja na Yesu.
1Korintho14 Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu;
maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa
jinsi ya rohoni.
Kwa hiyo kwa
kumpokea Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wetu, tumefungua mlango wa kupokea kipawa
cha Roho Mtakatifu na kupokea nguvu na karama mbalimbali kutoka kwa Mungu.
Nne, Kumbukumbu za matendo yako mabaya zinafutwa,
na kuanza ukurasa mpya wa maisha. Maandiko yanatuthibitishia kwamba hakuna
dhambi inayokumbukwa tena, baada ya kutubu kweli na kumwamini Yesu. Katika
Isaya 1:18
“Mungu anasema, Haya, njoni,
tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu Sana, zitakuwa nyeupe
Kama theluji; zijapokuwa nyekundu Kama bendera, zitakuwa kama sufu”.
Isaya 43: 25 “Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu
mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako.”
1Yohana
1:9 “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni
mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu
wote.”
Kwa
hiyo katika maneno haya tunapata ujasiri wa moja kwa moja kwamba mtu
anapokubali kutubu dhambi na kuziacha kisha kumwishia Kristo katika maisha yake
yote, maovu na dhambi zote alizozitenda vinafutwa kabisa. Tena, Mungu anasema
hatazikumbuka tena na hakutakuwa na hukumu tna juu yake.
Tano, Uhusiano wako
na Mungu unarejea upya; Kumbuka Yesu alikuja kufanya upatanisho kati ya
mwanadamu mwenye dhambi na Mungu Mtakatifu. 2
Wakorintho 5:19 yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu
na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la
upatanisho.
B.
Kwenye
mazingira yake (Duniani)
Unakuwa
wakili wa Mungu katika dunia hii. Katika 1 Wakorintho 4:1 Paulo anasema, “Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu.” Tena
Mtume Petro anasema, “Kila mmoja kwa
kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu” 1 Petro 4:10. Kwa hiyo ni lazima ujijue kwamba Mungu anataka
akutumie kama mwakilishi wake hapa duniani katika eneo alilokuweka.
Unarejeshewa
mamlaka ya kutawala na kumiliki pamoja na Kristo Yesu, Ufunuo 5:9-10 “Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa
hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu
kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa,ukawafanya kuwa
ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki
juu ya nchi.”Kwa hiyo, tunapokuwa ndani ya Kristo tunakuwa tumerejeshewa
ile mamlaka tuliyoipoteza kupitia dhambi ya Adamu katika bustani ya Edeni.
Unakuwa adui wa
dunia/unatengwa na dunia. 1Yohana 2:15 “Msiipende
dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. Maana kila
kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha
uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na
tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.”
Warumi 8:7 “Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya
Mungu, kwa maana haitii sheria ya
Mungu, wala haiwezi kuiti.”
Yakobo 4:4 “Enyi
wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia
hujifanya kuwa adui wa Mungu.”Kumbe Mungu anatutaka tukajitenge na uovu
wa kila namna na kuuvaa utakatifu pamoja na Kristo.
C.
Kwenye maisha
binafsi
Unakuwa kiumbe
kipya. 2 Wakorintho 5:17 “Hata imekuwa, mtu
akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.”Hapa
tunaelezwa wazi kabisa kwamba ndani ya Yesu tunakuwa viumbe vipya, tena yale
mambo ya kale (ya dunia) yamepita.
Unafanyika
mtoto/mwana wa Mungu. Yohana 1:12 “Bali wote
waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto
wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake.” Warumi 8:16 “Roho
mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu.” Ni muhimu sana ukajua kuwa sasa wewe ni mtoto
wa Mungu, na Mungu ni Baba yako.
Unapata raha
nafsini baada ya kuondolewa mizigo na kusamehewa dhambi. Mathayo 11:29 “Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni
mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu” Tena katika Warumi
6:22 Mtume Paulo anazungumza juu ya kuwekwa huru mbali na dhambi, “Lakini sasa mkiisha kuwekwa huru, na kuwa
mbali na dhambi, na kufanywa watumwa wa Mungu, mnayo faida yenu, ndiyo
kutakaswa, na mwisho wake ni uzima wa milele.”
Neema ya
kuwekwa huru kutoka kwenye vifungo inakuwa juu yako. Wakolosai 1:13 Naye alituokoa
katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa
pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi” Unapokuwa
ndani ya Kristo shetani anakuwa hana tena mamlaka ya kukaa ndani yako, hivyo
unakuwa huru mbali na aina zote za vifungo. Japo maombi huwa yanahitajika ili
mtu aweze kuwekwa huru kabisa. Yakobo anatupa kanuni moja ya msingi sana katika
maisha yetu ya wokovu; anasema, “Basi
mtiini Mungu. Mpingeni
Shetani, naye atawakimbia.” Yakobo 4:7
Mfumo wa kufikiria na kuamua unabadilika. Wakolosai 3:2 Yafikirini
yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi. Tena Paulo katika Warumi 12:2-3 anatupa ushauri wa msingi
sana, unaolenga kutusaidia katika kila maamuzi tunayofanya. “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali
mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo
mema, ya kumpendeza, na ukamilifu. Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia
kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na nia
ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani.”
