KWA NINI NIKO HAPA HAPA?
(Why Am I here?)
Hili ni swali ambalo kila mwenye akili atajiuliza akiona amekaa eneo moja kwa muda mrefu bila kuona mabadiliko chanya yaliyokusudiwa au yaliyotazamiwa. Kuna kipindi wana wa Israeli walifika mahali wakawa wanazunguka milima ya Seiri, tena kwa miaka mingi Mungu aliwatokea na kuwasaidia kwa kuwapa mwelekeo mpya. "Mlivyouzunguka mlima huu vyatosha; geukeni upande wa kaskazini." (Kumbukumbu 2:3)
Angalia maneno haya aliyoyasema mwanamashahiri mahiri William Shakespeare ‘There is nothing good or bad, but thinking makes it so.’ kwa kiswahili anasema, "Chochote kiwe kibaya au kizuri, ni mawazo au fikra hukifanya hivyo. Hakika vile unavyofikiri ndivyo utakavyojijenga. Kwani maamuzi ya mtu huongozwa na mawazo ya mtu. Mawazo duni husababisha maamuzi duni. Matendo ya mtu ya leo ni matokeo ya mawazo yake ya jana.
Biblia inazunguimza juu ya vitu ambavyo humtia mtu unajisi. "Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi." (Marko 7:23), Kwa hiyo kumbe mtu hawezi kuwa mzinzi kama mawazo ya uzinzi hayako ndani yake; tena hawezi kuwa muuaji, mwizi, mkorofi, mlafi nk nk kama hajawahi kuyawaza hayo.
Hebu nikuulize wewe unawaza nini? Unaweza ukawa unapambana na mambo fulani au tabia fulani ndani ya maisha yako bila mafanikio. Anzia kwenye kubadili jinsi unavyofikiri. Leo nakushauri kama unataka kufanya tofauti, fikiri tofauti. Fikra zako zikiwa zinawaza mambo madhaifu, ugumu, mabaya, maovu na mengine kama hayo bila shaka huweza kuyaepuka mambo haya. Mawazo ya kujidharau yakikutawala hautakaa uheshimike, hashima ya kweli, mafanikio ya kweli huanzia ndani ya mtu. Ili uwaze tofauti kuna mambo ni lazima uyape kisogo, uyaepuke kwa nguvu zote.
Epuka:
1. Kuangalia mambo yaliyopita (your past) na kuvunjika moyo. Huwezi kurudi nyuma kurekebisha makosa ila unweza kujifunza kitu cha kuzalisha (constructive) kutoka kwenye makosa au kufeli huko kulikopita. "Past is past because it has passed, future is future because it is yet to come. Nothing can be changed about past but future is your decision."
Kuangalia mambo yaliyopita sio kwamba ni vibaya kwani ni muhimu kuishi maisha ya kujitathmini, tatizo lipo kwenye kuwekeza moyo wako (fikra) zako huko. Waswahili husema, "Yaliyopita si ndwele tugange yajayo" tena wakasema"Maji yakishamwagika hayazoleki" Paulo naye akasema "Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele. (Wafilipi 3:13)
2. Kuwaza mambo manyonge. Mambo makubwa ndiyo yatakayokupa kupanuka kifikra, kiubunifu na hatimaye kiutendaji na Mafanikio. Waza mambo makubwa yanayowezekana, mwamini Mungu na kutenda kwa bidii utafanikiwa.
3. Kuwa na mawazo ya kushindwa. Mawazo ya kushindwa ni sumu ya mafanikio, hata kama umejaribu ukakwama. Jaribu tena na tena hadi uone mafanikio. Mawazo ya kushindwa yatakufanya utangetage hata kukosa kabisa mwelekeo.
4. Kuwaza maovu na mambo machafu. Mawazo machafu ni kitovu cha maamuzi mabovu. Tunza fikra zako kwa kutazama, kusoma na kusikiliza vitu vya kujenga ufahamu badala ya vitu vya kipuuzi. Soma vitabu, sikiliza wasomi na watu wenye hekima, tazama mambo mazuri achana na marafiki wabaya.
5. Kuchukulia mambo kikawaida. Kumbuka kuna leo na kesho, fanya mambo kwa umakini na maarifa. Ongeza bidii na juhudi zaidi kila siku.
6. Kufanya mambo vilevile kila siku kila wakati. Tafuta kuboresha jambo lako kila siku, litazame ujiridhishe.
Kumbuka Mungu alipomaliza kuumba ulimwengu na vitu vyote, alitazama na akaona kuwa ni vyema. Na wewe jifunze kuyatazama mambo kwa jicho la tathmini.
NENO LANGU KWAKO MPENDWA:
"FIKIRI TOFAUTI ILI UWE WA TOFAUTI".
Ili ufikiri tofauti:
1. Yakumbuke makuu ya Mungu ( Yale uliyofanikiwa) na utiwe moyo kwa hayo.
Daudi alipokuta wana wa Israeli na jeshi lote wamenywea kwa jeshi la wafilisti alifikiri tofauti na hatimaye akafanya tofauti. Alitazama mambo makuu ambayo Mungu alimtendea akatiwa nguvu akasimama kumwangusha Goliati. Unapowekeza muda wako mwing kufikiria juu ya mambo uliyoshindwa ndivyo unavyozidi kujidhoofisha.