Unakuwa
mbali na utumwa wa dhambi. Warumi
8:10 “Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili
wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu i hai, kwa sababu ya haki.”
Yohana 8: 31-32, 34-36 “….Ninyi
mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu
kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru. Yesu
akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. Wala
mtumwa hakai nyumbani sikuzote; mwana hukaa sikuzote. Basi Mwana akiwaweka
huru, mtakuwa huru kweli kweli.”
Mistari hii inatuonyesha kwamba tulikuwa watumwa wa dhambi lakini
sasa YESU anatuweka huru kabisa.
Unapokea vipawa na karama, pamoja na nguvu za Roho Mtakatifu.
Matendo
ya Mitume 2:38 “Petro akawaambia, Tubuni
mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi
mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.” Tena kwenye Waefeso
4:8 Paulo anasema, “Hivyo husema, Alipopaa juu aliteka mateka, Akawapa wanadamu vipawa.”
Unaanza mfumo mpya wa mahusiano. Waefeso 2:14 Kwa maana yeye ndiye
amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati
kilichotutenga.” Hapa tunaona kulikuwa na
matengano katikati ya wanadamu, ila Yesu alipokuja akajenga mahusiano upya.
Katika Mathayo tano Yesu anatoa kanuni mpya za mahusiano.
Mathayo 5:38-45
“Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa
jicho, na jino kwa jino; Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili. Na mtu atakaye
kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Na mtu atakayekulazimisha
mwendo wa maili moja, nenda naye mbili. Akuombaye,
mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo. Mmesikia kwamba imenenwa,
Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,
ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua
lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.”
Mfumo wa uchumi na kazi unabadilika. Mathayo 6:33-34 “Bali
utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi
msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku
maovu yake. Mathayo 12:30 Mtu asiye
pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya. Kwa
hiyo baada ya kuokoka Ufalme wa Mungu unakuwa mbele, na tunakusanya pamoja na
Mungu.
Tabia
za Mungu zinaanza kudhihirika ndani yako kwa msaada wa Roho mtakatifu, na tabia
za kidunia zinakosa nguvu. Wagalatia 5:22
“Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili,
uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.”
D.
Kuzimu (Kwenye
ufalme wa Shetani)
Jina linafutwa kwenye kumbukumbu za shetani. Wakolosai 1:13
Naye alituokoa katika nguvu za giza,
akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake. Kuwa
katika nguvu za giza maana yake tulikuwa katika himaya ya shetani, kumbukumbu
zetu zilionekana kwa shetani. Tunapookoka kibao kinageuka, mambo yote
yanafutwa.
Hati ya mashitaka inafutwa. Katika Wakolosai 2:14 Paulo anasema, “akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na
uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena,
akaigongomea msalabani”.
Shetani
anatangaza mpango rasmi wa kukutafuta. 1 Petro 5:8 Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba
angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Kwa hiyo ni muhimu
ukatambua kwamba, kuzimu kuna mpango maalumu umekwisha kuwekwa ili kuhakikisha
kwamba unarudi tena mikononi mwa shetani. Ni wewe sasa kusimama vizuri na Yesu
anayesema, Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote
ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe. Yohana
6:37
Kimsingi, Mambo haya yanatuonyesha kuwa
kuna mabadiliko makubwa ambayo hutokea mara tu matu anapoamua kuokoka (Kumpa
Yesu Kristo maisha yake) Mabadiliko haya ndiyo humfanya mtu aone uhalisia wa
wokovu katika maisha yake, na kumpa ujasiri wa kusimama katika upya kila siku.
Tunaambiwa kwamba Neema YA Mungu
hutufundisha kuukataa ubaya na tama za kidunia kisha tunapata kuishi kwa kiasi,
na haki na utauwa katika ulimwengu huu wa sasa. Haya ni mabadiliko makubwa
sana.
Katika
Mathayo 3:8 “Yohana akawaambia Wayahudi,
“Basi zaeni matunda yapasayo toba”
Tena Paulo anawaambia Wafilipi “Lakini
mwenendo wenu na uwe kama inavyoipasa Injili ya Kristo” (Wafilipi 1:27)
Tena kwenye Waefeso 4:22 anasema, “mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu
wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya”
2Wakorintho 5:17 inasema, “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo
amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.
Mistari hii inathibitisha zaidi na
kukazia swala la kuwa na badiliko kamili na lenye matunda yaliyokusudiwa kwa
majira na nyakati. Yaani matunda yaipasayo Toba na matunda yaipasayo Injili.
No comments:
Post a Comment