Wekeza muda wako kuyakumbuka makuu ya Jehova, utasikia kuinuliwa sana. Kazi kubwa ya waliyoshindwa ni kutengeneza hadithi nzuri juu ya kushindwa kwao, bali waliofanikiwa hutengeneza hadithi mbaya kuonyesha sabababu zilizoshindwa kuwafanya washindwe. Majaribu kwao ni mtaji si mateso.
2. Kataa maovu kama Yusufu aliyofanya.
Uovu na dhambi vimezimisha ndoto za wengi. Wengi wameishia mahali duni na pa kukosa tumaini kwa sababu ya kuendekeza maovu. Hakuna raha wala amani kwa watenda mabaya. Mafanikio ya kweli huambatana na wenye haki, wanaowatanguliza wengine. Yusufu alimkimbia mke wa Potifa akaendelea kushikilia maono yake. Majaribu kama hayo ni mengi nyakati hizi lakini ukiamua kukimbia hakika Mungu atakupeleka kwenye ndoto zako. Uovu na nguvu ya kutawala moyo (nia, hisia, na mawazo).
3. Jifunze kutazama fursa mbalimbali na kuchukua hatua.
Usione fursa zote ni za wengine, kaa mkao kutafuta na kuchangamkia fursa. Daudi alipomwona Goliati alitafuta namna ya kuitumia ile fursa kwa kuulizia wengine. Alipochukua hatua ngumu alipanda thamani ndani ya dakika chache. Na wewe usilale, fanya kitu. Pigana na Goliati wetu nasi tutakupa heshima. Hupaswi kulazimisha kuheshmiwa kama wengi wanavyong'ang'ania heshima za vyeo, fanya kitu heshima yako itapanda yenyewe.
4. Ambatana na watu waliofanikiwa zaidi yako kifikra na kimaendeleo.
Watu waliopiga hatua wakati mwingine huwa sababu ya sisi kuvutwa na kufuata nyao zao. Wengi pia hupenda kuwainua wengine. Watu waliofanikiwa wanaweza kukujenga sana kifikra, kwani wengi huwa hawaamini katika kushindwa. Na huwa na mbinu nyingi na shuhuda zenye kujenga sana. Pia, huwa wanakutana na fursa nyingi sana.
5. Fuatilia mambo yenye kujenga (achana na mambo ya kipuuzi)
Tumia muda wako katika mambo ya kujenga, pata taarifa zenye tija. Mawazo ya wengi yamejaa mambo yasiyo na faida kwa sababu ya kusikiliza, kutazama na kusoma upuuzi. Tafuta kanda, vitabu, magazeti na sikiliza vipindi vya maana. Kuangalia ponografi, kusikiliza manyimbo ya kihuni, kushabikia mipira, kubeti, na mengine kama haya ni kupoteza muda wa thamani wa maisha yako.
6. Soma vitabu na kujifunza kila siku.
Kusoma si lazima uende shule, nunua vitabu vya kiroho, vya uchumi, vya kisiasa na vinginevyo ujiendeleze. Mawazo yako yanaweza kunolewa na watu waliofanikiwa kupitia yale waliyoandika. Usiwe mvivu wa kusoma.
8. Mtegemee Mungu na kusoma neno lake kwa bidii.
Mungu ndiye chanzo cha mafanikio yake. na kumcha yeye ni chanzo cha maarifa yote (Mith 7:7). Mtegemee Mungu, usiamgalie mazingira na kukata tamaa, Ishi ahadi za Mungu na uache kufikiri kinyonge. Mungu akiwa upande wetu hatupaswi kuogopa.
9. Sikiliza mahubiri na kanda za mambo ya kiroho.
Kusikiliza kuna nguvu kubwa sana. unaposikiliza unajipa fursa ya kufikiri na watu waliofanikiwa kupata fikra njema kutoka kwa Mungu. mahubiri yana siri kubwa sana. Pata muda usikilize na Mungu atakupa kufikiri kwa utofauti.
10. Badilisha marafiki ulionao (Achana na marafiki wasiojitambua)
Katika kitabu cha Mithali tunasoma "Chuma hunoa chuma; Ndivyo mtu aunoavyo uso wa rafiki yake." Mithali 27:17 Marafiki wa umbea, mizaha, masengenyo, wavivu, wenye wivu, walevi, wazinzi, wezi, wahuni ni kaburi wazi la ndoto zako. Hakikisha kama wewe ni chuma (Strong) unatafuta marafiki chuma ili mnoane. Marafiki wabaya huharibu tabia ya mtu mwema. Watakupotezea heshima. Huwezi kuaminika ukiwa na marafiki wasioaminika.
Uwe na marafiki wenye fikra za mafanikio, mawazo ya kujenga, wanaojiamini na wanaoamini katika kufanikiwa, wenye imani katika Mungu. Nawe utafikiri kama wao au zaidi yao na kisha utafanikiwa kama wao au zaidi yao.
Katika haya na mengine utakayojaliwa na Mungu kibinafsi, utaanza kuwaza kwa tofauti na baadaye utaamini kwa tofauti, kisha kufanya kwa tofauti na kufanikiwa kwa tofauti.
Mungu akubariki kwa kuwa sehemu ya blog hii. Karibu kwa masomo mengine.
Mwl. Stephen M. Swai
0713511544
No comments:
Post a Comment